Social Icons

Friday, 4 January 2013

LEO KATIKA MAHUSIANO:MFANYE MPENZI WAKO ASAHAU MAUMIVU YA MWAKA JANAKWANZA kabisa namshukuru Mungu kuweza kunifikisha salama mwaka 2013 nikiwa na afya njema. Nina imani hata wewe msomaji wangu ambaye leo umeshika gazeti ukipitia mada ya kwanza ya kufungua mwaka upo salama.

Natumia nafasi hii kuwaombea wote walioingia mwaka huu wakiwa wagonjwa na ambao walitaka kufika lakini Mungu aliwapenda zaidi wakaishia mwaka jana. Naungana na watu wote kumlilia rafiki yangu Sajuki aliyetangulia juzi mbele ya haki, Mungu ampe mapumziko mema.
Leo napenda kuzungumza na wapenzi wangu wa kona hii ambao nimekuwa nao mwaka mzima katika kufuatilia mada zangu. Mwaka umekwisha umejifunza nini? Je, kupitia kona hii matatizo yameondoka , yamepungua au yameongezeka?
Nimeandika mada nyingi ambazo zimewagusa watu wengi. Ujumbe wenu na simu mlizopiga zinaonyesha jinsi kona hii inavyosomwa na watu wengi, tena makini.
Kwa vile tunauanza mwaka, basi napenda kuwapa ‘homework’ ya kufanya utafiti kuhusiana na mwenendo mzima wa maisha yenu ya kimapenzi. Huu ndiyo muda muafaka wa kujichambua mwenyewe ulibeba vipi uhusiano ndani ya penzi lako.

Katika muda wote kulikuwa na migongano, je, chanzo chake nini? Kama ni wewe ni muda wako wa kujirekebisha ili usiwe chanzo cha matatizo ya kila siku.
Ni makosa mtu kurudia kosa moja kila mara, mwanadamu anayejitambua hujifunza kupitia lile linalokemewa sana na mwenzake, japokuwa unapenda kulifanya.

Sifa kubwa ya mwanadamu ni kufikiri kabla ya kutenda, siku zote mapenzi ni kusikilizana, kufarijiana na kubembelezana. Bila shaka mwaka uliopita kuna mambo yalitokea hadi kufikia hatua ya kutishia kuvunja ndoa au uhusiano wenu.
Mwaka umeisha, umekaa na kujiuliza tatizo nini? Umejichunguza na kujua labda wewe ndiye chanzo?
Mmeukaribisha mwaka, mmekaa kama wanandoa au wapenzi kumaliza tofauti zenu ili kuuanza mwaka nanyi mkiwa wapya?

Kama hamjakaa kujadili mwenendo mzima wa uhusiano wenu kwa mwaka mzima hamjachelewa. Hebu kupitia makala haya kaeni chini na kuchambua matatizo yote yaliyowakwaza sana.
Tafuteni sehemu tulivu ili kupata nafasi ya kuzungumza kwa kujiamini. Sehemu hii haitakiwi mmoja kujiona yupo juu ya mwenzake au ubishi kwa kile ambacho kimemgusa.

Mazungumzo yenu yawe ya kirafiki, kosoaneni kwa sauti za kawaida, ondoeni jazba kwani muda huo haina nafasi. Uwe mwepesi kukubali kosa na kuomba msamaha. Kwa vile nia yenu ni kujenga, hakikisheni yote yaliowakwaza mwaka uliopita hamyapi tena nafasi.
Jiepusheni kuwa chanzo cha maumivu ya wenzenu, umeamua huyo awe wako wa kufa na kuzikana kwa nini muumizane? Sawa, mwanadamu ana upungufu, basi makosa yako yasiwe mazoea kwa vile tu upo juu ya mwenzako. 

Mapenzi hayaangalii cheo, fedha wala uzuri wa sura na umbile, bali kujitoa kwa ajili ya mwenzako.
Jutia makosa uliyofanya mwaka jana na kutokuwa tayari kuyarudia, hii itakufanya mwaka huu uwe makini sana na kumfanya mpenzi wako asahau maumivu ya mwaka jana. Muahidi mpenzi wako kuwa mwaka huu utakuwa sehemu ya furaha yake ya kila siku, kama utakwenda tofauti basi utakuwa msaliti.
Kiapo hiki si cha mtu mmoja bali kiwe cha wote. Kama kweli unayoyasema yanatoka moyoni na kuwa tayari kutorudia yaliyomkwaza mwenzako mwaka jana, basi mwaka huu utakuwa wa furaha na amani. Nakutakieni mwaka mpya wenye mapenzi ya dhati, kila mmoja awe sehemu ya furaha ya mwenzake.

No comments: