Social Icons

Wednesday, 18 April 2012

Chelsea Dhidi Ya Barcelona: Nani Atashinda Leo? ( Uchambuzi)



Na Olle Bergdahl Mjengwa,Iringa.
 
OK, leo kivumbi kitatimka. Ni mechi ya kukata na shoka; Chelsea dhidi ya Barcelona.

Timu hizi mbili zitaingia uwanjani zikiwa kila moja ikiwa ina  nguvu sana.

Tuanze na kuichambua Chelsea;

 
Chelsea ya leo si ile tuliyoiona miezi miwili iliyopita. Ni nyingine kabisa. Hiyo ya miezi miwili ya nyuma ni Chelsea iliyokosa msisimko hata kwa wachezaji walipokuwa wakiingia uwanjani. Tuliona kwa macho.

Ilikuwa ni Chelsea iliyojaa nyota wenye kucheza ' kibinafsi zaidi' na si kama timu. 


Na kilichotokea kilitegemewa; Andres Boas  akapigwa chini kama kocha.  Tunajua, kuwa kocha kwa muda mrefu Chelsea lazima uwe ni mtu wa kujituma zaidi. Na anachokitaka sana mmiliki wa klabu, Roman Abramovic si kingine bali  taji la Kombe la Mabingwa.



Tuliona hilo, pale Chelsea ilipomtimua kocha Ancelotti mwaka 2011 hata kama chini yake Chelsea ilitwaa ubingwa wa Ligi ya Uingereza na FA Cup mwaka wa nyuma yake. Na Ancelotti, bila kutarajiwa,  alifukuzwa katikati ya msimu wa  ligi  na ikapelekea Chelsea kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Kombe la Mabingwa na wakawa nyuma ya Man United kwenye ligi ya Uingereza.



Ujumbe  Abramivich kwa makocha baada ya kufukuzwa kwa Ancelotti ni huu;  haisaidii kushinda ligi ya Uingereza au Kombe la FA, kilicho muhimu kabisa ni kutwaa taji la ubingwa wa  Kombe la Ligi ya Mabingwa.



Mara ile alipofukuzwa  kocha Villas Boas  baada ya matokeo mengi mabaya kwa Chelsea  ikawa kama moto mpya kwa Chelsea  umechochewa wakati kocha mpya, Roberto Di Matteo aliyekuwa chini ya kocha Villas Boas, alipokabidhiwa mikoba.



Kocha Di Matteo amefanikisha ushindi wa Chelsea katika mechi tano za mwanzo akiwa kama kocha.  Mechi waliyopoteza ni dhidi ya Manchester City iliyokuwa ikiongoza ligi.



Tumeona kwenye uwanja wao wa nyumbani, Chelsea wakisonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa  kwa kuipachika Napoli mabao 4-1. Ni hapo ndipo ilipoonekana  Chelsea mpya.

 
Zikiwa zimebaki timu nane kwenye ligi ya Mabingwa, Chelsea ikakumbana na Benfica. Hakuna aliyeamini macho yake  pale kocha Di Matteo  alipochagua kikosi chake cha wachezaji kumi na mmoja  wakiwamo wachezaji waliokalia benchi takribani msimu mzima chini ya kocha wa zamani , Villas Boas.

 
Kikosi hicho cha wachezaji kumi na mmoja kilikuwa na wakalia benchi kama vile Salomon Kalou aliingia kwenye kumi na mmoja wa mwanzo .  


Mikel ambaye naye alikalia benchi karibu msimu mzima alijikuta akishangazwa kwa kupangwa kwenye kikosi cha kumi na mmoja wa mwanzo.  Na Essien pia, ambaye hajaingia uwanjani kwa karibu miaka miwili alijikuta akiaminiwa kukimbizana na mpira uwanjani.

Katika mechi hiyo dhidi ya Benfica, na ikiwa na kikosi hicho cha kushangaza, Chelsea iliibuka washindi kwa bao moja kwa bila.  Ni Kalou aliyeamua hatma ya mechi hiyo kwa kufunga bao hilo pekee katika dakika  tisini za mchezo. Chelsea ilicheza kama timu.



Leo Chelsea inajitupa uwanjani dhidi ya Barcelona ikiwa inajivunia rekodi ya ushindi wa mechi zake tano katika kipindi kifupi kilichopita. Mechi ya mwishoni kabisa waliyoshinda ni dhidi ya Tottenhamn kwenye nusu fainali ya Kombe la FA.  Ni hapo Chelsea iliwafunga Tottenhamn kwa mabao 5-0.

 
Ni katika mechi hiyo, Chelsea walioonekana kuwa ni wenye kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu . Ilikuwa ni Chelsea iliyojihami vema  na iliyoshambulia kwa malengo.



Kwenye mechi ya leo Chelsea itacheza kwa kujiamini zaidi baada ya matokeo yao mazuri ya Jumamosi iliyopita. Siku zote, Chelsea huwa hawasifiwi kwa kusakata kandanda safi ila ni mahodari wa kukusanya pointi kwa kupambana kushinda mechi zao.


Na mwisho wa mchezo wowote wa kandanda, mashabiki huuliza nani kashinda. Hicho ndicho kinachohesabiwa. Na ndicho Chelsea wamedhamiria kukifanya dhidi ya Barcelona  jioni ya leo.





Hata hivyo, Chelsea watapambana na Barcelona inayocheza soka maridadi.  Ni Barcelona yenye wachezaji wenye kupiga  pasi za uhakika. Wenye kufanya mbwembwe na mpira, na zaidi, wana uwezo wa kupachika mabao mengi.

 
Jioni ya leo wachezaji wa Chelsea wasiwaze sana , kuwa leo wanatacheza mpira mzuri sana kuwashinda Barca na hata labda kumpiga tobo Xavi.

 
Inavyoonekana, Chelsea leo watafanya wawezalo kuhakikisha walau wanatoka sare ya bila kufungana ili Barcelona wasipate faida ya magoli ya ugenini. Badala yake, ni Chelsea watakaojitahidi kufunga mabao wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.



Wengi wenu mnajua, kuwa Barcelona ni mahodari wa kumiliki mpira  kwenye sehemu kubwa ya mechi. Hii ina maana moja, kuwa  Chelsea haitapata nafasi sana ya kucheza mpira wake. 


Nafasi nzuri za Chelsea kupachika mabao zitakuwa kwenye counter attack kwa maana ya mipira ya kurudisha mashambulizi. Mara nyingi mabeki wa Barca wenye hulka ya kupanda na washumbuliaji wao , hutokea wakafanya makosa ya kujipanga kwenye mazingira ya counter attack.



Wachezaji funguo kwa maana ya wachezaji muhimu kwa Chelsea jioni ya leo ni kama wafuatavyo;  Ramirez, Torres and Juan Mata. Hawa ndio kwa kiasi kikubwa wataichezesha Chelsea.

 
Kwa vile nafasi kubwa leo kwa Chelsea kufunga mabao ni kupitia counter attack- mipira ya kurudisha mashambulizi, basi, wachezaji wa Chelsea niliowataja hapo juu watakuwa na umuhimu mkubwa sana kwa vile wameonyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kukimbia kwa kasi wakiwa na mpira.



Chelsea pia inamuhitaji mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kutoa pasi za uhakika kwa maana ya kuwalisha wenzake mipira, na huyo si mwingine bali ni Malta. Kwa hakika, Malta ndiye Iniesta wa Chelsea.



Mabeki wa Chelsea David Luiz na Cahill watakuwa na umuhimu mkubwa uwanjani na hususan kwenye jukumu la kumsimamisha Messi.



Na Barcelona je?

 
Barca  wanaingia uwanjani jioni hii huku wakijivunia kushinda mechi zao nne za hivi karibuni. Katika mechi yao ya mwisho kabisa, Barca waliwafunga Levante kwa mabao 2-1 wakichezea kwenye uwanja wa ugenini.



Bila ya shaka, moja ya bao walilofunga bado ni la utata. Hata hivyo, kwenye mechi na Levante Barcelona hawakucheza na kikosi chao bora.

Silaha kubwa ya Barcelona dhidi ya Chelsea jioni ya leo ni  Lionel Messi.

 
Hakika, Messi amekuwa wa ' miujiza' kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa mwaka huu.  Hata kabla Ligi hiyo haijaisha, Messi tayari ameshavunja rekodi ya kufunga mabao mengi yaliyopata kufungwa kwenye Ligi ya Mabingwa.

 
Hadi sasa, Messi ameshafunga mabao 14 kwenye Ligi ya Mabingwa.  Huyu, Lionel Messi, ndiye mchezaji ninayedhani  atawasumbua sana vichwa Chelsea jioni ya leo.

Wachezaji wengine funguo kwa maana ya kuwa muhimu kwa Barcelona hii leo ni pamoja na Xavi na Iniesta.



Messi mwenyewe amekiri, si mara moja, kuwa asingeweza kuwa mzuri uwanjani kama alivyo sasa bila Xavi na Iniesta. Wawili hawa ndio uhakikisha Messi anaipata mipira anayohitaji katika kufanya miujiza yake uwanjani.



Na Xavi atakuwa na umuhimu wa ziada hii leo. Hii ni kwa sababu, katika aina ya mpira wanaocheza  Barcelona, Xavi ndiye 'injini kuu'. Ukiangalia Barcelona wanavyocheza, karibu mipira yote hupitia kwa Xavi. Ndiye ambaye mara nyingi huanzisha mashambulizi hata bila msaada wa mchezaji mwingine, na pasi zake nyingi ni sahihi kwa maana ya pasi za uhakika.

 
Wengi tunajua, kuwa Barcelona inacheza haswa mpira wa mashambulizi. Hivyo, hii leo mashambulizi hayo yatawapa nafasi nyingi za kufunga mabao.

 
Lakini, kama nilivyoweka wazi huko nyuma. Kuwa mashambulizi ya Barcelona yatatoa nafasi pia kwa Chelsea kufanya counter attack. Kurudisha mashambulizi ya haraka na ya hatari sana.

 
Barcelona ni timu ngumu kuifunga. Kwani, hata inapopoteza mpira wa pasi uwanjani, wachezaji wa Barca kwa pamoja watausaka mpira huko kwa juhudi zote hadi waukamate tena. Ni kama vile wanaamini kuwa uwanjani mpira ule wa duara ni wa kwao. Wametoka nao nyumbani kwao!


Ni katika hali hiyo Chelsea leo watakuwa na kazi ngumu pia ya kupata mipira ya kufanya counter attack dhidi ya Barcelona.Na wakati huo huo, Barceloa ni wazuri kwenye kujihami.  Ngome yao ya ulinzi inaundwa na watu kama Adriano, Mascherano, Pique na  Dani Alves.



Tusisahau pia, kuwa Barcelona wana mechi muhimu sana dhidi ya Real Madrid Jumamosi hii.   Kama hawatashinda mechi ya Jumamosi dhidi ya Real Madrid, basi, Barcelona watakuwa wamepoteza nafasi ya kutwaa ubingwa wa Hispania.



Hiyo inamaanisha, kuwa kocha Pep Guardiola  anaweza leo kuamua kuwapumzisha baadhi ya wachezaji wake muhimu.  Mpenzi wa soka usije ukashangaa kuona, kuwa mmoja ya wachezaji muhimu hawa kwa Barcelona; Xavi au Iniesta anaweza asicheze kwenye mechi ya jioni ya leo ili kujiandaa na pambano la Jumamosi dhidi ya Real Madrid.

 
Hilo likitokea laweza kuwa na faida kwa Chelsea, ingawa, bado naamini, kuwa , kutokuwepo kwa uwanjani kwa Xavi au Iniesta, kunaweza pia kusibadili sura ya mchezo kwa faida ya Chelsea.

 
Sasa nani anashinda leo?

 
Kwa kuangalia historia, Barcelona ina wakati mgumu kushinda mechi ya leo. Siku zote, Barcelona imekuwa ikipata tabu sana kuzishinda timu za Uingereza kwenye ardhi ya Uingereza. 



Itakumbukwa, mwaka jana Barcelona ilipoteza mechi yake dhidi ya Arsenal kwenye uwanja wa Emirates kwa mabao 2-1. Barcelona ikaja kuwafunga Arsenal nyumbani kwenye uwanja wa Camp Nou kwa mabao 3-1.  Ni kwenye Ligi ya Mabingwa iliyokuwa katika hatua ya timu 8 zilizobaki.


Na mwaka mmoja kabla ya hapo, Barcelona ilikutana na Arsenal   katika Ligi ya Mabingwa kwenye hatua ya timu 16. Pale uwanja wa Emirates matokeo yalikuwa 2-2 na baadae Barcelona ikashinda nyumbani Campo Nou kwa mabao 4-0.



Mwaka 2009, Barcelona ilikutana na Chelsea hii hii kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa. Pale uwanja wa  Stanford Bridge matokeo yalikuwa 0-0. Barcelona ilisonga mbele.

 Ikumbukwe, kwa Barelona, Chelsea ilikuwa ni klabu pekee ambayo Barcleona haikuweza kuifunga kwa mwaka huo.


Utabiri wangu:

Hivyo basi, kwa kuiangalia historia, natabiri matokeo ya mechi ya leo yatakuwa ni ya sare ya magoli. Au, Barcelona inashinda.



Ingawa, Chelsea inacheza uwanja wa nyumbani na ikiwa na matokeo mazuri ya mechi ya hivi karibuni dhidi ya Tottenhamn, nadhani, Chelsea hawana kile kinachohitajika kuifunga Barcelona.

No comments: