Social Icons

Wednesday, 7 December 2011

Watu 18 wauwawa katika ghasia za uchaguzi DRC

Kundi la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch linasema ghasia zinazohusiana na uchaguzi mkuu nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC zimesababisha vifo vya takriban raia 18 na wengine 100 kujeruhiwa vibaya
Kundi hilo lenye makao makuu yake nchini Marekani lilisema Ijumaa kwamba wengi wa waliokufa walipigwa risasi na wanajeshi wa kikosi maalum cha Repuplican Guards katika mji mkuu wa Kinshasa. 
Umoja wa Mataifa ulitoa wito Alhamisi wa kutaka kuwepo na hali ya utulivu nchini humo, baada ya wafuatiliaji wa kimataifa kuripoti ghasia na kuenea kwa kasoro nyingi za uchaguzi ulioanza  Jumatatu. 
Wakati huo huo, serikali ya Congo inasema inajitayarisha kukabiliana na ghasia zinazoweza kutokea kufuatia kutangazwa kwa matokeo wiki ijayo.

Waziri wa usalama nchini humo Adolphe Lumanu, anasema vikosi vyake vinajitayarisha kwa mzozo wowote wa baada ya uchaguzi.
Ripoti ya awali ya Umoja wa Ulaya inasema wafuatiliaji wa uchaguzi waliona masanduku ya kupiga kura yaliyojazwa kura kabla ya kuanza upigaji kura na upungufu wa karatasi za kupigia kura na kwamba baadhi ya watu hawakuruhusiwa kupiga kura.
Mashahidi pia wanasema waliona maelfu ya mifuko ya plastiki iliyokua na karatasi za kura zikiwa zimejaa katika eneo la kuegesha magari mjini Kinshasa. Wanasema karatasi za kura zilipeperuka na nyingine ziliharibiwa na mvua baada ya baadhi ya mifuko kuchanika.
Afisa mmoja wa tume huru ya uchaguzi nchini humo ameiambia Sauti ya Amerika kuwa ripoti hizo zimekuzwa. 
Rais Joseph Kabila anawania mhula mwingine ya uongozi akikabiliwa na wapinzani 10, watatu kati yao wametaka upigaji kura ubatilishwe.

Mgombea wa nne wa kiti cha rais, Vital Kamerhe, amerekebisha usemi wake wa kutaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe, akisema hali ya upigaji kura iliimarika wakati upigaji kura ukiendelea. 
VOA

No comments: