Social Icons

Wednesday 25 April 2012

SIMBA YATAJA VIINGILIO VYA PAMBANO LAKE NA AL AHLY SHANDY JUMAPILI, MAANDALIZI YAMEKAMILIKA




Jumapili ya Aprili 29 mwaka huu, timu ya soka ya Simba inakutana na klabu ya Al Ahly Shandy kutoka Sudan katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF), kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba
ni timu pekee kutoka katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
iliyobaki katika michuano yote ya kimataifa inayosimamiwa na CAF.

Kubwa zaidi, ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania waliobaki katika michuano ya kimataifa na hivyo wanabeba bendera ya taifa kokote kule waliko.

Maandalizi yote kwa ajili ya pambano hilo yamekamilika.

Wapinzani wetu, Al Ahly wanatarajiwa kuwasili kesho saa saba mchana kwa ndege ya Ethiopia Airlines.

Waamuzi na Kamishina wa mchezo wamepangwa kuwasili Ijumaa (keshokutwa) wakitokea nchini Swaziland na Rwanda.


Kutokana
na ukweli kwamba mechi hiyo itakuwa ya kimataifa, Simba imepanga
viingilio ambavyo kila mwananchi ataweza kuvimudu. Viingilio vitakuwa kama ifuatavyo.

Viti vya bluu na kijani itakuwa Sh. 5,000, Rangi ya Chungwa Sh, 10,000, VIP C 15,000, VIP B 20,000 na VIP A 30,000.

Tiketi zitauzwa katika maeneo yafuatayo, Big Bon, Benjamin Mkapa, Stears Mjini, Mbagala Dar Live, OilCom Buguruni, Tandika Mwembeyanga, Ubungo Oilcom, Mwenge Bus Stand, BP Mwananyamala na Gapco Ukonga.

Tiketi zitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa asubuhi katika maeneo yaliyotajwa.

Klabu
imepokea maombi mengi kutoka kwa wanachama na wapenzi wake kutoka
mikoani na ingeomba kwamba wale wanaotaka kuja kutazama mechi hii kwa
makundi kutoka mikoani, wawasiliane mapema na uongozi ili wanunuliwe
tiketi zao mapema.

Simba SC imechapa tiketi za kutosha na ingeomba wapenzi na wanachama wake kujitokeza kwa wingi kwenye pambano hilo.

Wana Simba wote wanaombwa kuja uwanjani wakiwa wamevalia mavazi yao ya rangi Nyekundu na Nyeupe ili uwanja mzima upendeze kwa rangi hizo.

Tunatoa wito kwa vyombo vya habari kuisaidia Simba na Tanzania
kwa kuelekeza nguvu zao katika uandishi wa taarifa ambazo zitaisaidia
timu yetu kusonga mbele na si kuondoa morali au kusababisha watu
wasiende uwanjani.

Uongozi wa Simba SC
unatoa shukrani, kwa namna ya kipekee kabisa, kwa serikali kutokana na
uamuzi wake wa kuruhusu Wekundu wa Msimbazi kufanya mazoezi katika
Uwanja wa Taifa kujiandaa na mechi hii muhimu.

No comments: