Social Icons

Thursday 4 October 2012

LEO KATIKA MAHUSIANO:TUSIKATAE, KUNA WANAUME HAWARIDHIKI HATA WAFANYIWE NINI!



KATIKA ulimwengu wa mapenzi, kuna mambo mengi yanayowafanya baadhi ya watu wajute kupenda na hata kupendwa. Hii ni kutokana na sampuli ya watu ambao mara nyingi mioyo yetu hutokea kuwazimikia.
Tufahamu kwamba, kupenda ni suala linalotokea ‘automatikale’, yaani unajikuta ghafla umetokea kumpenda flani bila kujua kama naye anakupenda, ni laghai wa mapenzi au hana mpango kabisa na mambo ya mapenzi. 

Nasema hivyo kwa kuwa najua wapo wanaume ambao si watu wa kupenda, ukimshobokea unamalizana naye siku moja kisha kila mtu anachukua hamsini zake.
Lakini kwa wanaume hawa hawa, unaweza kukuta msichana anatokea kumpenda tena kuliko kawaida. Kwa kifupi msichana kutokea kupenda wanaume wa sampuli hii ni kujipa vidonda vya tumbo bure.
Nasema hivyo kwa kuwa, huwezi kupata lile penzi ulilotarajia na matokeo yake sasa maisha yako yanakuwa ni ya kumegwa na kuachwa.
Hata hivyo, mapenzi yanahitaji uvumilivu wa hali ya juu sana. Mapenzi ya dhati sasa hivi hakuna, usanii umekuwa ni mwingi na kusalitiana imekuwa si jambo la ajabu. 
Yaani unakuta mwanamke kwa mdomo wake anadiriki kusema kuwa, anajua mumewe atakuwa na kimada lakini kwa kuwa hamjui na mumewe anamheshimu, anampenda na kumpatiliza katika kila jambo, haoni sababu ya kuumia.
“Wanaume wa siku hizi ukiwafuatilia unajitafutia presha ya bure, mimi wangu kwa kuwa ananipenda, ananijali, ananiheshimu na ananipatiliza katika kila jambo, sina haja ya kumfuatilia kwani najua nikifanya hivyo utawabaini wake wenza wengi tu, ya nini kujikondesha?” anaeleza mama Husna wa Kinondoni jijini Dar.
Sitaki kuamini kwa asilimia 100 kile anachokisema mama Husna lakini ukweli unabaki kwamba, kuna baadhi ya wanaume hata wake zao wawafanyie nini, hawatosheki. 
Ukijaribu kufuatilia utabaini wanawake wengi wanajitahidi sana kuwapatiliza waume zao katika kila jambo wakijua kwamba kubweteka kwao ni kutafuta kusalitiwa.
Cha ajabu ni kwamba, licha ya jitihada za wanawake hao, bado kuna wanaume wamekuwa ni watu wa kubadili wanawake kila siku. 
Ukijaribu kufuatilia utabaini hata huko nje wanakoenda hakuna jipya, yaani ni tamaa zao za kijinga tu zinazowasukuma kuzisaliti ndoa zao bila kujua kwamba kuna madhara makubwa ya kufanya hivyo.
Kwa maana hiyo basi, wanawake ambao wako ndani ya ndoa wanatakiwa wajue kwamba, wapo wanaume ambao siku zote hawaridhiki na kuwagundua ni vigumu. 
Mke anaweza kukaa na mumewe kwa muda mrefu akijua anamdatisha sana kiasi kwamba anaamini hawezi kusalitiwa, kumbe mumewe huyu huko nje ana utitiri wa nyumba ndogo.
Kikubwa ni mwanamke kujitahidi kutimiza wajibu wake kama mke ikiwa ni pamoja na kuhakikisha anampa mumewe ‘mambo’ ambayo yatamfanya asiwe na sababu ya kwenda kwa wanawake wengine. 
Pale ambapo mwanamke atabaini kuwa licha ya kujitahidi kwake bado anasalitiwa, ajue ameingia kwenye penzi na mtu ambaye si sahihi hivyo uamuzi mzuri na unaofaa ni kujiweka pembeni kuepuka msongamano.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo.


www.globalpublishers.info

No comments: