Na Mwandishi Wetu
KATIKA kusherehekea sikukuu ya Iddi El Hadji, bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo 'Next Level' inatarajia kufanya onyesho la aina yake katika ukumbi wa Vatican Hotel, Sinza jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa bendi hiyo Ally Choki alisema jana kuwa onyesho hilo maalum litakalojulikana kwa jina la 'Onyesho la kuzaliwa upya' limepamgwa kufanyika kwenye ukumbi wa Vatican Hotel Sinza, jijini Dar es Salaam, siku ya Iddi.
Choki alisema onesho hilo limeandaliwa na kampuni ya Media Entertainment Group, na litakuwa na vionjo vya aina yake ili kuwapa burudani wapenzi wa muziki wa dansi nchini.
Alisema burudani hiyo ni maalumu kwa ajili ya kusindikiza sherehe ya Iddi El Hadji, lakini pia itakuwa ni maalumu kwa ajili ya kutambulisha nyimbo mpya na wanamuziki wapya waliochukuliwa hivi karibuni kutoka bendi pinzani.
Alisema onesho hilo litatumika kutangaza nyimbo zote mpya na za zamani za wanamuziki wa bendi hiyo waliotamba katika bendi mbalimbali.
Baadhi ya nyimbo mpya za bendi hiyo zinazotikisa ni pamoja na Ufisadi wa Mapenzi wa Roggart Hegga Katapila, Mtenda akitendewa wa Choki na Watu na Falsafa ya Maisha wa Ramadhani Masanja 'Jenerali Banzastone,' huku nyimbo za zamani zikiwa ni Mjini Mipango, Regina Zanzibar na nyingine tofauti tofauti alizowahi kuziimba Choki wakati akiwa na bendi za Mchinga na The African Stars,Twanga pepeta.
Aidha onyesho la Jumapili, litatumika kuwatambulisha wanamuziki wapya watano waliochukuliwa kutoka kwa bendi pinzani huku pia shoo mpya kutoka kwa wanenguaji akina Queen Aisha Madinda na Super Nyamwela waliojiunga hivi karibuni zikitolewa.
Wanenguaji hao na wanamuziki wengine, watataonesha ustadi wao katika kusakata mitindo ya Extra Bongo.
Shoo hiyo ya nguvu ya bendi hiyo itatolewa katika ukumbi huo ikiwa ni baada ya kumalizika kwa shoo ya bonanza la kila Jumapili katika uwanja wa TP uliopo Sinza darajani ambapo Extra Bongo sambamba na Bantu Group hutoa burudani katika viwanja hivyo.
"Tumepania kuwapa raha mashabiki wetu watakaofika Vatican, tunajua wengi wao watakuwa ni watu wazima, ndio sababu tumeamua ingawa ni Siku Kuu tungeweza kufanya shoo ya kiingilio tangu mchana, sisi tutatoa burudani bure pale viwanja vya TP Sinza ili watoto nao wapate raha na kuifurahia siku kuu hii.
"Lakini kwa watakaokuja ukumbini, basi watafurahia Idd kwani tutatoa shoo kali tunazotamba nazo sasa kama ile ya Mdudu, Kizigo, Vuvuzela na nyingine nyingi kwani Super Nyamwela ambaye ni kiongozi wa shoo katika bendi amepania mno kuonyesha mavituuuz siku hiyo sambamba na wanenguaji wengine," alisema Choki.
Alisema katika kuhakikisha Siku Kuu hiyo inanoga, wameamua kulialika kundi la khanga moja ama baikoko ambao bado wanaendelea na mzungumzo nao hivyo kudai kuwa shoo hiyo itakuwa ni ya kufa mtu.
No comments:
Post a Comment