Na: Luqman Maloto
CHANGANUA mambo inavyotakiwa, kadiri unavyoyafanya maisha yako kuwa na majanga, ndivyo na umri wako unavyoufupisha. Hii ikupe changamoto ya kuchagua jema kati ya mambo mawili. Kuongeza siku za kuishi au kuzipunguza.
Mantiki hapa ni namna ya kuyatumia mapenzi ili kupata umri kulingana na namna utakavyokadiriwa na Mwenyenzi Mungu. Vilevile, ni jinsi unavyokwenda kinyume nayo, matokeo yake yakakufanya umri wako upungue.
Hapa hakuna maana ya matumizi ya ARV ambayo humuongezea siku za kuishi mwathirika wa VVU, muongozo ninaoutoa hapa ni namna bora ya kuyatumia mapenzi ili uweze kuishi kwa furaha. Hii ni kwa sababu furaha huleta amani ya moyo.
Moyo unapokuwa na amani, inakuweka huru kutoka kwenye msongo wa mawazo. Inakulinda na shinikizo la damu kwa sababu utulivu unaokuwa nao, unawezesha moyo kufanya kazi yake ya kusambaza damu kwenye kona mbalimbali za mwili kama inavyotakiwa.
Inapotokea moyo unashindwa kufanya kazi sawasawa, hutengeneza sumu hatari kwenye mishipa ya damu, huathiri mtiririko wa damu kwenye ubongo, hivyo kusababisha oksijeni ikose mtiririko mzuri kwenda kwenye ubongo.
Kumbe sasa mapenzi ni afya, utayaona matunda yako endapo tu utakwenda nayo vizuri. Unapaswa kuhakikisha moyo wako unakuwa huru kila siku (au kwa kadiri ya muda mrefu) ili kuondoa msongo kwa ajili ya usalama wako.
Kanuni kuu ya kuhakikisha unafanikiwa kwenye lengo lako ni kusimama katika muongozo huu: Penda unapostahili, wekeza penzi lako kwa mtu anayestahili. Macho na tamaa visikupoteze njia, mengi uyaonayo ni fahari ya macho tu.
Ndugu wengi waliodanganywa na tamaa ya macho, wakaingia kichwakichwa, wameshatangulia mbele ya haki, wengine wanaendelea kuteseka na dunia. Hakikisha unayempenda, anakuwa ni yule anayeweza kurejesha upendo unaompa.
Hakikisha unayewekeza mapenzi kwake, naye yupo tayari kwa ajili yako. Penzi la upande mmoja huzaa matokeo mabaya. Hugeuka mateso makubwa kwako, huumiza moyo kabla ya kusababisha madhara ya kiafya kama nilivyotangulia kueleza hapo awali.
Wapo watu ambao siku zote wanaonekana wana miili dhaifu. Wanaishia kutuhumiwa na wengine kwamba wameathirika na virusi vya ugonjwa wa kisasa, kumbe sivyo, wapo salama kabisa na maradhi hayo, isipokuwa kinachowauguza ni mapenzi.
Hapa nikuongezee kitu kwamba siku zote unapaswa kutambua kwamba uimara wa mwili wako, unaanzia moyoni. Ukiwana moyo imara, utaona namna mwili wako utakavyokuwa na nguvu, udhaifu wa moyo huzaa udhaifu wa mwili.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment