Social Icons

Monday, 5 May 2014

LEO KATIKA MAHUSIANO: UNAFAHAMU UCHAWI WA NENO SHUKURANI KATIKA MAPENZI? SOMA HAPA UJUE NA ULITUMIE IPASAVYO

KATIKA mapenzi, hili neno halitakiwi kuishia mdomoni, lazima liishi ndani ya nyoyo za wapendanao. Hapo ndipo unaweza kuona maana yake. Linarahisha suluhu pale wahusika wanapotofautiana, kadhalika ni chachu ya kuepusha shari, hapohapo ni grisi inayolainisha moyo na kukuza uvumilivu.

Shukurani ni zaidi ya kumwambia mwenzi wako ‘asante’ pale anapokufanyia kilicho bora au kukununulia zawadi. Yafanye maisha yako yawe ya shukurani na uhakikishe unamwambukiza mwenzi wako awe hivyohivyo, baada ya hapo utajionea matunda ya penzi linaloitwa la kushibana.

SHUKURANI NI KURIDHIKA!
Hapa ndipo kwenye ukweli! Ikiwa utashukuru kutoka moyoni kwa kumpata mwenzi wako uliyenaye, matokeo ya juu kabisa kutenda kila lililo jema na kumfurahisha mwandani wa maisha yako. Na hivyo ndivyo kila mmoja anatakiwa ahusike kwa mwenzake.

Mapenzi ni mchezo wa kuchukua na kutoa, kwa maana hiyo unavyohusika kwake ndivyo naye anapaswa kuwajibika kwa ajili yako. Hivyo, anatakiwa kushukuru kwa kukupata na kutenda kila kinachowezekana kukufanya uwe mwenye furaha siku zote za uhai wa penzi lenu.

Uaminifu ni shida, usaliti ni kansa kwenye mapenzi. Uhusiano na ndoa nyingi, zinasumbuliwa na ugonjwa huu. Mtu kumzunguka mwenzi wake na kwenda kugawa ‘heshima’ ya mwenzio kwa mwingine. Kuna nyakati mtu anaamua kumkimbia kabisa mwenzie. Ni vijimambo vya mapenzi.

Ukweli ni kuwa tafsiri ya juu kabisa ya usaliti ni zao la mambo mawili. Mosi, dharau, na pili ni kukosa shukurani. Usizungumze kuhusu tamaa kwa sababu yenyewe inadhibitiwa kirahisi kama tu mtu husika atamheshimu mwenzi wake ana atakuwa anaridhika naye.

Ni dharau kwa sababu umehisi na umeona ama hakufai au hatajua udanganyifu wako. Kwamba hakufai au lugha rahisi zaidi ni kuwa hakutoshelezi ndiyo maana ukautoa utu wake kwa mwingine. Mapenzi ni utu, ndiyo maana wanasema heshima ya mke ipo kwa mumewe, na ya mume kwa mkewe.
Ufafanuzi wa msemo huo ni kuwa kama mke atakuwa waluwalu/mapepe, moja kwa moja mumewe atavuna dharau ya hali ya juu mitaani. Vitendo vya mkewe ndivyo vitakavyokuwa vinamfanya adhalilike. Vivyo hivyo, mume akiwa mchafuzi, mke hataheshimiwa.

Katika hili, ndiyo maana kukawa na msisitizo wa hali ya juu kwamba omba sana Mungu kwa sababu peke yako huwezi, ili upate mwenzi sahihi wa maisha yako. Waswahili wanasema kuwa heri upotee njia wapo wasamaria wema watakuelezeza lakini ukipotea kuchagua mke au mume, hilo ni janga lako la maisha.

Kwa vyovyote vile, kuwaza hatajua au kuona hakufai ni dharau. Mweleze mwenzi wako kama unadhani hakufai ili ikiwezekana muachane kistaarabu kuliko kumfanyia vitiko na kumuumiza bila matarajio. Ukifanya hivyo kwenye ndoa ndiyo balaa zaidi. Chunga nyendo zako.

Kuhusu kukosa shukurani hapa ndipo kwenyewe, kwani ndiyo msingi unaobeba mada yetu hii. Mtu anayekosa shukurani, ni yule mwenye tamaa, asiyeridhika, mbinafsi, mlafi, mtaka vyote na maneno mengine yanayofanana na hayo. Ongezea msemo wa tahadhari kwamba mtaka vyote kwa pupa, hukosa vyote.

Kwanza jiulize, huridhiki na mwenzi wako kwa lipi ambalo umekosa? Kwa hicho unachohisi hukipati, ni kwa nini usikae na mwenzi wako mkazungumza ili msaidiane kufanya masahihisho? Je, kwa huyo unayekwenda kumsaliti, ndiko unakohisi utatimiziwa kila kitu? Una uhakika gani?

Shukuru kwa kile ambacho unakipata kwa mwenzi wako, mengine ni majaliwa! Ukishukuru kutoka moyoni, maana yake utakuwa umeridhika naye. Unapotosheka naye, maana yake ni kwamba hata aje nani, hutashtuka. Nakuomba ujifunze kushukuru kutoka moyoni, itakusaidia sana!

HOJA YA KITAFITI; Wanaume na wanawake ambao huamua kuchepukia njia za pembeni, si kwamba hawatosheki na njia kuu.

GLOBAL PUBLISHERS

No comments: