Social Icons

Wednesday 20 January 2016

SERIKALI YAKANUSHA UZUSHI UNAOENEZWA KATIKA MITANDAO YA KIJAMII KUMHUSU RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Ikiwa unataka tengenezewa Blog, Tukiko lolote la Harusi,Msiba, Mahafali, Tamasha, Matangazo auHabari yoyote usisite kututumia kupitia whatsapp 0765056399 au Barua Pepe fredynjeje@live.com. Follow me instagram @officialfredynjejeblog Twitter @Fredynjeje



Hivi karibuni kumejitokeza uzushi unaosambazwa katika mitandao ya kijamii ya ndani ya nchi na nje ya nchi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amefukuza wageni kutoka nje waliokuwa wanafanyabiashara zao nchini kwa kuwa serikali yake haitaki wageni kufanya biashara nchini.


Serikali haijafukuza wageni kutoka nje ya nchi kufanya biashara nchini na haina mpango wa kuwafukuza wageni wanaoishi nchini kwa vibali vilivyotolewa kisheria na Idara ya Uhamiaji.

Uzushi huo usiokuwa na ukweli umeenezwa kufuatia Idara ya Uhamiaji kutekeleza jukumu lake la kufuatilia wageni wote wanaoishi nchini bila vibali halali vya ukaazi ambapo kwa mwezi Novemba na Desemba mwaka 2015 wageni 372 walioondoshwa nchini.

Kazi ya kufuatilia wageni wanaoishi nchini bila vibali halali vya kisheria haijaanza katika Serikali ya Awamu ya Tano. Idara ya Uhamiaji nchini tangu Januari hadi Desemba mwaka jana iliondosha nchini jumla ya wageni 1,642 waliokuwa wanaishi na kufanya shughuli zao nchini kinyume na Sheria.

Uzushi unaoenezwa hauna ukweli wowote na hauna nia njema na nchi yetu kwani kati ya mwaka 2014 na 2016 Idara ya Uhamiaji imetoa vibali vya ukaazi (Residence Permits) 40,765 kwa wageni wawekezaji na wafanyabiashara, wageni wanaofanyakazi za kuajiriwa, wageni wanaokuja kwa ajili ya Masomo, matibabu, dini, utafiti na wastaafu kuishi na kufanya shughuli zao nchini.

Serikali inawakaribisha wageni kuja nchini kuwekeza na kufanya shughuli zao kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.

Aidha, kuna uzushi unaenezwa kuwa Rais Dkt John Pombe Magufuli amepiga marufuku wanawake kuvaa nguo fupi kama njia ya kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.

Mheshimiwa Rais tangu aingie madarakani hajawahi kuagiza wala kutoa tamko kuhusiana na uzushi wa kukataza uvaaji wa nguo fupi ili kupunguza maambukizi ya Ukimwi kama inavyoenezwa katika mitandao ya ndani na Nje ya Nchi ambayo inanukuu habari hiyo kuwa imeandikwa na Gazeti la Kenya “The Standard”

Serikali inapenda kuutangazia umma kuwa uzushi huo unaomhusu Mheshimiwa Rais Magufuli umetungwa na watu wasioitakia mema nchi yetu kwa lengo la kumdhalilisha Rais na hauna ukweli hivyo watu wasishiriki kuueneza kwa njia yeyote ile.

Serikali kupitia balozi zake za Kenya na Afrika Kusini zinafuatilia chanzo cha uzushi huu kuhusu Rais Magufuli kwa kushirikiana na nchi husika na watakaobainika kutunga na kueneza uzushi huu watachukuliwa hatua za kisheria.

No comments: