Social Icons

Tuesday 17 April 2012

AUA BINTIYE KWA RISASI AKIDHANI NI NYANI

Maembe yakiwa shambani Kitui, kenya. Mkulima nchini Gambia aliua bintiye akidhani ni nyani aliyekuwa akiiba maembe yake. 

********

MSICHANA wa umri wa miaka 12 alifariki baada ya kupigwa risasi na babake aliyemdhania kuwa nyani aliyekuwa akivamia maembe yake nchini Gambia. Kisa hicho kilitokea kijijini Kerr Mot Ali kaskazini mwa taifa hilo ndogo la Afrika Magharibi Jumanne.
Msichana huyo, Hawa Mbaye, alikuwa amerudi kutoka shuleni majira ya alasiri pale alipoamua kupanda mti muembe kuchuma maembe. Gazeti la Daily Observer limeripoti kuwa nyani wamekuwa wakihangaisha wakulima wa maembe na hata kula maembe ambayo hayajaiva.
Babake msichana huyo, Mamud Mbaye, alisikikia kelele juu ya miti na akadhani kwamba nyani ambaye amekuwa akimhangaisha alikuwa amerudi. Alichukua bastola na bila kuangalia akavyatua risasi. Badala ya nyani kuanguka ardhini, Bw Mbaye alishangaa kuona msichana wake akianguka huku mwili wake ukiwa umejaa damu.
Mwili wake ulipelekwa hospitali ya Royal Victoria Teaching Hospital katika mji mkuu, Banjul, kwa uchunguzi. Waombolezaji wameendelea kufurika nyumbani kwa marehemu kutoa rambirambi.
Chanzo:Swahili Hub

No comments: