Social Icons

Monday, 12 October 2015

LEO KATIKA MAHUSIANO: UNAFAHAMU NDOA SIYO MWISHO WA MATATIZO, MCHUNGUZE KWANZA.. SOMA HAPA KWA KINA UELEWE

Ikiwa una Tukiko lolote au Habari yoyote usisite kutumia whatsapp 0765056399 au Barua Pepe fredynjeje@live.com

Namshukuru Mungu kuona nina afya njema. Kabla sijaongea mengi leo nimekuja na mada hii ili kuwakumbusha wasichana wanaokimbilia ndoa halafu hawafiki mbali na ndoa zao wanaishia kuzivunja tena kwa mikiki na visasi.
Nina visa vya kijana mmoja ambaye alinisimulia kuhusiana na mkasa wake wa mapenzi na kusema kuwa yeye alikuwa si mtu wa mademu sana na alifanya hivyo kutokana na malezi aliyolelewa na wazazi wake.

“Sikuwahi kupenda kuwa na wanawake bila ndoa hivyo nilipomaliza masomo yangu na kupata kazi niliamua kumuoa msichana mmoja ambaye nilimpenda baada ya kumuona kwa harakaharaka niliona nifunge naye ndoa ili nisiharibu azma niliyojiwekea kuwa sitakuwa na mpenzi zaidi ya mke, kwenye hilo nilifeli kwa mara ya kwanza kwani nilikaa naye kwa muda wa mwaka mmoja kisha akaniacha na kunifanyia visa kibao.
“Nilizaa naye mtoto mmoja nikaona isiwe tabu huenda Mungu hakunipangia kuishi naye mpaka tunazikana hivyo niliachana naye.“Baada ya huyo nilikaa ndani ya miezi sita na kukutana na mwanamke mwingine ambaye naye niliamua kufunga naye ndoa kwani hata dini yangu ilikuwa ikiruhusu, niliishi naye kwa miaka miwili, akaanza kubadilika mara akienda kwao anajipa ruhusa ya kukaa zaidi, nikimuuliza anasema amechoka ni bora apumzike.
“Siku moja nikaamua kumchunguza na kugundua kuwa ana mwanaume ambaye anatoka naye kwa siri na akipata upenyo wa kwenda kwao ndiyo anakuwa huru zaidi kukutana na mwanaume huyo, hapo nilijikuta nachanganyikiwa na kujiona ni mtu nisiye na bahati.
“Kiukweli nimeamua kuachana na wanawake na kukaa mwenyewe kwani sijawahi kumtenda mwanamke, wao ndiyo wamekuwa wakinigeuka siku hadi siku na mwisho tunaachana.
“Nimeona nikueleze wewe Bi. Chau kwa jinsi nilivyosoma mada zako huwa nahisi zinanifariji, ” alimaliza msomaji wangu kwa kunung’unika.
Kwa mikasa hii miwili huenda ukawa umejifunza kitu msomaji, mimi ni mtu mzima mpaka nakuwa mfundaji maarufu nimekutana na mikasa mingi lakini nimegundua matatizo mengi, siku hizi ni wasichana kukubali kuolewa harakaharaka na vijana kutowachunguza wao wanaingia tu kwenye ndoa.
Ndoa inahitaji kuchunguzana kwanza
Mpaka unaingia kwenye ndoa na mtu unahitaji kumchunguza kwanza maana ule ni mkataba wa maisha lakini siku hizi wanandoa wanaamua kufunga ndoa tu ilimradi kamuona mrembo watu watamsifia au kamuona ana hela.
Unamchunguzaje sasa?
Nikisema kumchunguza simaanishi vile vijana wanavyofanya starehe na wasichana eti wanawachunguza hapana.
Namaanisha usikurupuke kufunga ndoa na mtu wakati hujamjua ana tabia gani, ukoo wao ukoje, heshima za kwao zikoje maana makabila mengine huwa ni vigumu kutulia kwenye ndoa na mume mmoja nadhani sina haja ya kuyataja lakini yapo na wengi mmeshashuhudia.
Ingawa sitaki kuongelea sana mambo ya makabila kwa sababu wengine ni hulka tu na tabia si kwa sababu ya kabila.
Wazee wa zamani walifanyaje?
Kwa wazee wa zamani, kijana alikuwa akipata mchumba wanatuma watu wanamchunguza kwa kina na kujua historia yake ya ndani zaidi.
Wazazi pia walikuwa wakitembeleana kujaribu kujuana, yote hiyo ikiwa ni njia ya kuchunguza sehemu wanapokwenda kuoa au kuolewa.Imekuwa ni tofauti sana kwa vijana wetu siku hizi wanakwambia mambo ya utandawazi mtu akikutana na mwenzake kwenye mitandao ya kijamii (Facebook) na kumpenda kwa matamanio basi anaamua kumfanya mke au mume hapo ndiyo tatizo linapoanzia.
Wazee wa zamani wamekuwa kwenye ndoa mpaka miaka hamsini kwa sababu wamejuana kiundani na kuvumiliana kwa shida na raha.
Ndoa siyo mwisho wa matatizo
Wasichana wengi hushindwa kusoma au kufanya kazi kwa kujitafutia riziki, kuna watu wanahisi akiolewa ndiyo mwisho wa matatizo, wanasahau hata ndoa ina mambo yake usipokuwa mvumilivu unaweza kujikuta unamaliza wanaume kisa matatizo.

NA GPL

No comments: