Social Icons

Wednesday 2 March 2016

UMILIKI WA ARDHI KWA WANAWAKE WAONGEZEKA - ELUKA KIBONA


Meneja utetezi wa Oxfam Tanzania, Eluka Kibona


Meneja utetezi wa Oxfam Tanzania, Eluka Kibona amesema uelewa wa wanawake katika kumiliki ardhi na kufuatilia haki zao za ardhi unaongezeka siku hadi siku nchini na kuondoa ile dhana kwamba wanawake wako nyuma katika shughuli za maendeleo.



Bi Eluka ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Blogs za Mikoa kuhusu namna taasisi binafsi zinavyotetea harakati za wanawake katika kumiliki ardhi hapa nchini na kujiendeleza kiuchumi ambapo amesema kwa kulinganisha miaka 10 iliyopita na sasa, wanawake kwa sasa wamekuwa na muamko zaidi wa kupambana na changamoto za umiliki wa ardhi wanazokutana nazo.



''Sisi tunaunga mkono harakati na jitihada za kuleta usawa kati ya wanaume na wanawake mjini na vijijini na hii ni baada ya kutambua kuwa matatizo ya umiliki wa ardhi kwa wanawake wa mjini na vijijini yako sawa kutokana na mfumo ulivyo katika jamii.''Ameeleza Bi Eluka.


Mmoja wa wanawake (Kulia) akipokea hati yake ya kumiliki ardhi kutoka kwa Mkurugenzi Mkazi wa Oxfam Tanzania Jane Foster katika kijiji cha Gongoni wilayani Kilosa.


''Kuna madai ya ardhi ambayo wanawake wanakumbana nayo katika jamii kwa kudhulumiwa na wengine kwa kunyimwa haki zao za msingi hivyo tunawasaidia katika kuwawezesha kutambua namna ya kupigania haki zao.''Amesisitiza Bi Eluka.



Kuhusu siku ya wanawake duniani ambayo huazimishwa kila Machi 8 kila mwaka, Bi Eluka amesema Oxfam Tanzania imejipanga kufanya maadhimisho katika mkoa wa Mtwara ili kuunga mkono jitihada za wanawake katika kujikwamua na mifumo kandamizi hapa nchini na kujiendeleza kiuchumi.

Mmoja wa wanawake akiwa katika kilimo
 

Kwa mujibu wa Bi Eluka, Oxfam imewezesha wanawake wengi kuweza kupata haki zao katika mikoa mbalimbali nchini na baadhi ya mikoa hiyo ni Shinyanga, Arusha, Tanga Morogoro.



Aidha kwa mujibu wa sheria ya ardhi inatamka bayana kuwa mwanamke ana haki sawa na mwanaume katika kupata, kumiliki, kutumia na kugawa ardhi. (Kifungu 3(2) cha sheria ya ardhi na sheria ya ardhi ya vijiji za 1999).



Hata hivyo ni muhimu kila mmiliki wa ardhi awe na hati/ cheti halisi cha hakimiliki kuthibithisha haki yake ya kumiliki ardhi kisheria.

No comments: