PENGINE kuna vitu unavyotegemea kuvisikia au kuvipata kutoka kwake lakini haujaambulia chochote. Kabla ya kukimbilia kumtoa kasoro kwamba hakufai, hebu jiulize mwenyewe, ni lini ulimwambia unachopenda kusikia kutoka kwake? Umetaka awe anakwambia anakupenda, je, wewe umemwambia unampenda mara ngapi?
Usidai kile ambacho wewe mwenyewe hutekelezi. Unataka mwenzi wako awe anaonesha hisia za juu pindi mnapokuwa faragha, je, wewe huwa unamuonesha hizo hisia? Utagundua kwamba wewe unadai kile ambacho hukitekelezi kwake. Pengine hakuoneshi kwa kuamini hupendi.
Upo kwenye uhusiano, inapita miezi mitano hujawahi kumtamkia mwenzi wako neno “nakupenda”. Siku moja unajitahidi, unajitutumua unamwambia mpenzi wako “nakupenda sana my sweet love”. Kutokana na ugeni wake, anakujibu “asante.” Sasa jibu lake linakukera nini?
Ingekuwaje kama ungemwambia hivyo halafu naye akakujibu “najua”, si ndiyo pangechimbika. Mapenzi yanahitaji moyo wa subira. Akikujibu “asante” au “najua”, chukulia kwamba yote ni majibu, unachotakiwa kufanya ni kumfanya mwenzi wako atambue jibu la kukupa ili uwe na furaha. Wengine haya mambo ni ‘mashokolo mageni’, kwa hiyo hawajazoea.
Unaweza ukafanya uamuzi halafu baadaye ukajutia, usiseme kwa heri kama unajisikia kuendelea, usiseme humpendi mtu tena kama unajua huwezi kumuacha aondoke . Hii ndiyo sababu ya kukutaka uishinde jazba. Amekuudhi leo, hebu lala kwanza ili kesho ulitafakari tukio ndiyo utoe uamuzi.
Kumbuka inachukua dakika kumuona mtu na kumtamani, ila baada ya huyo uliyemtamani, ukimuingiza ndani ya moyo wako na kumpenda, ni ngumu kumsahau. Wapo wanaoteseka maisha yao yote kwa kushindwa kuwaondoa kwenye vichwa vya wale ambao waliachana nao. Wengine, hugharimu kabisa maisha yao. Acha jazba, uamuzi wako wa hasira leo, unaweza kukutuma kubwia sumu. Mimi nimeyaona.
KIRUSI NO. 5, ULIMI
Chunga sana ulimi wako. Maneno yako yanaweza kumfanya mpenzi aliyekupenda kwa moyo mmoja, akimbie. Tamka maneno matamu kwake, siyo yake la kumkera. Hakuna adhabu kubwa kwa mtu kama kumsemasema. Atakukimbia tu.
Atajitahidi kukuvumilia kadiri anavyoweza lakini mwisho ataachana na wewe. Kwa hiyo ulimi wako unapaswa kuuchunga na kuuelekeza kutamka maneno mazuri. Siyo ugeuke kero na kumdhalilisha mpenzi wako. Ulimi wako unaweza kutoa picha wewe ni mtu wa aina gani.
Maneno mabaya unayotamka, yatatoa picha kwamba wewe ni kiburi, jeuri na usiye na heshima kwa mwenzako. Kama utafanikiwa kuudhibiti ulimi wako, utakuwa umefanikiwa kukishinda kirusi hatari mno kwenye uhusiano wako. Nakutakia kila heri kwenye maisha yako ya kimapenzi.
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment