Kuna ndoa ambazo ukizifuatilia zinasikitisha sana. Ni ndoa ambazo furaha imetoweka, yaani kila mmoja yuko kwenye ndoa ili mradi tu yupo lakini hatimizi yale ambayo yanatakiwa kufanywa na mwanandoa.
Upweke ni jambo linaloumiza sana hasa kwa mtu aliye kwenye ndoa. Kuna dada mmoja ambaye hivi karibuni nilizungumza naye kuhusiana na maisha yake ya ndoa. Aliyonieleza yalinisikitisha sana na ndiye aliyenipa mwanga wa kuandika mada hii.
Anasema: “Mume wangu anafanya kazi ila mimi ni mama wa nyumbani, nashukuru napata mahitaji yote muhimu kutoka kwake.
“Kikubwa ninachokikosa kutoka kwa mwanaume huyu ni penzi. Amekuwa ni mtu ambaye yuko ‘bize’ sana, yaani anarudi nyumbani usiku, ukimgusa anakuambia amechoka sana na anahitaji kupumzika.
“Mbaya zaidi, hata siku ambazo anastahili kuwepo nyumbani ananiambia anakwenda kwenye mishemishe za kusaka pesa. Wakati mwingine namkubalia lakini imefika wakati naona ni ‘too much’.
“Yaani sina muda wa kukaa na mume wangu, siku ikitokea hivyo ni kwa muda mfupi sana hali inayonifanya niikose ile furaha ya kuolewa.”
Dada huyo aliongea maneno mengi lakini kwa kifupi utakuwa unaona ni kwa jinsi gani anajuta kuolewa licha ya kwamba anapata mambo mengine ya msingi.
Mapenzi si pesa, mapenzi si kumvalisha na kumlisha mkeo kila anachokitaka. Mapenzi ni ukaribu wa wewe kwake. Unatakiwa kujua kwamba, mumeo/ mkeo atajisikia faraja sana ukiwa pembeni yake pale atakapokuhitaji.
Ni jambo linaloumiza sana kwa mke kukosa muda wa kuwa na mume wake eti kisa ‘ubize’. ‘Ubize’ huu mpaka lini? Sikatai kuchakarika ndiyo maisha lakini ndiyo iwe kila siku?
Hiyo furaha ya ndoa itapatikana vipi ikiwa wanandoa wenyewe hawapati muda wa kuwa pamoja? Hili ni tatizo na kwa kweli tusipoangalia tunaweza kuwanyong’onyesha wenza wetu bila kujua na mwisho kuwafanya waumie kimoyomoyo.
Lakini cha ajabu ni kwamba, kama ilivyo kwa wanaume, wapo wanawake pia ambao wanajifanya wako bize sana na maisha kuliko kuzijali ndoa zao.
Yaani wao wanakutana na waume zao kwenye tendo la ndoa kwa masharti na tena kwa ratiba. Mapenzi gani haya? Mumeo anataka haki yake unamwambia umechoka!
Sasa kuna faida gani ya wewe kuolewa? Kama unahisi kazi ni bora kuliko kumjali mumeo, heri uwe muwazi kwake ili aoe mwanamke mwingine atakayejali hisia zake.
Kikubwa ninachotaka kusisitiza kwenye makala haya ni kwamba, kila aliye kwenye ndoa ahakikishe anatenga muda wa kutosha wa kuwa karibu na mwenza wake bila kujali ubize unaotokana na mishemishe za kimaisha.
Hii itaimarisha ndoa na hakika kila mmoja atafurahia uwepo wa mwenzake. Tukumbuke hakuna asiyetaka mwenza wake kujishughulisha kwani maisha bila kuwa bize hayawezi kuwa mazuri lakini sasa ubize huu ukizidi kiasi cha kumfanya mwenza wako akawa mpweke, inakuwa siyo poa.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.
GPL
No comments:
Post a Comment