Bi. Fatma Kange akiongea na wadau wa Sanaa kuhusu mfumo maalum wa kimataifa wa utambuzi na udhibiti wa bidhaa mbalimbali wakati akiwasilisha mada kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA mapema wiki hii. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA Godfrey Lebejo na Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Bw. Materego akisisitiza jambo wakati akiongea na wadau wa Sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA wiki hii. Alieleza kuwa, ni wakati sasa wa kuirasimisha sekta ya Sanaa.
Mtendaji kutoka Kampuni ya Global Standard One (GS1), Andrew Karumuna akionesha moja ya kazi ya Msanii Judith Wambura (Lady Jay Dee) iliyowekewa alama maalum ya kimataifa ya utambuzi na udhibiti wa bidhaa kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.Lady Jay Dee ni msanii pekee ambaye amekwishaingia na kuanza kunufaika na mfumo huu.
Mdau na mkereketwa wa Sanaa na Jukwaa la Sanaa, Francis Kaswahili akiuliza na kuchangia mada kuhusu mfumo huo wa utambuzi na udhibiti wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za Sanaa.
Mdau huyu alipongeza ujio wa mfumo huu lakini akataka Wasanii wahamasishwe kuingia katika mfumo ili kudhibiti uharamia.
Sehemu ya Wadau wa Jukwa
Na Mwandishi Wetu
Huenda kilio cha wasanii juu ya wizi wa kazi zao kikapungua kama si kufikia kikomo iwapo wasanii wataamka na kushirikiana na kampuni ya Global Standard One (GS1) ambayo imekuja na mfumo wa kimataifa wa kutambua na kudhibiti kazi za Sanaa.
Akizungumza wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Kaimu Mkurugenzi wa kampuni hiyo Fatma Kange alisema kuwa, mfumo huo wa kuziwekea alama ya utambuzi ya kimataifa (barcode) kazi za wasanii utasaidia kudhibiti uharamia kwenye sekta ya sanaa na kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi.
“Mfumo huu ni wa kimataifa, umekuwa ukitumika duniani kote miaka 38 iliyopita, hapa kwetu ni mpya kabisa. Ni mfumo wa kutambua bidhaa halali kwa kuziwekea alama maalum (barcode) ambayo itazifanya zitambuliwe kimataifa na kutokughushiwa” alisema Bi. Kange.
Aliongeza kuwa, mfumo huo unalenga kurasimisha sekta ya Sanaa kwa kuwafanya wasanii kwanza kujisajili na baadaye kazi zao kuwekewa alama maalum ambapo sasa watajua idadi halisi ya nakala (bidhaa za sanaa) walizozalisha, fedha walizoingiza na zaidi kutazuia kazi zao kuuzwa hovyo mitaani pasipokufuata taratibu.
“Lengo ni kazi za wasanii kutambuliwa kimataifa, kuuzwa kwenye maduka makubwa na kupewa thamani halisi. Wenzetu katika nchi zilizoendelea wako mbali katika hili, kazi zao zinauzwa kwenye art stores tu (maduka maalum ya kazi za Sanaa)” alisisitiza Kange.
Akieleza jinsi Wasanii watakavyojiunga, Bi. Kange alisema kuwa, wako kwenye mikakati ya kuwaelimisha Wasanii lakini akasisitiza kuwa, mfumo huo huendeshwa kwa wasanii wenyewe kuridhia na baadaye kazi zao kuwekewa alama hiyo ambapo hukatwa kiwango kidogo sana cha fedha baada ya kukubaliana na wasanii wote.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema kuwa, kwa muda mrefu sekta ya Sanaa imekuwa ikichukuliwa kama ya burudani tu kwa hiyo muda umefika wa watanzania kuichukulia Sanaa kama biashara na kuipa thamani halisi.
“Kwa sasa Sanaa imekubalika, ule wakati wa kuiona kama burudani tu umepita. Hatuna ujanja lazima tuirasimishe sekta ya Sanaa” alisisitiza.
Aliwaahidi Wasanii kupitia mashirikisho na vyama vyao kuwa, kutakuwa na vikao vya mara kwa mara na kampuni hii ili kuona ni kwa kiwango gani suala la udhibiti na utambuzi wa kazi zao kupitia nembo hii linaweza kutekelezwa.
No comments:
Post a Comment