Social Icons

Wednesday 25 June 2014

LEO KATIKA MAHUSIANO: USILIE, ACHA KUJIUMIZA, MAPENZI HAYATAKIWI KUKUTESA!-2 ACHA KULIA LIA KAMA MUVI ZA KIHINDI SOMA HAPA CHUKUA HATUA!

WAKATI mwingine maumivu ya mapenzi huwa ni ya kujitakia. Kama mtu ukijua vyema kuhusu mapenzi, kwa hakika mateso yatakaa mbali na wewe. Kikubwa ni kuwa tayari kujifunza na kuchukua yale yanayoonekana yanafaa.

Wiki iliyopita nilianza kwa kuelezea kisa cha Ben na Lucy. Naamini ulijifunza kitu kupitia kisa hicho. Sasa hebu tuangalie kisa kingine cha msichana niliyempachika jina la Amina halafu tutajifunza kitu.

Amina akiwa darasa la sita tayari alishaanza mambo ya mapenzi, mpaka anafika kidato cha tatu alikuwa ameshatembea na wanaume zaidi ya ishirini! Hakufanikiwa kufanya mtihani wake wa mwisho wa kidato cha nne kwa sababu aligundulika ana ujauzito wiki chache kabla ya mtihani huo, mwisho wa masomo yake ukawa hapo.

Alivyojifungua akaanza kufanya kazi ya kuuza genge na kwa bahati mbaya mwanaye hakuwa na baba, maana hakujua mimba ni ya nani na kati ya wanaume watatu aliowashuku kuwa wanaweza kuwa ni mimba ya mmoja wao, alipowafuata walimfukuza!

Baadaye Amina aliamua kutulia na kwa bahati nzuri akapata mpenzi mwingine ambaye alitulia naye akiamini anaweza kufuta machungu yake katika historia yake ya mapenzi, cha ajabu sasa baadaye akaachika!

Akatafuta bwana mwingine akawa naye na kuachwa. Amina sasa ana miaka 27 lakini ana watoto wanne na kila mmoja ana baba yake. Maisha yake siyo mazuri na chanzo kikubwa hapo ni mapenzi. Anajilaumu kujiingiza katika mapenzi ya utotoni. Maisha yake ni ya kubangaiza akiwa hana uhakika wa kupata mlo wa siku inayofuata.
Bila shaka kuna kitu umejifunza hapo.

MWANZO ULIKUWAJE?
Visa hivi vinatoa mwanga hakika katika maisha yetu ya kimapenzi. Vina mafunzo makubwa sana.
Lakini kuna wengine hukumbwa na mateso ya mapenzi siyo kwa makusudi bali mazingira ndiyo yanayosababisha.

Katika maisha yako ni vyema kuwa makini sana na ahadi za wapenzi, siku zote chunguza kauli za mwandani wako, tumieni muda mwingi kuchunguzana.
Matapeli wa mapenzi siku hizi ni wengi, mtu anajifanya anakupenda kumbe hakupendi wewe bali anapenda kitu fulani ulichonacho na siku kikitoweka mwisho wa mapenzi yenu unakuwa umefika.

Kwa nini uweke maisha yako rehani? Kwa nini ujilaani kuwa eti huna bahati ya kupata mpenzi wa kweli? Nasema hivyo kwa sababu kuna baadhi ya wasichana huamua kumkubali kila mwanaume kwa madai kuwa anaogopa kuacha bahati!

Akitongozwa na mwanaume mchana, jioni wanakutana beach na usiku wapo kitandani wanafanya mapenzi.

Ukiwauliza wanadai eti wanaonyeshana mapenzi ya dhati! Mapenzi ya dhati ya aina hiyo yameanzia wapi? Kwa nini ukubali kumpa mtu uhai wako kwa kukutana kwenu siku moja?

Kama uliwahi kupitiwa kwa kufanya hivyo acha kabisa kuanzia leo na kamwe usijaribu kurudia tena.
Mapenzi ya kweli yapo, siku ikifika utakutana na yule maalum kwa ajili yako na wala hutakuwa na kazi kubwa ya kugundua kuwa anakupenda au anakutamani kwa sababu matendo yake yataonekana wazi kuwa anakupenda.

Unapoingia katika uhusiano wa mapenzi lazima uwe umejipanga vilivyo kwa ajili ya kukabiliana na kila kitu kilichopo ndani yake. Inawezekana kabisa kuepuka mateso katika maisha yako.
Kuna mambo machache ya kumalizia ili upate kuelewa vyema somo hili, wiki ijayo nitakuwa hapa katika sehemu ya mwisho, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.

GPL

No comments: