Social Icons

Saturday 22 September 2012

LEO KATIKA MAHUSIANO: MAHABA NIUE NI MATOKEO YA KUKOSEA VIPIMO VYA MAPENZI



KAMA nilivyoanza mada hii wiki iliyopita, mapenzi ni changamoto. Ni mtihani mzito pale unapokutana na mwenzi wa maisha ambaye ana hulka sawa na rafiki mnafiki. Inahitaji utulivu na umakini wa hali ya juu mno.


Kila siku nashauri watu wayaheshimu mapenzi. Hii ni kwa sababu yenyewe ndiyo huamua furaha na utulivu wa akili na mwili. Vilevile yanaweza kukupa nguvu ya kutekeleza majukumu yako ya kila siku kwa kiwango cha hali ya juu. Yakiutonesha moyo wako ni ulemavu mkubwa.

Pamoja na heshima, ni lazima ujenge kiburi kwa mtu ambaye unamuona hakupendi. Haeleweki, kila siku anakuingiza kwenye mawazo na maumivu ya moyo. Huyo hupaswi kuumiza moyo kwa ajili yake. Unatakiwa ‘kum-scan’ halafu ‘um-delete’ haraka.

Huyo ni kirusi hatari kwenye maisha yako. Angekuwa wako angekujali na kuthamini upendo wako. Unapoona hasikilizi shida zako wala kujali maumivu unayoyapata kutokana na jinsi yeye anavyokutenda, unachotakiwa kufanya ni kumbadili kutoka mpenzi hadi kuwa rafiki mnafiki. Inawezekana.

Hujui huyo anayekutenda malengo yake ni nini. Sasa basi, kama dhamira yake ni kukuumiza na unapomuonesha kwamba kweli umeumia, unakuwa umemfanya ajione amefanikiwa. Hii ndiyo sababu ya mimi kukutaka usikubali kuonesha udhaifu wake kwake. Atakwenda kuwakenulia wenzake.

Hata kama una moyo mdogo mpaka unaingia kwenye kundi la akina “mahaba niue”, hakikisha udhaifu huo rafiki mnafiki hauoani. Lia ndani peke yako, akitokeza jikaushe. Akikuuliza mbona macho mekundu? mjibu ulikuwa umelala kisha tabasamu halafu mwambie, “usijali sweetheart, lete stori nyingine.”

Ni falsafa ya kukuwezesha kupata alama A kwenye mapenzi. Kama ambavyo kanuni inakwambia usimuoneshe adui yako udhaifu ulionao, ndivyo ambavyo na rafiki mnafiki unavyotakiwa kumkabili. Hakupendi, kwa hiyo siyo mtu mwema kwako, anakucheza shere, hana tofauti na adui.

Kwa faida yako, uimara wako kwa mwenzi ambaye haoneshi kukujali, unaweza kumbadili kutoka alipo hadi kuwa mpenzi bora wa maisha yako. Atabadilika pale tu atakapogundua kwamba wewe ni mtu makini na huhitaji kuchezewa.

Atabadilika pale atakapogundua kuwa wewe ni moyo wa chuma. Mwenye malengo ya kukucheza shere halafu akakutana na kisiki cha mpigo, humfanya afikirie mara mbili, fikra hizo humzalishia mawazo, anapokuwaza sana mwisho huumia. Unaona sasa, alitaka kukuumiza lakini kaumia yeye.

Maumivu anayoyapata ndiyo yatakayomfanya ajirudi. Atakuheshimu na mwisho atakuonesha upendo wa dhati. Sasa wewe shika hili, anapoanza kukuonesha upendo, upime kwa umakini wake halafu jiridhishe kama kweli ana vigezo vya kumfungulia moyo.

Sikushauri ukimbilie kumuacha mpenzi asiyeeleweka, kwani inawezekana akawa ndiye mpenzi bora ila anasumbuliwa na mapepe tu. Siku zote usilaumu uhusiano, tambua kwamba mpenzi mzuri atakupa furaha ya maisha na mpenzi mbaya ni changamoto ya kukupa uzoefu.

Zingatia kwamba wewe unaweza kumbadili mpenzi asiyeeleweka mpaka kuwa mpenzi muwajibikaji.
Kwa hisani: GPL

No comments: