KATIKA hali ya kawaida kila mwanadamu unahitaji kufarijiwa juu ya matatizo unayokumbana nayo kwa namna mbalimbali maishani. Mkwamo wa vifungo vya hali ngumu ni suala linalohitaji msaada wa faraja kama tiba mbadala.
Hata hivyo, uchunguzi unaonesha kuwa karne tuliyonayo kwa sasa, hali ya watu kujali na kujitolea kwa ajili ya wengine inaonekana kunyauka siku hadi siku. Mume, mke, ndugu, matajiri na watu wenye uwezo wanaonekana kushindwa kutoa faraja kwenye matatizo ya watu.
Maisha ya sasa kila mtu anaishi sawa na msemo wa ‘abiria achunge mzigo wake’. Aidha kasumba ya kutegemea msaada wa kufarijiwa inatajwa kuwa mzigo unaoelemea wanadamu nyakati hizi hasa pale unapokuwepo ukweli kwamba wafariji hawapo au wamepungua kabisa ulimwenguni.
Jitihada za wanasaikolojia ulimwenguni zimekuwa zikijaribu kutafuta jibu la tatizo hili la nini kifanyike ili watu waweze kufarijika bila kuwategemea watu wengine. Msingi wa utafiti huo ni kupata suluhisho linalokwenda na wakati kwa watu kuvunjika moyo na kuangamia kwa ukosefu wa watu wa kuwafariji.
Kama wanadamu tuna shinda zinazotusonga, tumedhulumiwa, tumefiwa na tuliowategemea na kuwapenda, tuliowaamini wametusaliti, tunaumwa magonjwa sugu, ni masikini wa kutupwa, tunahitaji faraja, lakini ndugu zetu tunaowategemea wamegeuzwa na kushupaza shingo, yaani hawataki kutusaidia hata kidogo. Sasa tufanye nini?
Njia pekee inayoweza kutusaidia kukabiliana na maisha magumu ambayo hayana watu wa kutupenda, kutusaidia, kutuhurumia na kutujali, ni sisi wenyewe kuchukua jukumu la kuzifariji nafsi zetu na njia za kufuata ni hizi:-
TUSIKOSOE UTU WETU
Tatizo kubwa linalowakabili watu wengi ni kuukosoa utu wao. Ndiyo maana wanakimbilia kuamini kwamba wasipoweza wao ndugu na jamaa zao watawasaidia.
Udhaifu huo wa kujikosoa ndiyo unaozaa tunda la kuhitaji faraja kutoka kwa watu. Lakini jambo linalosikitisha zaidi ni ambalo liliwahi kumchekesha Tara Parker-Papa mwandishi wa blogu ya afya aliyochangia kwenye tovuti ya New York Times pale mtu anaposubiri sauti toka kwa mwingine imwambie POLE.
Ni wazi kwamba hatuwezi kusubiri sauti za pole kwa sababu nasi tunazo. Tunachotakiwa kufanya ni kuziamini nafsi zetu. Zaidi ya hilo, kukiwepo na mahitaji yoyote ya fedha au nguvu kutoka kwa mtu kutuwezesha kufarijika, si faida kwetu kusubiri zije wakati wenye nazo hawataki kutupatia.
Sisi wenyewe kama binadamu tunaweza kusimama peke yetu na kujipenda kwa jinsi tulivyo bila kuainisha na kujali upungufu wowote tulio nao kwa vile matatizo ya mwanadamu hayajapata kumalizwa na uwezo wa mtu, uwe wa kuazima au wa kwake mwenyewe. Lazima tujiwekee mazingira ya kujithamini sisi wenyewe.
Yamkini nitakuwa sawa nikisema matajiri tunaowasubiri watufariji kwa misaada yao nao wana shida zinazowatoa jasho. Hao ndugu, rafiki na jamaa zetu tunaodhani wamekamilika kimaisha, wana yao yanayowaondolea faraja. Huu ni ukweli usiopingika.
Itaendelea wiki ijayo, usikose.
GPL
No comments:
Post a Comment