Na Luqman Maloto
Wiki iliyopita tulianza kujadili mada ya wivu na dawa zake. Tuliangalia mbinu muhimu zinazoweza kukufanya ukaondokana na tatizo la wivu wa kupitiliza kwa mwenzi wako. Leo tunaendelea kuanzia pale tulipoishia wiki iliyopita.
Amini kuwa mwenzi wako atafanya mambo sahihi hata kama wewe hutakuwepo. Muamini kuwa anajitambua, kwa hiyo hatakuwa na muda mchafu wa kutenda maovu kwa kigezo kwamba haupo. Ana akili timamu, akiamua kutenda ‘uwaluwalu’, hashindwi hata kama utakuwepo.
Kwa kawaida, anaweza kuwepo mtu ambaye atakufanya usimuamini mwenzi wako hata kidogo. Inawezekana akakujengea picha kutokana na maneno ya zamani au matukio yaliyopita. Je, unaona wivu kwa sababu umeambiwa mpenzi wako aliwahi kutoka na watu wawili tofauti kabla yako?
Wivu wa nini? Kwa nini maneno hayo yakuchanganye akili? Je, ulimkuta akiwa mbumbumbu wa mapenzi na hajawahi kutoka na yeyote? Kumbe utabaini kuwa historia ya mwenzi wako haina maana inayokubalika kwenye uhusiano endelevu.
Wanasema Shetani wa jana, leo anaweza kuwa malaika. Vilevile malaika wa leo kesho anaweza kuwa Shetani. Inawezekana hao ulioambiwa alitoka nao walimtenda ndiyo maana hakuwapa nafasi ya kudumu lakini wewe umepata fursa hiyo kwa sababu unakidhi mahitaji yake. Hata hivyo, hii haina maana kuwa kila wivu unaotokana na kuambiwa hauna maana. Yapo mengi yenye maana.
8. MWONESHE MWENZI WAKO
Ukiwa na mwenzi wako, muoneshe kwa mifano halisi jinsi unavyojisikia au unavyoweza kumtendea katika nyakati ambazo unamuonea wivu. Kufanya hivyo, ni rahisi kwake kutambua maumivu yako, vilevile na yeye atajua mahali ambapo anakosa mengi matamu.
Mtu anapoona wivu wa ndani, husumbuliwa na maumivu ya moyo. Aghalabu, akili yake hushindwa kufanya kazi inavyotakiwa. Mantiki ya hoja hiyo ni kwamba mwenzi wako hawezi kukutendea mambo matamu, ikiwa kichwa chake hakitakuwa katika hali ya kawaida.
Unaweza pia kuvuta picha na kujadili muonekano wako pindi unapokuwa na wivu. Hakikisha mwenzi wako anakuelewa kinagaubaga kile unachomaanisha. Je, umegundua umepoteza raha kiasi gani? Umefahamu namna ambavyo huwa unaboa? Mpe uhuru mpenzi wako akwambie ukweli.
Inawezekana akawa anasita kukwambia bayana kutokana na hofu. Unapaswa kulijua hilo mapema. Unaweza kumpa nafasi aseme, akakujibu hakuna kitu. Ukishagundua kuwa anakuhofia, jaribu kumshawishi ili afunguke. Akikubali kueleza la moyoni, ni tiba kubwa kwako.
Bila shaka utagundua ni kiasi gani anakerwa na tabia yako ya wivu. Je, ni nani anapenda kumuudhi mwenzi wake kila siku? Hakuna na kwa hakika hata wewe mwenyewe hupendi. Hivyo basi, amani yake itatokana na tabia yako ya kumuonea wivu.
Fikiria kuwa anashindwa kuwa mtulivu kufanya jambo lolote kwa sababu anahofia unaweza kulipokea tofauti. Kwa nini unamnyima uhuru kwa sababu ya wivu wako? Fungua moyo leo, muoneshe kuwa unamuamini. Imani yako itamfanya aongeze upendo kwako. Siku zote, mapenzi husafiri kwa mtindo wa nipe nikupe.
Hata hivyo, njia hii kwa watu wengine hushindwa kufanya kazi. Inapasa mtu mwenyewe awe amedhamiria kurejesha amani na furaha kwake na kwa mwenzi wake. Vema uzingatie kwamba wivu ukizidi ni ushamba. Jamii itakudharau, hata mwenzi wako akikuchoka, anaweza kukugeuza zuzu.
7. JIAMINI
Wivu mara nyingi huanza kutokana na kukosa kujiamini. Jiulize, unajisikia salama wewe mwenyewe? Je, unaogopa kwamba mpenzi wako anaweza kukuacha kwa sababu ya kupungukiwa sifa kadhaa? Mambo mengi kati ya hayo yanapogota kichwani, huyafanya maisha yako yatawaliwe na wivu.
Inawezekana mwenzi wako anakupenda kuliko wewe unavyompenda. Si ajabu, akawa anawaza kufanya maisha bora zaidi akiwa na wewe. Amekukubali kwa namna ulivyo kiasi kwamba hawazi kukupoteza. Tofauti na mawazo yake, tabia yako ya kutojiamini, hufikiria kwamba hakupendi.
Ikitokea akawa anafanya mawasiliano na mtu wa jinsia kama yako, hapo unaanza kuweweseka, mara ukasirike, upekue simu yake bila sababu, umkaripie, unune na kususa kuzungumza naye. Hiyo ni kujipa jakamoyo.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment