Social Icons

Tuesday 28 August 2012

LEO KATIKA MAHUSIANO:Mapenzi siyo presha, ila presha inaletwa na mpenzi uliyenaye -2



Ni mwendo wa kimagharibi. Hakuna mapenzi, ila kupozana haja. Wakitamaniana, wanamalizana leoleo tu. Ameimba Ali Kiba kwenye wimbo Single Boy.
KIINI CHA MAPENZI YA KICHINA
Kuna ulimbukeni uliwaingia watu. Ghafla, kuna tabaka fulani (wakiwemo hawa mastaa wetu), wakaanza kuona mapenzi kama mchezo. Yaani, mtu anaweza kuhusika kimapenzi na mwenzake hata kama hawapendani. Angalia skandali za Wema, Diamond, Jokate Mwegelo, Irene Uwoya na wengineo.

Ni mtindo wa kuyabeba mapenzi kama mchezo wa kujifurahisha. Masistaduu na mabrazameni, hawayabebi kwa uzito wake unaostahili. Wewe msomaji wangu, unayeamini maadili na unathamini moyo wako, utakosea kupita kiasi endapo utaacha njia inayopendeza na kushika mtindo huu wa kimapenzi.
Jaribu kutafakari: Leo inazungumzwa kwamba Diamond anatoka kimapenzi na Aunt Ezekiel. Hapohapo tambua kuwa Wema alikuwa mchumba wa staa huyo wa Bongo Fleva. Ongeza lingine kuwa Jokate naye kapita kwa kijana huyohuyo. Halafu nakupa siri moja kuwa wote hao ni washiriki wa Miss Tanzania mwaka 2006.
Inamaanisha kuwa walikaa kambi moja lakini wamediriki kuchangia mwanaume mmoja. Wema na Aunt ni marafiki, kwa hiyo hawana wivu. Hata kama ulikuwepo ila sasa umekwisha. Na hii ndiyo tafsiri ya mapenzi ya Kichina. Mwendo wa kuzungukana, leo kwako, kesho kwa mwingine.
Akina Wema, Jokate na Diamond, kwao inakuwa rahisi kujulikana kutokana na umaarufu wao. Waandishi wa habari wanawafuatilia kila kona, hivyo wanaripotiwa na jamii inajua nyendo zao. Kundi hilo ndilo linatajwa kwamba wahusika wake hawajatulia. 
Hata hivyo, upo ukweli uliotimia kuwa mitaani kwa jamii ya watu wa kawaida, wapo wachafu kuliko. Mwanamke mmoja anaweza kuwapanga wanaume watano kwa siku. Akitoka huyu anakwenda kwa mwingine. Anabadili nyumba za kulala wageni.
Huyu, hajitambulishi kama changudoa. Atasimama pembeni na kwamba yeye ni mtu mwenye heshima zake. Akiwaona machangudoa usiku wa manane wakiwa wamejipanga mawindoni na mavazi yao ya nusu uchi, atawalaani. Ni msemo wa nyani haoni makalioni kwake!
Huko nyuma nilishawahi kueleza mfano wa wanandoa kusalitiana. Nikabainisha kwamba baadhi ya wanaume hufanya makosa pale wanapowakataza wanawake wao kufanya kazi. Eti wanataka wakae tu nyumbani. Hapa ndiyo kuna jambo, kwani mtu anapokaa bila kazi, hukaribisha hisia za karibu.
Hii ikanifanya nijenge hoja kutokana na muongozo wa kisaikolojia kwamba akina mama wa nyumbani, ni kundi hatari mno kusaliti ndoa. Mara nyingi wanakuwa hawapo bize, kwa hiyo hisia za kimapenzi zinakuwa karibu na matokeo yake hujikuta wakifanya zinaa na watu wa kushangaza.
Hujawahi kusikia mke wa mtu katembea na ‘houseboy’ wake? Vipi mwanamke kufanya zinaa na mdogo wa mume wake? Je, muuza bucha kujilia vyake nyakati wa mchana kwa ofa za robo ya nyama anayomuongezea mke wa mtu aliyekwenda kununua kilo mbili? Hayo yapo kwenye mazingira yetu ya kila siku.
Kila siku wauza magenge na maduka, wanaingilia ndoa za watu. Nafasi hizo wanazipata kwa sababu ya kutokuwepo ubize kwa wanawake hao. Asili yetu tunapenda utani, hivyo wakitaniana mara mbili, mwanamke anahama kihisia. Keshokutwa asubuhi mume akiondoka, huyu anakimbilia gengeni.
Huu ni mfano katikati ya mada yetu. Mtu wa aina hii akiwaona machangudoa barabarani, atawalaani kupita kiasi. Hata hivyo, mtindo wa maisha yake hauna tofauti na changudoa kutokana na ukweli kwamba mtu mwenye staha na heshima, hawezi kujilimbikizia vidumu. Mume usiku, mchana muuza bucha au houseboy, haijakaa vizuri.
Inabidi kutoa mfano wa aina hii kutokana na ukweli kwamba masistaduu wanaweza kukaa vibarazani na kusogoa kuwa mbona wake za watu wanaojionesha ni watu makini, nao wanacheza sana mechi za nje? Wanadanganywa nao wanadanganyika. Maisha yanaendelea, mke wa mtu anaitwa fuska pasipo yeye mwenyewe kujijua.
Dunia ilivyo ni kwamba huwezi kutoka kimapenzi na mtu halafu ikabaki kuwa siri. Iwe isiwe lazima itavuja. Japo maneno yanaweza yasifike kwa mumewe lakini kwa watu baki watamzodoa au kumsogoa kila anapopita. “Yule ni mke wa mtu lakini tabia zake chafu.”
Wapo watakaozungumza: “Yule mwanamke hana kinyaa, ana mume lakini utadhani changudoa kwa jinsi anavyoisaliti ndoa yake.” Wewe hutayajua hayo unayosemwa, utajioni upo vizuri ukiamini unayofanya hayaonekani. 
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info

No comments: