Social Icons

Monday, 28 November 2016

Waziri Ummy mgeni rasmi maadhimisho ya siku 16 kupinga ukatili wa kijinsia

Ikiwa unataka tengenezewa Blog, Tukiko lolote la Harusi,Msiba, Mahafali, Tamasha, Matangazo au Habari yoyote usisite kututumia kupitia whatsapp 0765056399 au Barua Pepe fredynjeje@live.com. Follow me instagram @fredynjejephotography Twitter @Fredynjeje
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alikua mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika siku ya Ijumaa jijini Dar es salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Ummy alisema serikali ya awamu ya tano imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba watoto wanapata elimu salama bila aina yoyote ya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutoa elimu bora na ya bila malipo. "Lengo kuu la elimu bila malipo ni kuhakikisha kuwa watoto wetu hususan wa kike wanapata fursa ya kwenda shule kusoma na kufikia ndoto zao katika maisha."
Aidha alitoa wito kwa wadau na serikali kwa ujumla kutumia nafasi zao kupinga vitendo vyote vya udhalilishaji na ukiukwaji wa haki za binadamu vilevile kwa jamii kuwa na malezi bora na kuzingatia maadili kwa watoto na vijana wetu.
Naye Mkurugenzi wa shirika la WiLDAF nchini Tanzania, Dr. Judith Odunga alisema; "Ukatili dhidi ya wanawake na watoto umeendelea kuwa kikwazo kikubwa hapa nchini kwetu na hivyo kukwamisha juhudi za serikali katika kufikia usawa wa kijinsia na kupunguza umaskini."
"Utafiti wa UNICEF unaonesha kwamba watoto 3 kati ya 10 wa kike na mtoto 1 kati ya watoto 7 wa kiume wenye umri kati ya miaka 13 - 24 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kingono. Aidha, asilimia 6 ya watoto wa kike wamelazimishwa kufanya tendo la ngono kabla ya miaka 18." Aliongeza.
Aidha alisema; "WiLDAF na wadau mbalimbali wanaopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia wanaitaka serikali kufanya yafuatayo; Kufutwa kwa adhabu ya viboko mashuleni na walimu kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala. Kuboresha miundo mbinu rafiki kwa watoto wa shule ikiwa ni pamoja na  kuwepo kwa vyoo bora, mabweni, madawati, usafiri, uzio kuzunguka shule na mengineyo kwa ustawi wa watoto wa shule."
"Kuunda mabaraza yatakayokuwa yanasimamia malalamiko ya wanafunzi mashuleni. Kuboresha vifaa vya usafi. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Wizara ya sheria na Katiba zitunge sheria ya kudhibiti Ukatili Majumbani na kubadilisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuolewa, ama kwa ridhaa ya wazazi, mlezi au Mahakama." Aliongeza.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wageni mbalimbali wakiwemo wageni kutoka shirika la UN Women, Balozi wa Ireland nchini, mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya, USAID, wawakilishi wa balozi mbalimbali, wawakilishi kutoka wizara na idara za serikali, viongozi wa mashirika na asasi mbalimbali pamoja na maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es salaam waliojitokeza kushiriki maandamano ya amani kutoka viwanja vya Kinondoni Biafra hadi Millenium towers kupinga ukatili wa kijinsia.
Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni ya kimataifa inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kuelimisha jamii kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
WiLDAF inashirikiana na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI), wadau wa maendeleo na mashirika mengine kuadhimisha kampeni hizi kitaifa.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni: Funguka! Pinga ukatili wa kijinsia. Elimu salama kwa wote.
Kauli mbiu hii inahamasisha jamii na taifa kwa ujumla kuangalia ni kwa kiasi gani changamoto zilizopo katika miundo mbinu, mifumo ya kibaguzi na kukosekana kwa usawa wa kijinsia, sio tu kunachochea ukatili wa kijinsia, bali pia kunakwamisha juhudi za serikali, asasi za kiraia na wadau mbalimbali katika kuboresha elimu na hivyo kusaidia watanzania kujikwamua katika wimbi la ujinga na umaskini.
Uzinduzi wa maadhimisho hayo ulipambwa na burudani kutoka kwa Mwasiti.
#16DaysTz #ElimuSalama

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
  Maandamano ya amani kutoka viwanja vya Kinondoni Biafri hadi Millenium Towers jijini Dar es salaam
 Ummy Mwalimu, Mwakilishi kutoka shirika la UN Women, WLAC na LHRC, Balozi wa Ireland nchini pamoja na mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya wakipokea maandamo ya amani wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
 Wakiwa ukumbini
 Mwakilishi wa UN Women nchini Tanzania, Maria Karadenizli akizungumza wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
 Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Paul Sherlock akizungumza kwa niaba ya mabalozi wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. 2596: Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Roeland Van de Geer akizungumza wakati wa uzinduzi wa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
 Mwanamuziki wa Kizazi kipya Mwasity akitoa Burudani

No comments: