UKWELI ambao haukwepeki kuhusu uhusiano na mapenzi ni uwepo wa furaha,
amani na maelewano. Hivi ni vitu muhimu sana. Msingi wa yote ni pendo la
dhati. Ikiwa wapendanao wana upendo wa kweli toka mioyoni mwao ni
rahisi kutunza vitu hivyo.
Hakuna asiyependa kuwa na uhusiano wenye furaha na amani. Uhusiano wenye
masikilizano huzaa matunda mema – kama ni marafiki tu, basi ujue ndoa
inanukia lakini kama tayari ni wanandoa, maana yake mafanikio ndani ya
nyumba yatakuwa rahisi kupatikana.
Marafiki katika yote hayo, inategemewa zaidi na namna wahusika
wanavyoendesha uhusiano wao; kwa maana kwamba, yote yanahitaji
ushirikiano wa wote. Hapo ndipo mwanzo wa matatizo. Wenzi wawili huwa na
tofauti za hulka.
Kwa wanawake, wengi hupenda sana kufuatilia na kuhakikisha uhusiano
unakuwa imara. Likitokea tatizo, mwanamke huwa mstari wa mbele
kulishughulikia ili mambo yaishe. Wanawake wengi hawapendi kuwa
wamewaudhi wenzi wao.
Ikitokea
wakiona kuna tofauti ya kimawasiliano, mara moja husaka mbinu za
kutatua na kubakisha uhusiano ukiwa kwenye hali nzuri. Hiyo ni tofauti
na wanaume ambao mara nyingi wao ni watu wa harakaharaka.
Ni wepesi wa kusahau mambo au kuyachukulia kwa wepesi. Mfano, mwanamke
wake akikasirishwa na jambo fulani, ni rahisi tu kuishia kusema:
samahani. Wakati mwingine anaweza asiseme kabisa, akijua mambo
yameshaisha. Wanawake ni tofauti. Wanafanya mambo yao kwa taratibu sana.
Hasira zao zinachelewa kuisha, lakini ni rahisi zaidi kuzimaliza kwa
kumwambia tu: nakupenda mpenzi, najua nimekosea, samahani mama.
Ni sentesi fupi sana lakini kwao ina maana na thamani kubwa sana.
Mapenzi ni sawa na bustani, wakati mwingine inahitaji kumwagiliwa na
kuwekewa mbolea. Kama ni kweli unampenda, tuliza akili na muda wako
kuhakikisha furaha yake inaendelea kuwepo.
Inamaanisha kuwa, upendo wake kwako ukitamalaki muda wote – mafanikio ya
kazi ya mikono yako yapo jirani tu. Mfanye mwanamke wako atabasamu.
Pamoja na ubize wako, tenga nafasi kidogo kwa ajili yake.
MSAMAHA SI KUJISHUSHA!
Wanaume wengi wanaamini kumwambia mwanamke samahani ni kujishusha na
kuwa chini yake, si hisia sahihi. Msamaha ni uungwana. Kama kweli
unampenda kwa dhati, una shaka gani kumwambia akusamehe ili uhusiano
uendelee kuwa wenye nguvu?
Hutapungua mahali popote kukubali kosa, ikiwa umekosea au kumrekebisha
mwenzako badala ya kubaki bubu huku ukiwa umenuna na kusitisha baadhi ya
huduma. Kama ilivyo kwako, tambua kuwa mwanamke naye ni binadamu,
anaweza kufanya makosa lakini asijue!
Kumwambia kwa upole ni jambo zuri. Atakusikiliza, atakuelewa na atajirekebisha alipokosea. Kukaa nalo moyoni hakuna maana.
UBABE SIYO MPANGO
Wapo baadhi ya marafiki wanaamini kuwa ubabe ni sehemu ya ukamilifu wa
uanaume. Siyo kweli. Huna sababu ya kuwa mkali sana au mwenye amri muda
wote. Mwanamke anahitaji kubembelezwa, upendo na kuonyeshwa namna
anavyothaminiwa.
Wengine wana tabia ya kuwapiga wenzi wao, kitu kidogo tu, tayari kipigo.
Vipi akikutana na mkarimu, asiyepiga na anayebembeleza? Akiachana na
wewe utamlaumu nani? Ni kweli kuna wakati mwanamke anahitajika
kukaripiwa akikosea, lakini si sawa kuwa mkali kupitiliza wakati wote.
Wiki ijayo tutamalizia mada yetu, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia
Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha
Maisha ya Ndoa.
CHANZO GPL
No comments:
Post a Comment