Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushrikiano wa Afrika Mashariki inapenda kufafanua na kuweka sawa taarifa
zilizoandikwa kwenye baadhi ya Magazeti ya tarehe 07 Desemba, 2016 kuwa mgogoro
wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa unakaribia kuiva na kwamba
Mgogoro huo unatarajiwa kumalizwa na washauri wa kimataifa.
Taarifa hiyo haikuwa
sahihi. Ukweli ni kuwa, mgogoro wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwa sasa
upo chini ya Jopo la Viongozi Wastaafu wa Afrika wanaotokea kwenye nchi za Ukanda
wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa
Afrika (SADC). Jopo hilo linaongozwa na Mhe. Joachim Chissano, Rais Mstaafu wa
Msumbiji akisaidiwa na Mhe. Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana na Mhe.
Thabo Mbeki, Rais Mstaafu wa Afrika Kusini.
Aidha, Jopo hili ambalo
liliundwa na Umoja wa Afrika kupitia Jukwaa la Viongozi Wastaafu wa Afrika
(Forum for Former African Heads of State and Government) kwa ajili ya
kusuluhisha mgogoro huu, linaendelea na kazi hiyo kwa kupitia taarifa
mbalimbali na maandiko yaliyowasilishwa kwao na Tanzania na Malawi. Vile vile,
Jopo lilikwisha zikutanisha pande zote mbili katika mashauriano ya awali yaliyofanyika
nchini Msumbiji.
Wizara inapenda kuujulisha
umma kuwa licha ya kuwepo kwa mgogoro wa mpaka wa Tanzania na Malawi katika
Ziwa Nyasa, mahusiano ya nchi hizi mbili yamezidi kuimarika siku hadi siku
katika Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii. Hata wananchi wa pande zote
mbili za Ziwa wameendelea kuishi kwa amani na ushirikiano wa karibu.
Aidha, katika kuimarisha
uhusiano huu, Tanzania na Malawi zinatarajia kuwa na mkutano wa Tume ya Pamoja
ya Ushirikiano mapema mwakani. Mkutano huu utawaleta watalaam wa nchi hizi
mbili kutoka Sekta mbalimbali kwa lengo la kujadili changamoto za ushirikiano katika
sekta hizo, kubaini maeneo mapya ya ushirikiano pamoja na kuweka mikakati ya
kutekeleza miradi ya pamoja itakayokubaliwa baina ya pande hizi mbili.
Pamoja na mambo mengine,
Mkutano huo unatarajiwa kujadili masuala ya ushirikiano katika sekta za biashara
na uwekezaji, usafirishaji, fedha, nishati, utalii, ulinzi na usalama uhamiaji,
uvuvi na ardhi.
Hivyo, Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inawaomba Waandishi wa Habari, Wadau
mbalimbali na wananchi kwa ujumla inapohitajika kupata taarifa sahihi za suala
hili kwenda kwenye Mamlaka husika na kuziandika kwa usahihi kwa ustawi wa nchi.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam,
07 Desemba, 2016.
No comments:
Post a Comment