NAAMINI wasomaji wangu wapenzi mtakuwa wazima wa afya njema na mnaendelea vyema na shughuli zenu za kila siku. Karibuni tena katika uwanja wetu wa kupanuana mawazo juu ya mambo ya mapenzi.
Rafiki zangu, leo nahitimisha somo letu ambalo tumekuwa nalo kwa wiki tatu mfululizo. Bila shaka kuna vitu mmejifunza kupitia mada hii. Kama ndiyo mara ya kwanza kuanza kusoma somo hili, nazungumza na vijana ambao wanajiandaa kuingia kwenye ndoa.
Katika matoleo yaliyopita nimefafanua mambo mengi sana ambayo kijana anapaswa kuyazingatia kabla ya kuchukua uamuzi mzito wa kuingia kwenye ndoa.
KWA NINI MZITO?
Suala la ndoa si la maigizo, ni uamuzi ambao unatakiwa kuangaliwa kwa jicho la tatu. Inakupasa utambue kwamba unakuwa umeingia kwenye muunganiko wa maisha ya watu wawili.
Unakutana na mtu ambaye si wa familia yako, ambaye atakuwa na malezi yake aliyozoeshwa huko kwao. Hupaswi kukurupuka katika hilo.
Yapo mambo mengi sana muhimu ambayo unapaswa kuyazingatia ili uweze kuingia kwenye ndoa imara yenye amani.
KWANZA AKUPENDE...
Ni lazima mwenzi ambaye unatarajia kuingia naye kwenye ndoa awe anakupenda kwa dhati. Pendo ndiyo msingi wa kila kitu. Kama kweli anakupenda ni rahisi kujenga familia yenye maelewano mazuri.
Siwezi kuzungumzia kuhusu sifa za mwenzi anayekupenda, maana nimeshachambua hili kwa kina katika matoleo yaliyopita. Kwa kudodosa tu, anayekupenda atakuthamani, atakusikiliza na kukupa kipaumbele katika mambo yake yote.
Somo la alama za penzi la dhati, nimeshachambua mara nyingi sana. Kifupi mwenzi ambaye unatarajia kuingia naye kwenye ndoa anapaswa kuwa na penzi la dhati kwako. Upendo ndiyo nguzo kuu marafiki zangu.
NAWE UNAMPENDA?
Kama nilivyotangulia kusema, huwezi kuingia mkataba wa maisha na mtu ambaye humpendi kwa dhati. Lazima wewe pia umpende. Achana na utamaduni wa kuingia kwenye ndoa ukiwa mguu nje, mguu ndani kwa mategemeo kwamba eti utampenda ukiwa tayari mmeshaoana!
Hakuna kitu kama hicho rafiki yangu. Lazima nafsi yako ikuhakikishie kuwa ni kweli umempenda ndipo mambo mengine yafuate.
Mapenzi hayalazimishwi. Acha kujaribujaribu! Kama unampenda, utajua tu, kama humpendi usipoteze muda wa mwenzako; mwambie ukweli, jitoe!
KIPI KIZITO?
Kati ya mambo ambayo yanaongeza mapenzi ya dhati kwa wawili ni pamoja na kufanyiwa kitu kizito/kikubwa kisichosahaulika kirahisi. Je, kuna kitu ambacho umefanyiwa na mwenzako huwezi kukisahau?
Chunguza hili kwa makini. Marafiki zangu, hapa sizungumzii zawadi za sketi au suruali. Sipo kwenye upande wa manukato au mikufu? Yapo mambo makubwa ambayo ukitafakari na kukumbuka namna mpenzi wako alivyokusaidia unaona kweli anastahili kuwa mwenzi wako wa maisha katika ndoa takatifu.
Hakuna majaribio kwenye ndoa ndugu zangu. Ni maagano. Ni kifungo, wengine wanasema ni kitanzi! Umejiandaaje? Fanyia kazi kabla hujajutia, ukiwa tayari ndani si rahisi kutoka.
NI UAMUZI BINAFSI ZAIDI
Kamwe usikubali kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya msukumo wa kitu/mtu isipokuwa wewe mwenyewe na nafsi yako. Wewe ndiye unayepaswa kuwa mwamuzi wa mwisho katika kuamua nani anakufaa.
Achana na utaratibu wa kuangalia nani amefanya nini na wewe ukafuata mkumbo. Kuna wale ambao huoa au kuolewa kwa mashinikizo ya wazazi au ndugu zao. Hili ni kosa.
Kumbuka si kwamba wao ndiyo watakwenda kuishi na huyo wanayekuchagulia. Mwisho wa siku wewe ndiye ambaye utaingia kwenye ndoa hiyo, kama ni matatizo utayapata wewe peke yako bila yeyote kuingilia.
Fanya uamuzi wa dhati moyoni mwako, jiridhishe kwamba uliyemchagua ndiye yule ambaye ulikuwa unamsubiri siku zote, kisha ndipo uingie kwenye ndoa. Kukosea kuchagua mwenzi wa maisha ni tatizo kubwa marafiki zangu. Huwezi kukata rufaa ya kuchagua mwenzi mwingine.
Ndiyo maana inaelezwa kwamba, nyuma ya mafanikio mazuri katika familia kuna uhusiano mwema kwa wanandoa husika. Ndiyo kusema kwamba, kama ukikosea kuchagua mwenzi wako wa maisha, hakuna ubishi kwamba, hata maisha yako nayo yatayumba!
Utafanikiwa vipi kama kila siku mnagombana? Hakuna furaha ndani ya nyumba? Kwako kufanikiwa itabaki kuwa ndoto ya mchana. Mada imeisha marafiki zangu.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayendikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment