Social Icons

Tuesday 4 December 2012

LEO KATIKA MAHUSIANO: MAPENZI NI MAISHA, KUISHI KIMAPENZI KUNARAHISISHA MAENDELEO

MIGOGORO mingi itaondoka, familia nyingi zitakuwa imara, watoto wa mitaani watapungua kama siyo kwisha kabisa, kadhalika vitendo vya watu kutesana nyoyo, vitaadimika.
Sote tutakubaliana katika ukweli kuwa nafsi ya kwanza hutangulia kabla ya kufuata ya pili. Hiyo ndiyo imechochea tofauti za sasa. Kila mtu anakuwa anajijali mwenyewe bila kujua kwamba uhusiano wa kimapenzi na familia hauendi hivyo. Katika mapenzi hakuna masilahi binafsi.
Nguvu, elimu na maarifa ni vyako ila ukishavitumia kuingiza fedha zinakuwa si zako tena. Zinakuwa za familia yako. Endapo utakuwa na nidhamu binafsi kwenye kutumia, utakuwa umeushinda ubinafsi. Hebu anza leo kupambana na ubinafsi kwa ajili ya maisha yako.
SHINDA UBINAFSI, KOMESHA USALITI
Kama nilivyotangulia kueleza, kipengele cha usaliti kinachangiwa na ubinafsi. Kwamba mtu anajiona penzi ni lake, kwa hiyo anaweza kuligawa. Hayo ni makosa makubwa mno. Ukishaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, unakuwa umeingia mkataba usio na maandishi wa kukabidhi penzi lako kwa mwenzako.
Viungo vipo kwenye mwili wako lakini kwa mazoea tu. Anayevimiliki ni huyo uliyeingia naye mkataba wa kupendana. Hii ndiyo sababu anakuwa na haki ya kukudai pale anapobaini umemsaliti, vilevile nawe unakuwa na hoja za nguvu, unapomlalamikia usaliti wake.
Umekutana na kishawishi, unatamani kuvunja ile amri ya katazo la zinaa. Kabla ya kufanya chochote, vuta fikra kwamba penzi ni la watu, si lako. Ulishakubaliana naye kuwa mtakuwa mnapeana ninyi wawili tu. Ukifikiria kwa undani zaidi, utamwambia aende zake.
Kabla ya kutenda dhambi ya usaliti, hebu fikiria kwamba naye anakusaliti muda huo. Vuta picha kama ni tukio la kweli pale mwenzi wako akiwa hana staha yoyote, yupo faragha na mtu mwingine wanakusaliti. Kama utavuta picha na kujaza hisia za kweli, utaona namna inavyouma.
Kama wewe inakuuma, tambua na mwenzako itamuuma vilevile pale atakapogundua umemtenda. Usikubali mpenzi wako aumie, pia usijivalishe tabia chafu ambazo zitakufanya uwe ni mtu usieaminika kwenye jamii. Ukiwa msaliti, unasababisha aibu nne.
Mosi; Utamtesa mwenzi wako ambaye una mkataba naye. Kwamba mlishakubaliana kuwa penzi ni lake peke yake, ila wewe umeligawa.
Pili; Utamuaibisha mwenzi wako. Tamaa yako inamfanya ashindwe kutembea kwa kujiamini. Wewe ndiye unayeweza kumfanya atembee kifua mbele kila anapokwenda. Thamani na heshima yake vinatoka kwako lakini umeviharibu.
Tatu; Ni aibu yako mwenyewe. Unaweza kufanya usaliti wako faragha lakini mitaani kila mtu anajua wewe ni kicheche. Kuna mafumanizi ya aina mbalimbali. Utashindwa kuheshimika kwa sababu ya tamaa ya muda mfupi.
Nne; Utachochea aibu kwa kizazi chako. Una mtoto au watoto, hata kama huna basi kesho utakuwa nao. Elewa kwamba uchafu wako wa leo, utamkosesha amani mtoto wako kesho. Hisia na tamaa zako za kibinafsi, zisiwaaibishe wanao.


MFANO HUU UKUJENGE
Idrisa ni mfanyabiashara anayejitosheleza kwa sasa. Mungu amemjaalia kutimiza ndoto zake. Umaskini wa familia yake, umebaki historia, kwani juhudi zake zimeweza kuwakomboa hata wadogo zake. Pamoja na kufanya biashara za kusafiri nchi mbalimbali pia Idrisa anamiliki supermarket kadhaa jijini Dar es Salaam na Mwanza.
Wakati anafanya kazi zake, hajui kama kuna mzee anayeitwa Mataba ambaye hujisifu kwamba yeye ndiyo chachu ya yeye kufanikiwa. Mataba anasema hata nauli ya Idrisa kwenda shule, ilikuwa inatoka kwake. Mataba anadai alikuwa anamhudumia Idrisa kwa sababu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mama yake.
“Yule Idrisa amesoma kwa jasho langu. Nilikuwa natembea na mama yake, namhonga fedha ndiyo akawa anapata fedha za kumsomesha, hata mama yake aje hapa nitasema,” hizo ni tambo za mzee Mataba.

Itaendelea wiki ijayo.

www,globapublishers.info.

No comments: