AWALI ya yote nikushukuru wewe msomaji ambaye mara kwa mara umekuwa ukinipigia simu na kunitumia sms kuchangia mada ambazo nimekuwa nikiziandika kupitia ukurasa huu.
Nichukue fursa hii kumshukuru Mama Florine wa Morogoro ambaye mara baada ya kuandika mada hiyo hapo juu, alinipigia simu na kunieleza mambo mengi kuhusu wanawake ambao wameziweka ndoa zao rehani kwa kutengeneza mianya ya kusalitiwa tena na marafiki zao.
Kikubwa alichosisitiza ni wanawake kuchukua nafasi zao kwa kufanya kila wanaloweza kuhakikisha hawaibiwi waume zao. “Wanaume ni wadhaifu sana lakini ni rahisi ‘kuwashika’ endapo watapatilizwa yale wanayoyahitaji,” alisisitiza mama huyo.
Mpenzi msomaji wangu, naomba sasa nimalizie sehemu ya makala haya yaliyokuwa yamebaki ili wiki ijayo nienze nyingine mpya. Utakumbuka wiki iliyopita niliishi kueleza kwamba, mwanamke kushindwa kuchukua nafasi yake kama mke wa mtu ni moja ya sababu zinazoweza kumfanya akasalitiwa.
Kwa kifupi mwanamke kushindwa kumdatisha mumewe ni kumfanya aangalie wapi kwingine anakoweza kupatiwa kile anachokihitaji.
Hili liwe fundisho kwa wanawake waliobahatika kuingia kwenye ndoa. Kumridhisha mumeo ni kumfanya aepukane na vishawishi vinavyoweza kumfanya akusaliti.
Mpe mapenzi atosheke asifikirie kukusaliti. Hii itamfanya asiwe na tamaa ya kupoteza muda wake kwa marafiki zako ambao ni micharuko wanaotamani kuionja asali yako.
Baadhi ya wake za watu wamekuwa ni magoigoi, hawajui kuwaridhisha waume zao, matokeo yake wamekuwa ni watu wa kusalitiwa kila siku. Ni ukweli usiofichika kwamba, licha ya baadhi ya wanaume kusaliti kutokana na tamaa zao za kijinga, wengine wanasukumwa na wake zao.
Itakuwa ni jambo la ajabu kama umeolewa halafu ukawa si mtundu wala mbunifu wa kujua yapi umfanyie mumeo ili kumshika. Tambua dawa ya kutosalitiwa unayo wewe na kama utashindwa kumpa dozi anayostahili, wajanja watachukua nafasi yako.
Dawa yenyewe
Ninaposema ipo dawa ya kumzuia mumeo asikusaliti, simaanishi uende kwa waganga au labda kuna vidonge vya kumeza, lahasha! Dawa ninayoizungumzia hapa ipo mwilini mwako.
Kwanza maneno yatokayo mdomoni mwako. Katika maisha ya ndoa kuna kitu kinaitwa kubembeleza. Je, unautumia mdomo wako kumbembeleza mumeo na kumpa maneno yasiyoisha hamu kusikiliza?
Kama hufanyi hivyo utakuwa unakosea sana na unaweza kusababisha mumeo akapunguza mapenzi kwako na kuhamishia kwa mwingine anayeonesha kumjali.
Kwa maana hiyo utumie vyema mdomo wako kwa mumeo, tumia sehemu hiyo ya mwili wako kumfanya aamini amempata mtu sahihi.
Majonjo na utundu wako
Mwanamke anatakiwa kujua kwamba, akishaingia kwenye ndoa ana jukumu la kumfanya mume wake aone mkewe ni tofauti na wanawake wengine aliowahi kupitia (kama wapo).
Mwanamke anaweza kufanikiwa katika hilo endapo atakuwa mtundu wa kubuni manjonjo yatakayomdatisha mumewe. Si kazi rahisi lakini pia siyo ngumu endapo atakuwa amedhamiria kuidumisha ndoa yake.
Ninachomaanisha hapa ni kwamba, wewe mwanamke unatakiwa kumpatia mumeo penzi ambalo ataamini hawezi kulipata kwingine. Mfanye atosheke na asiwaze kabisa kukusaliti.
Ninaposema maneno hayo simaanishi umpe mumeo penzi hatarishi kwako, hapana! Mpe penzi halali lakini lenye uzito unaoweza kumfanya ajione mwenye bahati kukupata.
Ni lipi penzi hatarishi?
Hapa nazungumzia mapenzi kinyume na maumbile. Chondechonde wanawake, mapenzi haya ni hatari kwa maisha yenu.
Katika uchunguzi wangu nimebaini baadhi ya wanawake ambao naweza kusema ni malimbukeni, wamekuwa wakitumia njia hii wakiamini kuwa eti watawashika waume zao.
Jamani tusifanye hivyo, tuithamini miili yetu na tujue kwamba kukubali kwetu kutoa sampuli hiyo ya penzi ni kujidhalilisha na kujisogeza karibu na kifo.
Tabia zako
Mwanamke anatakiwa kujua kwamba hata kama atakuwa anamdatisha vipi mumewe wawapo faragha, kama atakuwa tabia mbaya ni kazi bure.
Wapo wanawake ambao ni viburi, wasiofuata yale wanayoelekezwa na waume zao. Yaani wanajiona kwa kuwa wamewashika waume zao, hawawezi kuachwa, hiyo ni mbaya!
Jitahidi sana kuwa mpole, msikivu na mwelewa wa yale ambayo mumeo anakuelekeza uyafanye. Kwenda kinyume ni kuonesha kutomheshimu na kama humheshimu mumeo hata umpe mapenzi ya aina gani, hawezi kukukumbatia, atakuacha!
www.globalpublishers.info
No comments:
Post a Comment