Social Icons

Saturday 21 April 2012

Wivu una dawa, soma hapa upone

Na Luqman Maloto
Bila shaka msomaji wangu umzima na unaendelea na majukumu yako ya kawaida. Kwa wiki ya tatu mfululizo, tunaendelea na mada yetu ya namna ya kukabiliana na tatizo la wivu uliopitiliza. Endelea kuanzia pale tulipokuwa tumeishia...
Kwa mwanamke, kama anamhofia mwenzi wake kwamba anaweza kumsaliti kwa kutoka na mtu ambaye huwa anawasiliana naye, hiyo ni sawa na kujiwashia taa nyekundu. Si ajabu kutojiamini kwako kukamfanya mwezi wako aone bora amalize kesi moja kwa moja. Vilevile, kwa mwanamke mwenzako atavimba kichwa kuona hujiamini kwa sababu yake.

Kwa mwanaume, itakufanya ukose sifa za kuonekana kidume. Mwenzi wako atakuona msumbufu na unamkosea heshima kumtuhumu kwamba anaweza kukusaliti. Amini kwamba wewe ni wa ukweli na mpenzi wako anatosheka kwa makali ambayo unayo.
Usipojiamini, utampa kichwa huyo unayemuogopa. Muamini kuwa hatakusaliti na endapo unadhani anaweza kukuendea kinyume, huna haja ya kuishi naye. Ni rahisi kuonekana katuni kwenye jamii, mjinga au bwege kama hujiamini.
Linda heshima yako, dhibiti wivu wako, jiamini. Hayo ni mambo ambayo yanaweza kukupa uwezo wa kukabili changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuusumbua moyo wako kwa kuupa wasiwasi kuwa mwenzi wako anakuendea ndivyo sivyo.
“Yule ndugu ananiogopa kweli, anahisi namchukua mtu wake,” hii kauli anaweza kuitamka huyo ambaye wewe huna imani naye. Tambua kuwa unampa kichwa kwa maana hata jinsi anavyozungumza anaashiria kuwa yeye ndiye aliyebeba amani yako. Usimfanye binadamu mwenzako akajiona hivyo.
6. WASILIANA MARA KWA MARA
Una wasiwasi na mahali ambako mwenzi wako yupo? Huna amani na unahisi anakusaliti? Moyo wako umefunikwa na jakamoyo na kila hatua mapigo yanaongezeka kasi au yanashuka? Kimsingi huna sababu ya kuwa hivyo. Usiishi kwa dhana, ila simamia vitu vinavyoonekana.
Mawasiliano ni njia bora kabisa ya kudhibiti wivu. Mnapozungumza mara kwa mara au ‘kuchati’ kwa SMS, Facebook au mitandao mingine ya kijamii, huwaweka karibu. Kama una hali ya wasiwasi, itakwisha au kupungua kwa sababu muda wote utajiona kama mpo pamoja.
Je, mkiwa wawili chumbani au sehemu yoyote ya faragha, bila simu wala mtu wa tatu anayeweza kuingilia ukaribu wenu, mnaweza kuanza kulumbana kwa sababu ya kuoneana wivu? Jibu ni hapana. Hivyo basi, mawasiliano ya mara kwa mara huwaweka karibu na ni salama zaidi kuliko hata mngekuwa wawili chumbani.
Mawasiliano yasiwe yenye kuishia katika simu au mitandao, kama hamjafunga ndoa au tayari ni wanandoa lakini hamuishi pamoja, jitahidini kukutana mara kwa mara. Ikiwa mnaishi eneo moja, wekeni
utaratibu wa kuonana kila inapobidi, hiyo itasaidia kukuza upendo na amani ambayo itayeyusha hulka za wivu.
Wakati ukitekeleza hili la kuonana mara kwa mara na mwenzi wako, si vibaya ukamwambia jinsi unavyoumizwa na tabia ya yeye kufanya mawasiliano ya karibu na watu wenye jinsi tofauti na yake.
Ukizungumza naye kwa upole, hali itakuwa nzuri kuliko kulaumu au kulalamika.
Hoja ya wivu iwekwe mezani halafu muijadili kwa upana. Kitendo cha kujadili na mwenzi wako jinsi wivu unavyokutesa, kitasaidia kuweka mwanga na kupata ufumbuzi wa tatizo husika. Kama atajua mambo ambayo akiyafanya utaumia halafu akatekeleza bila woga, maana yake atakuwa amedhamiria kukuumiza, hivyo hakufai katika maisha yako.
Kama usipomwambia ukweli, itakuwa ngumu kwa mwenzi wako kujua jinsi ya kukusaidia kuyakabili hayo maumivu unayoyapata kwa sababu ya wivu. Waungwana wanasema kuwa dirisha la mazungumzo, hurahisisha yabisi kuwa laini. Anza leo kuamini katika kumshirikisha mwenzi wako uone matunda yake.
Shika kanuni hii : “Zungumza sana, ubishi hapana,” utakuwa kituko endapo utajibidiisha na ubishi badala ya kuzungumza kwa lengo la kumpa muongozo. Wivu ni chachandu lakini ukizidi mapenzi huonekana tamu yenye uchungu.
Itaendelea wiki ijayo

www.globalpublishers.info

No comments: