LEO tufike kikomo cha mada yetu. Kuelekea kwenye hitimisho naomba niweke wazi kwamba hapa hatufundishani kuwa jeuri kwenye mapenzi, isipokuwa hili ni somo la kumjengea moyo wa ukombozi yule anayenyanyaswa kwenye mapenzi. Wanyanyasaji ni wengi, hivyo ni vema wadhibitiwe.
Lazima uwe makini kwa sababu hujui huyo anayekutenda malengo yake ni nini. Sasa basi, kama dhamira yake ni kukuumiza na unapomuonesha kwamba kweli umeumia, unakuwa umemfanya ajione amefanikiwa. Hii ndiyo sababu ya mimi kukutaka usikubali kuonesha udhaifu wake kwake. Atakwenda kuwakenulia wenzake.
Hata kama una moyo mdogo mpaka unaingia kwenye kundi la akina ‘mahaba niue’, hakikisha udhaifu huo rafiki mnafiki hauoni. Lia ndani peke yako, akitokeza jikaushe. Akikuuliza mbona macho mekundu mjibu kwamba ulikuwa umelala kisha tabasamu halafu mwambie, “usijali sweetheart, lete stori nyingine.”
Ni falsafa ya kukuwezesha kupata alama A kwenye mapenzi. Kama ambavyo kanuni inakwambia usimuoneshe adui yako udhaifu ulionao, ndivyo ambavyo na rafiki mnafiki unavyotakiwa kumkabili. Hakupendi, kwa hiyo siyo mtu mwema kwako, anakucheza shere, hana tofauti na adui.
Kwa faida yako, uimara wako kwa mwenzi ambaye haoneshi kukujali, unaweza kumbadili kutoka alipo hadi kuwa mpenzi bora wa maisha yako. Atabadilika pale tu atakapogundua kwamba wewe ni mtu makini na huhitaji kuchezewa.
Atabadilika pale atakapogundua kuwa wewe ni moyo wa chuma. Mwenye malengo ya kukucheza shere halafu akakutana na kisiki cha mpigo, humfanya afikirie mara mbili, fikra hizo humzalishia mawazo, anapokuwaza sana mwisho huumia. Unaona sasa, alitaka kukuumiza lakini kaumia yeye.
FAIDA NI IPI SASA?
Maumivu anayoyapata ndiyo yatakayomfanya ajirudi. Atakuheshimu na mwisho atakuonesha upendo wa dhati. Sasa wewe shika hili, anapoanza kukuonesha upendo, upime kwa umakini wake halafu jiridhishe kama kweli ana vigezo vya kumfungulia moyo.
Sikushauri ukimbilie kumuacha mpenzi asiyeeleweka, kwani inawezekana akawa ndiye mpenzi bora ila anasumbuliwa na tu na mapepe. Siku zote usilaumu uhusiano, tambua kwamba mpenzi mzuri atakupa furaha ya maisha na mpenzi mbaya ni changamoto ya kukupa uzoefu.
Kadiri atakavyokuona unajitambua ndivyo naye atakavyokuheshimu. Hebu mwache akwambie “I am sorry”, halafu mjibu kwamba hujamuelewa, kwa hiyo aende halafu arudi akiwa ana majibu ya kuridhisha ni kwa nini amekukosea. Muoneshe kwamba hutaki mchezo, kwani unaweza kumuacha wakati wowote kama hatakuheshimu.
Tabia ya unyonge kwa mpenzi wako, inaweza kumfanya akakuona wa bei rahisi mpaka akakutambulisha kwa mpenzi mwingine, akiamini huna la kufanya. Yupo ambaye alilazwa kitanda kimoja na mwanamke mwenzake, naye kwa sababu ni mahaba niue, akaogopa kumwacha mwanaume, eti anampenda sana.
Yupo mwanamke aliyemtambulisha mumewe kwa mwanaume wake mwingine, halafu mume badala ya kuchukua uamuzi, akakimbilia kulalamika kwa wakwe na mshenga. Jenga kitu kwamba unapolalamika sana, watu wanakuona dhaifu, hebu chukua uamuzi kwa ajili ya maisha yako ya leo na kesho.
KATAA KUWA MAHABA NIUE
Kila mtu anatakiwa ayaheshimu mapenzi. Hakikisha mwandani wako anakuwa upande wako kila siku. Mpenzi bora anapimwa kwa vitendo vyake. Je, anajali furaha yako? Anazingatia ujenzi wa maisha yako? Ni kwa namna gani anahakikisha unafurahi na anajengaje maisha yako?
Majibu chanya ya maswali hayo, yakupe sababu ya kuwa naye kwa moyo mkunjufu. Endapo uhusika wake hautakuridhisha, anza kutumia njia ambazo nimezieleza ili kumfanya akuheshimu. Siku zote unatakiwa ujiheshimu mwenyewe halafu na wengine ndiyo wakuheshimu.
Ukijionesha ni bei rahisi hakuna atakayekuona bei yako ni ghali. Hivyo basi, ukikubali kujionesha wewe ni mahaba niue, yatakuua kweli. Huyo utakayemlilia, hawezi kukuhurumia, badala yake utampa pointi ya kwenda kujisifu kuwa amekupata na umekamatika kwake huna ujanja wowote.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment