Social Icons

Saturday, 6 October 2012

MAHABA NIUE NI MATOKEO YA KUKOSEA VIPIMO VYA MAPENZI - 4


Wiki iliyopita tuliishia pale tulipoanza kupeana mbinu za namna ya kuepukana na matokeo mabaya ya mahaba niue. Sasa tuendelee.
Akikuuliza kama una mtu mwingine anayekupa kiburi, naye mjibu kwa mtindo wa kurudishia swali, mwambie: “Kwani wewe unaonaje?” Kisaikolojia, anayeanza akijibiwa huwa anaumia mara kumi zaidi. Hii ndiyo sababu ukawepo msemo wa mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu.
Kwa maana alipokuwa anakutenda ndivyo sivyo, alikuona wewe ni nguruwe, kwa hiyo mkuki haukupi machungu, sasa unamchoma yeye binadamu ndiyo anahisi chungu ya maumivu yake. Endelea kukaza uzi mpaka atakapokulalamikia maumivu anayoyapata kutokana na vitendo vyako.
Sababu ya kufanya hivyo hapa ni kwamba utakapombadilikia, kama hakupendi, isipokuwa alikuona wewe ni mtu wa kukuchezea shere na kuondoka zake, basi kwako atakuta wewe ni imara kuliko chuma cha pua, kwa hiyo atatafuta haraka njia ya kupita.


Ikiwa alikuwa anakupenda ila akawa anakufanya zumbukuku. Vitendo vyako vitamtesa mno. Atatamani akae na wewe mzungumze. Hata baada ya mazungumzo yenu na ikiwa utakubali kumfungulia moyo ili muishi kwa upendo, siku nyingine hatarudia kukufanya wewe zoba.
Atakuheshimu na kuthamini hisia zako kwa maana utakuwa umemuonesha kwamba wewe ni mtu unayejitambua. Si wa kupelekwapelekwa kama bendera isivyotulia wakati wa upepo. Utulivu wako kiakili na kiuamuzi, vitakuokoa katika mdomo wa mpenzi mbaya.
Hata ukiwa kwenye ndoa, tabia za mwenzi wako zisikupe ukichaa, ukawa mahaba niue. Badala yake wewe unatakiwa ubadilike kutoka huko anapokuona mwepesi. Mpe sababu ya kukuheshimu. Akuone mzito, uliye na thamani kamili. Busara zako zitamgeuza kuwa mwenzi bora wa maisha yako.
Tambua kwamba hawezi kukuheshimu ikiwa humpi sababu ya kufanya hivyo. Ikiwa kila anapokutenda unamlilia halafu akisema, “I am sorry baby”, unasahau yote na kumfungulia moyo wako, lazima atakuona huna thamani. Kwa maana ulivyo, inatokana na uamuzi wake mwenyewe.
Akitaka ukose raha, ni yeye anaamua. Akiamua ulie au utabasamu, inatokana na jinsi yeye atakavyowasiliana na wewe. Inapokuwa hivyo, usishangae sana anapokuona wewe ni ‘kitenisi’ cha kudundadunda. Anakudundadunda anavyotaka, ni kosa kubwa kumruhusu mpenzi wako akuchukulie hivyo.
Kadiri atakavyokuona unajitambua, ndivyo naye atakavyokuheshimu. Hebu mwache akwambie, “I am sorry”, halafu mjibu kwamba hujamuelewa, kwa hiyo aende halafu arudi akiwa ana majibu ya kuridhisha ni kwa nini amekukosea. Muoneshe kwamba hutaki mchezo, kwani unaweza kumuacha wakati wowote kama hatakuheshimu.
Tabia ya unyonge kwa mpenzi wako, inaweza kumfanya akakuona wa bei rahisi mpaka akakutambulisha kwa mpenzi mwingine, akiamini huna la kufanya. Yupo ambaye alilazwa kitanda kimoja na mwanamke mwenzake, naye kwa sababu ni mahaba niue, akaogopa kumwacha mwanaume, eti anampenda sana.

Itaendelea wiki ijayo

www.globalpublishers.info

No comments: