Social Icons

Thursday, 30 August 2012

Leo Katika Mahusiano:Mnaowawekea malimbwata waume zenu, someni hii!


MAPENZI ya siku hizi yana changamoto nyingi sana. Usanii umechukua nafasi kubwa kiasi kwamba kila aliye na mpenzi, hana uhakika wa asilimia zote kudumu naye. Kupendwa na kuachwa imekuwa ni kama fasheni.
Lakini, wapo ambao wakipenda wanamaanisha kweli na wako radhi kufanya lolote kuhakikisha wanadumisha penzi lao ili kujihakikishia furaha kwenye maisha yao.

Katika hili la kudumisha uhusiano, yapo mengi ya kufanya kwa wawili waliotokea kupendana. Kwanza, lazima kila mmoja awe na penzi la dhati kwa mwenzake. Kama itatokea mmoja ndiyo kapenda na mwingine anafuata mkumbo tu, ni vigumu kwao kudumu.
Hapo ndipo yanapotokea mazingira ya yule aliyependa kufanya kila awezalo kalazimisha kupendwa.
Hakuna kitu kibaya kama kulazimisha mtu ambaye hakupendi akupende eti kwa kuwa tu wewe umempenda. Nasema hivi kwa kuwa madhara yake ni makubwa kuliko tunavyoweza kufikiria.
Hivi karibuni niliongea na dada mmoja ambaye alitokea kumpenda sana mwanaume ambaye ni mfanyabiashara. Anasema: “Nilimpenda sana yule kaka, lakini niligundua hakuwa na mapenzi ya dhati kwangu. 
“Nilizungumza na rafiki yangu mmoja ambaye aliniambia kuna limbwata ambalo nikilipata naweza kumfanya mwanaume huyo akanipenda.
“Huwezi kuamini nilipelekwa kwa mganga mmoja ambaye alinipa dawa ambayo alinitaka nimuwekee yule mpenzi wangu kwenye chakula, chai na hata kwenye maji yake ya kuoga. Nilifanya vile nikiwa na dhamira ya kuhakikisha nakuwa na mwanaume huyo.
“Yaliyonikuta ni makubwa, nilipopewa ile dawa nikawa nimebweteka nikiamini ingenisaidia kumshika. Ni kama nilikuwa namfukuza kwani alianza kuchelewa kurudi nyumbani na ikafika wakati nikagundua kuna mwanamke mwingine ambaye tunashea penzi. Mbaya zaidi alimpa na ujauzito na hapo ndipo nikaachana naye.”
Tunajifunza nini hapa? Limbwata hilo linalotumiwa na baadhi ya wanawake kuwashika wanaume si la kutegemea katika kutengeneza penzi. Unaweza kutumia limbwata ambalo linaweza kukujengea imani kuwa litasaidia kujihakikishia penzi kisha ukasahau yale ya msingi ambayo unatakiwa kuyafanya kwa mpenzi wako na matokeo yake ukajikuta unaachwa.
Kwa kifupi hakuna limbwata ambalo limethibitishwa kuweza kumdatisha mwanaume isipokuwa mwanamke mwenyewe ndiye limbwata. Yale ambayo atakuwa anamfanyia mpenzi wake, ndiyo yanayoweza kumfanya akapendwa.
Kwa taarifa yenu, wapo wasichana ambao waliingia kwenye penzi na wanaume ambao walikuwa hawawapendi lakini wakajigeuza malimbwata kwa kutumia uanamke wao. Walinyenyekea, wakatoa penzi la kipekee, wakawaonyesha waume zao kuwa wao ni tofauti na wanawake wengine.
Mwisho wa siku walifanikiwa kuzibadili fikira za wapenzi wao ambao nao walijikuta wakipenda tena kupitiliza. Si kwa kulazimishwa lakini kwa kubaini wanafanyiwa mambo ambayo hawawezi kuyapata kwingine. Hapo ndipo unapoweza kuona namna mwanamke mwenyewe anavyoweza kuwa limbwata bila kwenda kwa mganga.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: