Social Icons

Wednesday 21 October 2015

FAMILIA YA DK. MAGUFULI YASEMA WATANZANIA WAMEPATA KIONGOZI MCHAPA KAZI, MWENYE MSIMAMO NA MPENDA MAENDELEO

Ikiwa una Tukiko lolote la Harusi,Msiba, Mahafali, Tamasha, Matangazo au Habari yoyote usisite kututumia kupitia whatsapp 0765056399 au Barua Pepe fredynjeje@live.com.

 
Kiongozi wa familia hiyo, Albert Michael, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geita.
---
Na Rashid Zahor, Geita.
FAMILIA ya mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli imesema Watanzania watakuwa na bahati ya kumpata kiongozi mchapakazi, mwenye msimamo na anayependa maendeleo.
Imesema iwapo Dk. Magufuli atachaguliwa kuwa rais, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii, atawaletea maendeleo makubwa kwa kuwa ni mtu mwenye msimamo, asiyeyumba na anayependa maendeleo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na kiongozi wa familia hiyo, Albert Michael, alipozungumza na waandishi wa habari mjini Geita.
Mzee Albert hakuwepo Katoma juzi wakati msafara wa Dk. Magufuli uliposimama kwa muda nyumbani kwa babu yake, ambako alipata nafasi ya kuzuru kaburi lake na la bibi yake mzaa wa baba na kuwaombea dua.
"Watanzania wasiwe na wasiwasi, Magufuli ni mtu anayependa watu na maendeleo na ni mchapakazi,"alisema Mzee Albert, alipokuwa akijibu swali kuhusu sifa za mgombea huyo tangu alipokuwa mtoto.
Aidha, Mzee Albert alisema Dk. Magufuli si mpole, sio mkali sana, lakini ni mtu mwenye msimamo na asiyeyumba katika jambo analotaka kulifanya.
Mzee Albert, ambaye ndiye aliyeachiwa mji wa Katoma kwa sasa, liliko chimbuko la ukoo wa Dk Magufuli, akiwa miongoni mwa wadogo zake marehemu baba mzazi wa mgombea huyo, alisema familia yao ipo pamoja naye na inamuombea Mungu aweze kutimiza dhamira yake ya kuwa rais wa awamu ya tano ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Ninachowahakikishia Watanzania ni kwamba Oktoba 25, watampata kiongozi bora, asiye na ubaguzi wa aina yoyote,"'alisema mzee huyo.
Akizungumzia majina ya mgombea huyo, alisema jina la Pombe alipewa na bibi yake siku alipozaliwa, kwa kuwa siku hiyo alikuwa akipika pombe. Alisema jina la Magufuli lilitokana na kupenda kwake michezo.
"Siku John alipozaliwa, bibi yake alipopelekewa taarifa, alisema 'huyo mume ni mume wangu aitwe pombe'," alisema mzee huyo, ambaye alifika Geita juzi usiku akitokea Chato.
Juzi, Dk. Magufuli alitembelea kwenye makaburi ya babu na bibi yake mzaa wa baba, eneo la Katoma, wilayani Geita Vijijini na kufanya ibada ndogo ya kuwaombea dua.
Dk. Magufuli alifika nyumbani kwa babu yake saa 6.30 mchana na kupokewa na baba yake mdogo, Sylvestr Magufuli, kabla ya kupelekwa kwenye makaburi hayo, ambako aliongoza ibada ndogo ya kuwaombea dua.
Akizungumza kwenye eneo hilo, baba huyo alisema makaburi hayo ni ya babu na bibi wa mgombea huyo pamoja na ndugu zake wengine, waliofariki dunia miaka mingi iliyopita.
Alisema asili ya ukoo wa Dk. Magufuli ni Katoma, ambako ndiko baba yake alikozaliwa kabla ya kuhamishia makazi yake Chato.
"Tumezoea kumuona ndugu yetu kwenye tv na kumsikiliza kwenye redio, leo tumefurahi kumuona yeye mwenyewe,"alisema na kuongeza kuwa wanamuombea dua kwa Mungu ili aweze kuchaguliwa kuwa rais.
Kwa upande wake, Dk. Magufuli alisema alifarijika kufika tena katika eneo hilo kwa sababu ndiko alikozaliwa na kukulia na pia ndiko ukoo wake ulikoanzia.
Dk. Magufuli alitumia fursa hiyo kuwatambulisha ndugu zake kwa wanahabari kabla ya kuingia kwenye nyumba ya familia, iliyoko umbali wa mita 30 kutoka barabara itokayo Kamanga kwenda Sengerema.
Mgombea huyo alisema jina la Pombe alipewa na bibi yake, aliyemtaja kwa jina la Anastazia, siku alipoivisha pombe yake.
Alisema babu yake, marehemu Michael, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 103 baada ya kumuuguza kwa muda mrefu akiwa Dar es Salaam na baadaye kumrejesha Katoma.
"Kwangu siku hii ni ya pekee. Nilipojua kwamba nitasafiri kwa kutumia njia hii, niliona ni lazima nipite hapa kwa sababu ndiko maisha yangu yalikoanzia,"alisema Dk. Magufuli na kusifu maendeleo yaliyopatikana katika kijiji hicho, ikiwemo nishati ya umeme.
Aliwaomba wakazi wa kijiji hicho wamuombee dua kwa Mungu ili aweze kushinda kiti cha urais, katika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, unaotarajiwa kufanyika nchi nzima Jumapili.

No comments: