Social Icons

Thursday 23 August 2012

MUHIMU, LEO KATIKA MAHUSIANO: MAWAZO HUCHANGIA UGUMBA KWA WANAWAKE.. SOMA UELIMIKE



TAFITI umebaini kuwa wanawake wengi wenye viungo salama lakini hawazai, wana kiasi kikubwa cha homoni ya Cortisol inayoletwa na uchovu. 
Aina hii ya homoni ndiyo inayosimamisha mchakato wa uzalishaji wa mayai kwa wanawake wanaoshiriki mchezo wa riadha.
 Hivyo basi, uwiano huu wa kasoro za ukuzaji mayai kati ya wakimbia riadha na wanawake wagumba unaweka usawa baina ya uchovu mkubwa wa mazoezi ya viungo na ule uchovu unaotokana na msongo wa mawazo ya ugumba. 
Ukweli pekee ambao nimeukusudia kuuzungumza leo ni kuhusiana na wanawake wasiokuwa na matatizo ya uzazi ambao utafiti  ulioandikwa katika jarida la Minerva Ginecologica la nchini Italia unaonesha mawazo ndiyo unaochangia kwa kiasi kikubwa wanawake hao wasipate watoto licha ya kwamba kibaiolojia hawana matatizo. 
Imebainika kuwa, wanawake wengi hujisogeza wenyewe katika nguvu ya kukosa watoto kutokana na ukubwa wa kiu yao ya kupata watoto hao. 
Hawa hujiweka katika uzalishaji mkubwa wa homoni ya Cortisol ambayo huchipuka kwa kasi kutokana na msukumo wa kiu kubwa na ya haraka ya kutaka kukumbatia mwana.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hili, imebainika kuwa wagumba wengi wasiokuwa na kasoro katika viungo vyao vya uzazi wanaweza kupona au kupata watoto bila hata kupewa tiba ya miti shamba au vidonge. Tiba kubwa iliyobainishwa ni kupatiwa nasaha zitakazowaondolea mawazo tasa, wasiwasi na kutojiamini.
Ukweli wa tiba hii ya ushauri imethibitishwa hivi karibuni na kituo kimoja nchini Marekani kinachojishughulisha na utafiti wa kuzalisha watoto, ambapo majibu yake yalichapishwa katika majarida na mitandao mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa ya kituo hicho asilimia 75 ya wanawake waliokosa watoto ambao walifika kituoni hapo na kupewa ushauri walifanikiwa kuzaa baada tu ya kuhudhuria kliniki na kupewa ushauri uliowatoa katika msongo wa mawazo.
Nasaha ambazo zimekuwa zikitolewa na wataalamu hao si ngumu, bali ni zile zilizojaa maneno yenye kugeuza fikra hasi zenye kuondoa kiu kali ya kupata watoto kwa utashi na nyakati zilizopangwa na wahusika. 
Pia, wagumba hufundishwa namna ya kuepuka migogoro ya kimapenzi na kutoumizwa kupita kiasi na kejeli za watu kuhusiana na matatizo yao, huku wakijengewa imani kuwa kuzaa ni suala linalowezekana kwao, hivyo kuwafanya watupilie mbali hofu na mawazo ya wao ni wagumba. 
Lakini pamoja na nchi zilizoendelea kuwa na vituo vya kutolea nasaha kwa waathirika, bado wanasaikolojia wanakiri kwamba mtu mwenyewe anaweza kujiepusha na uchovu unaoletwa na mawazo kwa kurahisisha tatizo lake kutoka kutowezekana na kuwezekana kutatuliwa. Akili ya mtu ndiyo inayopima na kuongoza utambubuzi wa ukubwa wa tatizo na si kwamba kuna matatizo makubwa na madogo kama watu wanavyofikiria.
Mtu aliyejiwekea ukuta wa kutozaa kutokana na msongo wa mawazo yake ili aweze  kuzaa ni lazima aondoe mawazo ya kwamba yeye ni mtu asiye zaa, kwani hakuna mtu wala vipimo vilivyompa majibu ya kwamba ni mgumba.
Jambo jingine la kufanya ni kupuuza maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa watu wengine. Hii ina maana kuwa lawama zozote kutoka kwa mume/ mke au wanafamilia zinazohukumu kosa la mtu kutokuza lazima zipuuzwe na zisipewe nafasi ya kutia simanzi moyoni.
Sambamba na hilo kuna suala la wanawake kuzingatia kalenda zao kwa kujichunguza na kubaini muda muafaka wa kukutana kimwili na wanaume ili kupata matokeo mazuri ya utungishaji mimba. 
Kwa mantiki hii kuna wanandoa wengi wameshindwa kupata mtoto kwa kutozingatia siku zenye uwezekano wa kupata mimba ambazo ni siku ya 11 hadi ya 16 tangu siku ya kumaliza hedhi.


Kwa Hisani ya GPL

No comments: