Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Shirika
lisilokuwa la kiserikali la Plan International mwaka 2016 lilifanya
utafiti na kugundua kuwa nafasi ya watoto wa kike ulimwenguni haionekani
machoni pa watu.
Hatua
hiyo inatokana na sababu zinazoonesha kuwa takwimu zinazowahusu watoto
wa kike ziko nyuma ya wakati, hazijakamilika na muda mwingine tafiti
zake hazifanyiwi utekelezaji.
Nchini
Tanzania imeonekana hakuna takwimu sahihi zinazoonyesha uhalisia wa
changamoto anazozipata mtoto wa kike kutokana na ndoa za utotoni, hivyo
kupelekea thamani ya mtoto wa kike kushuka katika nyanja mbalimbali za
kimaendeleo ambapo madhara yake yanaonekana baadae akiwa mtu mzima.
Mkuu
wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka Shirika la Plan
International–Tanzania, Jane Mrema anasema kiwango cha ndoa za utotoni
kwa Tanznia kimefikia asilimia 36 ambacho ni kiwango kikubwa zaidi ya
kiwango cha Dunia ambacho ni asilimia 34 na kwa hesabu za kimkoa ni
asilimia 59 kwa kila mkoa.
“Hiyo
ndio sababu kubwa iliyopelekea Shirika letu kuungana na Serikali pamoja
na mashirika mengine kufanya utafiti huo wenye lengo la kufahamu vitu
vinavyopelekea ndoa za utotoni pamoja na madhara yake baada ya ndoa hizo
kutokea,”anasema Bi. Jane.
Utafiti
huo umefanyika kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakiwemo ya
Shirika la kutetea haki za watoto (Plan International), Jukwaa la Utu wa
Mtoto (CDF), Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Shirika linalohusiana na Utafiti na maendeleo ya Afya ya Wanawake (FORWARD) pamoja na Shirika la Utafiti juu ya Kupunguza Umasikini (REPOA).
Baada
ya utafiti huo kukamilika, iliandaliwa ripoti ambayo ilizinduliwa mnamo
Machi, 2 mwaka huu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu, ripoti inayojulikana kama Ripoti ya Utafiti wa
Visababishi na Madhara ya Ndoa za Utotoni Nchini Tanzania.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa umasikini ndio sababu kubwa inayopelekea kuwepo kwa ndoa za utotoni.
Baadhi
ya mikoa ambayo wananchi walihojiwa wakati wa utafiti wamekubali kwa
nguvu zote kuwa fedha zinazolipwa kwa ajili ya mahari ndizo
zinazowasababisha kuwaoza watoto wao wakiwa bado wadogo.
Utafiti
huo unaonesha mkoa wa Mara wananchi asilimia 59 wanakubalina na majibu
ya utafiti huo ambapo mkoa wa Dar es Salaam asilimia 56, mkoa wa Dodoma
asilimia 53, mkoa wa Lindi asilimia 52 na mkoa wa Tabora asilimia 51.
Sababu
nyingine ya ndoa za utotoni ni mtazamo wa tamaduni, mila na desturi
baina ya jamii mbalimbali kuhusu miaka ya mtoto wa kike anayetakiwa
kuolewa, unyago, ukeketaji pamoja na ngoma za asili zinazopelekea watoto
kuozwa mapema.
Tafiti
hizo zinaonyesha kwamba maeneo ya vijijini asilimia 18 ya wanawake
wamekeketwa wakati Mijini ni asilimia 7 na Mikoa inayoongoza ni Manyara
asilimia 81, Dodoma asilimia 68, Arusha asilimia 55, Singida asilimia 43
na Mara asilimia 38.
Aidha,
asilimia 24 ya waliohojiwa mkoani Shinyanga na asilimia 20 ya mkoani
Tabora wamesema mikoa hiyo ina kiwango kikubwa cha ndoa za watoto walio
na umri chini ya miaka 18.
Utafiti
huo pia umegundua kuwa ukosefu wa elimu unapelekea wasichana kuingia
kwenye ndoa wakiwa bado wadogo kiumri hii inatokana na kushindwa
kuendelea na masomo baada ya kumaliza elimu ya msingi.
Kutokana
na utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Plan International-
Tanzania, Jorgen Haldorsen anasema “Matokeo ya utafiti huo yanawapa
mwongozo wa kujua sehemu zilizoathirika zaidi ili kuweka nguvu za
kutosha na kufahamu namna mbalimbali za kutumia kuwafikia waathirika
hao”.
Akizindua
ripoti hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu anasema kuwa anapozindua ripoti hiyo ni dhahiri
anapinga kwa vitendo ndoa na mimba za utotoni kwani ni changamoto kwa
maendeleo ya Tanzania.
“Tunataka
Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini hatutaweza kuwa na nchi yenye
viwanda wakati watoto 36 katika kila watoto 100 nchini wanaolewa kabla
ya kufikia umri wa miaka 18 na watoto 27 wa kitanzania wanapata mimba
kabla ya umri huo, hili ni tatizo kubwa ambalo athari zake zitaonekana
baadae”anasema Waziri Ummy.
Katika
kuhakikisha ndoa hizo zinakoma, Waziri Ummy ameanza kutumia marekebisho
ya Sheria ya Elimu yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mnamo June 2016 ambayo yanakataza mtu yoyote kumuoa mtoto wa
shule ya Msingi au Sekondari kwani ni kosa la jinai lenye adhabu ya
miaka 30 jela.
Pia,
Waziri Ummy amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kila Halmashauri
kupita nyumba kwa nyumba kuwaibua wazazi wanaofanya vitendo hivyo na
kuwasilisha taarifa hizo sehemu husika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa
sheria hiyo.
Waziri
Ummy ameyaahidi mashirika hayo ya kutetea haki za watoto kuendelea
kushirikiana nao katika kuwapa semina wazazi juu ya athari za ndoa za
utotoni, kuwapa watoto elimu ya afya ya uzazi pamoja na kuboresha
mazingira ya shule ili kuwawezesha wasichana kupata hamasa ya kwenda
shule.
Kwa
upande wa viongozi wa dini Mchungaji Cistus Mallya pamoja na Sheikh
Swedi Twaibu wanasema mtoto lazima apate malezi mazuri kutoka kwa wazazi
ili aweze kufahamu mabaya na mazuri na aweze kujiepusha na vitendo
viovu vikiwemo vya kudanganywa na kuingia katika mapenzi wakiwa na umri
mdogo.
Viongozi
hao wamemuomba Waziri Ummy kuangalia utaratibu wa kuwalea watoto
wanaoishi katika mazingira magumu ili nao baadae waje kuwa wanawake
wanaoweza kuleta maendeleo katika taifa lao.
Akiwakilisha vijana wa kike, Catherine Kapilima amesema ndoa za utotoni uhathiri afya, elimu na maendeleo ya mtoto wa kike.
Aidha,
Catherine amesema kuwa wazazi kupewa elimu pekee haitoshi kwani kuna
wengine ambao sio waelewa, hivyo ni jukumu la Serikali kuweka nyumba
ambazo ni salama kwa ajili ya kuwapokea na kuwapatia huduma muhimu
watoto wa kike wanaokimbia kutoka kwa wazazi wasiokuwa waelewa.
Ni
wakati muafaka sasa Wadau wote wa Maendeleo nchini kwenda zaidi
Vijijini kuwasaidia wanawake na wasichana waliopo huko kwani ndio maeneo
yenye waathirika wengi wa ndoa na mimba za utotoni ikilinganishwa na
mijini.
Ikiwa
Dunia inakarabia kuadhimisha siku ya wanawake duniani mnamo Machi, 8
mwaka huu, Serikali, wadau pamoja na wananchi waungane kwa pamoja kuzuia
ndoa za utotoni ili kuandaa wanawake imara katika miaka ijayo.
Tunaamini
kuwa watoto wa kike wa sasa ndio wanawake wa kesho hivyo ni vema
kuwaandaa kuwa wanawake bora wenye kuweza kujitegemea na watakaoweza
kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi nchini.
No comments:
Post a Comment