Social Icons

Saturday 6 October 2012

MBUNGE SUGU ATAKA TRA WAMTOZE KODI RICK ROSS SHOW YA LEO


Na Mahmoud Zubeiry
MWANAMUZIKI nguli wa Hip hop Tanzania na Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Osmund Mbilinyi amewapa mwongozo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu ziara ya mwanamuziki nyota wa Hip hop Marekani, William Leonard Roberts II anayetambulika kama Rick Ross au The Boss, kwamba anastahili kulipa kodi kutokana na pato atakalaolingiza katika shoo yake ya leo.
Rick Ross atatumbuiza usiku wa leo katika tamasha la Serengeti Fiesta 2012 kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam, ambalo linaandaliwa na Prime Time Promotions na kudhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL).
Mbunge Mbilinyi ambaye anajulikana kwa majina ya kimuziki kama Mr II au Sugu, ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook; “RICKY ROSS ANAKUJA, SAWA HAINA SHIDA…ILA TUNATAKA KUJUA AMELIPWA KIASI GANI NA ATAKATWA KIASI GANI KIBAKI KWENYE KODI YA TAIFA LETU KAMA AMBAVYO MIMI NIKIENDA KUFANYA SHOW/CONCERT MAREKANI NAKATWA KODI NA SERIKALI YAO…”.
The Boss, ameahidi kukonga nyoyo za mashabiki watakaohudhuria tamasha la Serengeti Fiesta 2012 jioni ya leo kwenye viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, Dar es Salaam.
Rapa huyo, aliyefikia katika hoteli ya Hyatt, zamani Kilimanjaro Kempensky, Dar es Salaam, ambaye alizaliwa JanuarI 28, mwaka 1976 huko Carol City, Florida, Marekani alisema hayo baada ya kutua Dar es Salaam usiku wa jana.
“Rick Ross ametua na ameahidi kufanya shoo kali sana,”alisema Allan Chonjo, Meneja wa Bia ya Serengeti, wadhamini wakuu wa Fiesta.
Rapa huyo mwenye miraba minne, ambaye ana bifu kali na Curtis Jackson ’50 Cent’ aliyewahi kuzuru Tanzania pia, aliwasili Dar es Salaam usiku wa jana na anatarajiwa kuwapagawisha wapenzi wa Serengeti Fiesta kwa nyimbo kali kutoka kwenye albamu zake za Port of Miami aliyoitoa mwaka 2006, Trilla ya 2008, Deeper Than Rap ya 2009, Teflon Don ya 2010 na God Forgives, I Don't ya mwaka huu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, wadhamini wakuu wa Serengeti Fiesta 2012, Ephraim Mafuru Balozi alisema kwamba wanajisikia fahari kubwa kwa bia ya Serengeti kuwa mdhamini mkuu wa tamasha hilo kwa muda wa miaka minne sasa.
“Bia ya Serengeti inafahamika kwa umahiri wake katika ubora na ladha yake. Imejinyakulia medali za dhahabu kutoka katika mashirika ya ushindanishaji bia duniani DLG na Monde na pia ni fahari kwa kuwa bia ya kwanza Tanzania kuwa na kimea cha asilimia 100. Bia hii imejiwekea historia ya kuwa bia inayokua kwa haraka katika ujazo na thamani yake,”alisema Mafuru.
Mkurugenzi huyo aliwaomba wakazi wa Dar es Salaam kujitokeze kwa wingi jioni ya leo katika viwanja vya Leaders Club wakaburudike na muziki wa vijana wa Tanzania na pia kumshuhudia mwanamuziki Rick Ross kutoka Marekani. “Pia tunawahakikishia kwamba watapata bia ya Serengeti yenye muonekano mpya, na ladha yake ni ile ile yenye ubora thabiti. Kwa hiyo watapata bia yenye muonekano tofauti, burudani ile ile,”alisema. Mafuru aliongeza; “Tunazo Bia za aina nyingi kutoka Kampuni ya Bia ya Serengeti pia zitakuwepo kama vile; Tusker Lager, Pilsner Lager, Tusker Malt Lager, Uhuru Peak Lager, Smirnoff Ice Black na Red, na kwa wanaopendelea vinywaji vikali watapata Johnnie Walker Whisky, Smirnoff Vodka, VAT 69, Captain Morgan, Baileys na Gilbeys Gin. Pia kutakuwa na vinywaji visivyo na kilevi cha Malta Guinness na Alvaro. Tumejiandaa vya kutosha kuwapatia vinywaji hivyo kwa bei ya shilingi 1,800 tu,”alisema

No comments: