Mkurugenzi wa Compass Communications, Maria Sarungi Tsehai akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya uamizi wake wa kujitoa na kutoshiriki tena mashindano ya urembo ya Miss International na kuiomba serikali za Tanzania, Japan na China kutotoa ushirikiano wowote kwa shirika la International Cultural Association (ICA) ambao ni waandaji wa mashindano hayo nchini Japani kutokana na ubaguzi wa rangi ambao wameundeleza kwa miaka 51 tokea shindano hili lilipoanza.Kulia ni Mshiriki wa Shindano hilo Nelly Kamwelu wakati walipokuwa wakiwasili nchini kutokea China yalikofanyika mashindano hayo.
Compass Communications yenye leseni ya mashindano ya urembo ya Miss International tokea mwaka 2005 imetangaza kujitoa rasmi katika shindano hilo na kuiomba serikali za Tanzania, Japan na China kutotoa ushirikiano wowote kwa shirika la International Cultural Association (ICA) ambao ni waandaji wa mashindano haya nchini Japani kutokana na ubaguzi wa rangi ambao wameendeleza kwa miaka 51 tokea shindano hili lilipoanza.
Msimamo huu umetolewa na mkurugenzi wa Compass, Maria Sarungi Tsehai ambaye amerudi kutoka mashindano haya na mrembo Nelly Kamwelu ambaye alishindana na warembo wengine 65. Fainali ya mashindano haya yaliyofanyika mji wa Chengdu China tarehe 6 Novemba na katika fainali hiyo hakukuwa na mwakilishi kutoka Afrika katika 15 bora.
“Tanzania tuliwaandikia waandaji (ICA) mwaka 2009 kuwa tunajitoa katika mashindano haya kutokana na ukweli ya kuwa kwa miaka 50 hawajawahi kumpa taji mwafrika na hata 15 bora hawajawahi kuweka mwafrika.” Alieleza mkurugenzi huyu. “ICA walitujibu kuwa watafanya mabadiliko kuanzia mwaka 2010 na kutoa ushindi wa kila bara ambao wataweza kuingia katika fainali yaani hatua ya 15 bora”.
Mwaka 2010 Tanzania haikushiriki katika Miss International kutokana na kile alichoeleza Sarungi kuwa ni hatua ya kutaka kuangalia maendeleo. Hata hivyo mwaka 2010 bado hakukuwa na mabadaliko na hivyo nchi ya Kenya na nchi zingine za kiafrika zilijitoa mwaka huu. Mwaka huu kulikuwa na washiriki 3 wa Afrika ingawa katika mtandao wao awali walionyesha wasichana 6 wa kiafrika, alieleza Sarungi.
“Hata hivyo tulielezwa ya kuwa katika shindano la mwaka huu tutaona maboresho. Na hivyo tulijiamini na kumtuma mshindi wetu wa mwaka huu katika mashindano haya”
Kwa upande wake mwakilishi wa Tanzania, Nelly Kamwelu ambaye pia aliwakilisha Tanzania katika shindano la Miss Universe alieleza ya kuwa anaamini kuwa alishiriki vizuri na alikuwa moja wa washiriki waliopigwa sana picha na kuoneshwa katika televisheni, pia alikuwa mstari wa mbele katika shindano dogo la vipaji.
“Zaidi ya siku yenyewe ya shindano, niliombwa mara 5 zaidi kucheza katika tafrija mbalimbali na nilikuwa mshiriki wa pekee ambaye alichezeshwa mara nyingi” alieleza mrembo huyu ambaye alionyesha kipaji cha kucheza miondoko ya kiarabu yaani bellydancing “Baada ya hayo yote, nilipatwa na mshangao mkubwa kuona tuzo ya vipaji anapewa Miss China. Lakini kilichonishangaza zaidi ni kuwa katika 15 bora wameingizwa wasichana ambao hawakushiriki kikamilifu katika shindano dogo wala kuonyesha ucheshi wowote na hawakuwa na vigezo vya urembo ninavyovijua’
Nelly Kamwelu anashikilia mataji ya Miss Universe Tanzania, Miss Southern Africa International na pia alishiriki katika mashindano makubwa kupita yote duniani – Miss Universe.
Mkurugenzi wa Compass alisisitiza kuwa sababu nyingine kuu ya malalamiko yao kwa waandaji ilikuwa kukosekana kwa vigezo vya kueleweka vya kutafuta washindi na kuonekana kuwa waandaji walikuwa wanabadilisha masharti siku ya mwisho. “Warembo hawakufanyiwa usahili na majaji hivyo haieleweki hawa 15 bora waliwatafutaje!”
Maria Sarungi amesihi serikali ya Japan kusitisha msaada wowote kwa ICA kwani hawazingati kanuni na misingi ya ushirikiano wa kiutamaduni (cultural exchange) kutokana na kuwabagua waafrika. Pia ameiomba serikali ya China ambayo imedhamini mashindano haya kupitia serikali ya jiji la Chengdu kutodhamini tena mashindano haya. “Kuendelea kudhamini na kutoa ruzuku kwa shirika la ICA inaweza kueleweka kwetu sisi waafrika ya kuwa serikali hizi hazijali ubaguzi wa rangi unaoendelezwa na ICA kwa miaka 51 sasa”
No comments:
Post a Comment