Na Joseph Shaluwa
INAWEZEKANA kabisa upo kwenye uhusiano na mpenzi wako kwa muda mrefu sasa, lakini hujui upo katika penzi la aina gani. Si ajabu upo na mtu ambaye kichwani mwake anawaza kukuacha kesho, lakini akilini mwako unapanga kuoana naye!
Lazima uchunguze kwa makini uhusiano wako. Umjue vizuri mwenzi wako, maana matapeli ni wengi siku hizi. Mapenzi ya siku hizi yamejaa ulaghai mtupu, hayana ukweli, kila siku ni maumivu juu ya maumivu.
Matatizo mengi yanaweza kutokea ikiwa utakosa uaminifu kwa mpenzi wako, wakati mwingine matatizo hayo huweza kumlenga mwenzi wako moja kwa moja bila kukusumbua wewe lakini mwisho wa siku wewe utakuja kuwa na matatizo zaidi ya hayo unayoyafanya nyuma ya pazia hivi sasa.
Unaweza kujifanya mjanja sana kwa kuunganisha wapenzi zaidi ya kumi huko gizani ukiamini huonekani na hakuna matatizo yoyote ambayo unaweza kuyapata, kumbe unajidanganya maana kuna siku utakuja kuumbuka kwa kuonekana kwako huna uaminifu!
Wewe ukoje? Uko kwenye uhusiano wa aina gani? Kuna nuru ya kuingia kwenye ndoa au ni kupotezeana muda tu? Utaendelea kuwa chombo cha starehe hadi lini? Hebu twende darasani tukaone.
USANII UKO HIVI!
Wapo wenye mapenzi ya usoni, moyoni hawana pendo. Wana alama nyingi; wana tabia ya kutamka maneno ya mapenzi lakini ndani ya moyo wake kuna vitu viwili, kwanza anakutamani wewe na fedha zako na wakati huo huo anatamani kuwa na bwana mwingine kwa ajili ya kuongeza kitega uchumi.
Mwanamke wa aina hii siyo ngumu kwake kukuita majina mazuri ya kimapenzi lakini akiwa hamaanishi kutoka moyoni mwake kwamba anakupenda. Hawa wapo wengi lakini ni vigumu sana kuwagundua mapema.
Ngoja nikuulize wewe unayemsaliti mpenzi wako, unavyomfanyia mwenzako hivyo unadhani yeye hana moyo? Hivi hujui kuwa mwenzako anakupenda kwa mapenzi yake yote na amekuchagua wewe uwe mwandani wake?
Siku akijiua kwa sababu yako utakuwa katika hali gani? Hebu acha utapeli wako wa mapenzi haraka sana!
Kuwa muwazi na kama unadhani haupo tayari kuwa na mpenzi basi mwache huru atafute mwingine mwenye msimamo uendelee na mambo yako na kama ni kujiuza ujiuze vizuri lakini ukijua kuwa siku moja utakuja kuingia mahali pabaya. Achana na tamaa za muda mfupi ambazo mwisho wake ni mbaya.
Huyo mwanaume anayekudanganya leo, ujue kabisa kesho hayupo na wewe! Kama umeamua kuwa kiruka njia, mwache mwenzako atafute wake wa maisha. Siyo kumpotezea muda.
KUNA HILI LA USHAWISHI
Hili ni tatizo lingine linalochochea kuharibu maana ya mapenzi. Ushawishi ni sumu nyingine katika hili. Hapa nitazungumizia pande mbili; mosi ni ya mshawishi na mshawishiwa!
Naweza kusema wote wana makosa maana anayeshawishi hutumia kila njia kumpata anayemhitaji lakini wakati huo huo anayeshawishiwa kukubali wakati akijua ana mpenzi ni kosa kubwa sana.
Wanaume wengi watu wazima tena wenye familia zao hivi sasa ndiyo wanaoongoza kutafuta dogodogo wakidai kuwa damu zao zinachemka! Hutumia fedha, magari na kila aina ya vishawishi ili waweze kuwanasa wasichana hao wadogo wakitafuta penzi. Sijui kama wanaume wa aina hii wanatafuta nini kwa hao mabinti? Hivi kama ukigundua mkeo anakusaliti utajisikije?
Wewe unayewarubuni wasichana ambao wapo masomoni na kuwashawishi kwa fedha zako je, kama ni mwanao ndiyo angekuwa anafanyiwa hivyo ungejisikiaje? Kwa nini unakuwa na moyo wa chuma kiasi hicho?
Ni ulimbukeni wa ajabu sana kumuacha mkeo nyumbani halafu uanze kuhangaika na vimada. Wa kazi gani kwanza? Labda unatafuta penzi shatashata, sasa si bora umfundishe mkeo akufanyie hayo unayoyapenda? Kwani umemwambia unachotaka akashindwa kukupa?
Unapaswa kubadilika ndugu yangu maana dunia ya sasa siyo ya kuchezea! Kutoka nje ya ndoa siyo suluhisho. Upande wa pili ni wa wasichana ambao hushawishiwa na watu wazima, asilimia kubwa ya wasichana wa aina hii huwa na wapenzi wao, lakini kwa tamaa ya fedha hujikuta wakijitumbikiza katika uhusiano na wanaume hao.
Kwanza hivi wewe binti hujipendi? Kwa nini unaiacha akili yako bila kufanya kazi kiasi hicho? Hebu jiulize, mpaka amekufuata wewe ameshatembea na mabinti wangapi kama wewe? Kitu gani kilichomvutia kwako na wewe umevutiwa na nini wakati una mpenzi wako anayekupenda kwa dhati?
Hebu chekecha kichwa chako vizuri, mpenzi wako ameshakuvisha pete ya uchumba lakini unamsaliti ukijua wazi kuwa unafanya makosa kwa nini unafanya hivyo? Tamaa ya fedha ndogo ndogo itakufikisha wapi?
Acha kuudhulumu moyo wa mpenzi wako, magonjwa siku hizi ni mengi, unatakiwa kutulia na kuachana na tabia zisizofaa ili mwishoni uweze kuwa bora kwa mwandani wako.
Natamani kuendelea na darasa letu, lakini nafasi yangu haitoshi. Naweka kituo kikubwa hapa, wiki ijayo tutaendelea. Si KUKOSA!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment