Na Jumia Travel Tanzania
Miongoni mwa maeneo ya kitalii ambayo hayapewi kipaumbele au kutokuwa maarufu ni pamoja na Kusini mwa Tanzania. Tofauti na vivutio vya kitalii vya kanda ya Kaskazini kuwa maarufu kama vile Mlima Kilimanjaro, Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro, kuna uwezekano mkubwa kwamba Kusini mwa Tanzania kuna hazina kubwa ya vivutio kwa watalii ambavyo havitangazwi au kuvumbuliwa na wengi.
Miongoni mwa sababu ambazo zimekuwa zikikwamisha shughuli za kitalii kwa ukanda wa Kusini ni pamoja na miundominu hafifu kama vile barabara, viwanja vya ndege ambavyo hupelekea maeneo hayo kufikika kwa ugumu pamoja na upungufu wa malazi kama vile hoteli za kisasa na zinazokidhi vigezo.
Kwa kutambua umuhimu wa ukanda huu, serikali ya awamu ya tano imekuwa ikifanya jitihada za makusudi ambazo zitakuwa ni chachu katika kukuza utalii. Jitihada hizo ni pamoja na kuzinduliwa kwa mpango wa uwekezaji katika miundombinu ya mradi wa kuendeleza utalii ukanda wa Kusini mwa Tanzania (REGROW) eneo la Kihesa, Kilolo mkoani Iringa. Mradi huo ulizinduliwa hivi karibuni na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Bi. Samia Suluhu na kuhudhuriwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Dkt. Hamisi Kigwangala.
Pamoja na jitihada hizo watalii na watanzania kwa ujumla wanahitaji kujua vivutio vinavyopatikana katika eneo hilo. Kwa kutambua umuhimu wa kutoa elimu juu ya vivutio mbalimbali nchini Tanzania, Jumia Travel imekukusanyia vivutio na shughuli zifuatazo za kitalii pindi utembeleapo eneo la Kusini mwa Tanzania.
Iringa. Mkoa wa Iringa ni kivutio tosha kutokana na historia yake ndefu tangu enzi za utawala wa kikoloni wa Wajerumani. Ni eneo ambalo Wajerumani walijenga ngome yao kwa ajili ya kupambana na vuguvugu za harakati za kukataa kutawaliwa kutoka kwa kabila la Wahehe ambazo ziliongozwa na Chifu Mkwawa. Mji huu ambao ulijengwa tangu karne ya 19 una mambo mengi ya kujifunza na kujionea pindi utembeleapo ambayo hayapatikani sehemu yoyote nchini.
Isimila. Mbali na harakati za wazi za kupinga ukoloni wa Wajerumani, eneo la Kusini linasifika kwa kupatikana kwa mabaki ya historia za kale. Eneo hili limegundulika kuwa na masalia ya kutosha ya zana za kale za Zama za Chuma kuliko eneo lolote duniani, ambapo inasemekana ni maeneo ya mwanzo kabisa kuzalisha zana za viwandani na vichwa vya mishale.
Bonde la Kilombero. Ukubwa wa bonde hili ambalo hujaa maji kwa msimu umelifanya kuwa ndilo kubwa katika ukanda wa Afrika ya Mashariki. Kuna shughuli nyingi za kufanya kama mtalii na mambo kadhaa ya kujifunza pindi utembeleapo eneo hili linalopatikana mkoani Morogoro. Miongoni mwa shughuli za kufurahia ni pamoja na kujionea ndege wa aina mbalimbali wa kuvutia pamoja na shughuli za kijadi za wakazi wa eneo hilo kama vile uvuvi.
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. Kama unaishi Dar es Salaam itakuchukua mwendo wa nusu siku kwa gari ili kufika kwenye mbuga hiyo. Ikiwa imezungukwa na safu ya milima, hifadhi hiyo ya taifa inatoa mandhari nzuri ya mawio na machweo. Mikumi ni mahali pazuri kwa kujionea wanyama wa aina mbalimbali wanaoonekana kwa urahisi na ndani ya muda mfupi. Lakini pia ni sehemu ambayo unaweza kuvinjari aina tofauti za ndege.
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Mbuga hii ni maarufu kwa kujionea wanyama mbalimbali ambao watalii wengi hupendelea kuwaona. Ukiwa kwenye hifadhi hii wanyama kama vile chui, duma, simba na mbwa mwitu ni jambo la kawaida kuwaona.
Selous. Hii ndiyo hifadhi inayoshikilia rekodi ya ukubwa duniani kama ulikuwa haufahamu. Kutokana na ukubwa huo hutoa fursa ya kuwatazama wanyama kwa utulivu zaidi kwani watalii sio wengi tofauti na ukanda wa Kaskazini. Hifadhi ya mbuga ya Selous ni nyumbani kwa wanyama wakubwa kama vile simba, chui, mbwa mwitu, viboko na makumi ya maelfu ya tembo.
Milima ya Udzungwa. Hifadhi ya Taifa ya milima ya Udzungwa ni hifadhi ya misitu ambapo hurusiwa kutembea pekee. Miongoni mwa vivutio ukiwa hapa ni pamoja na kuvinjari matembezi katikati ya msitu wenye miti mirefu yenye urefu wa takribani mita 60 na kujionea maporomoko marefu ya maji yanayotiririka kutoka milimani. Safu ya milima ya Udzungwa ina utajiri wa takribani 40% ya misitu na wanyama wa aina mbalimbali.
Milima ya Uluguru. Badala ya kufunga safari kwenda mikoa ya Kaskazini unaweza kutembelea safu ya milima ya Uluguru ambayo ipo umbali mchache kutokea mji wa Morogoro. Ikiwa na urefu wa takribani mita 2300, milima hii itakupatia wasaa mzuri wa kuepuka pilikapilika za jiji la Dar es Salaam. Kama kupanda milima hiyo haitoshi, eneo hili pia limepakana na Hifadhi za Taifa za Selous na Mikumi.
Zipo shughuli nyingi za kufanya na mambo ya kuvutia pindi utembeleapo vivutio vilivyopo eneo la mikoa ya Kusini. Lakini ni karibu zaidi na hivyo kuokoa gharama za usafiri kwani hakuna umbali mrefu. Faida nyingine ni kwamba kutokana na watalii wengi kumininika ukanda wa Kaskazini, maeneo ya Kusini hutoa fursa ya kujionea vivutio vingi zaidi kwa utulivu bila ya kuwa na msongamano mkubwa.
No comments:
Post a Comment