PAMOJA na umaarufu mkubwa alioupata wakati akivaa jezi la rangi nyekundu za mabingwa wa soka nchini, Simba Patrick Mafisango amezikwa katika mazingira magumu, huku klabu yake ikikalia pesa za rambirambi na hivyo kuibua mjadala wa maswali mengi kuliko majibu toka kwa ndugu za marehemu.
Mafisango alifariki kwa ajali ya gari wiki moja iliyopita jijini Dar es Salaam na kuzikwa mwishoni mwa wiki iliyomalizika kwenye Makaburi ya Kinkole, nje kidogo ya Jiji la Kinshasa, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hali ya mazingira magumu katika kukamilisha safari ya mwisho ya Mafisango ilianza kuonekana tangu kuwasili mwili wake kwenye Uwanja wa Ndege wa N'Djili, Kinshasa ambapo msafara ulikosa utaratibu wa kueleweka.
Pia ukiachilia mbali uzuri wa gari lililobeba mwili wa marehemu, magari mengine yaliyokuwa kwenye msafara kuelekea nyumbani kwake, ilikuwa aibu kuyaangalia kwa jinsi yalivyokuwa 'vimeo'.
Asilimia kubwa ya gharama za mazishi zilibebwa na baba mlezi wa Mafisango, Papaa Pierre na baadhi ya ndugu walioshangazwa na kitendo cha Simba kushindwa kupeleka rambirambi ambazo zingeweza kusaidia shughuli hiyo kufanyika bila matatizo kama zingewasilishwa kwa wakati.
Aliyekuwa kwenye wakati mgumu ni mtoto wa dada wa marehemu, Orly Elemba(21) waliyekuwa wakiishi naye Dar es Salaam ambaye alikabwa vilivyo na ndugu zake waliohoji ni vipi hakupewa pesa za rambirambi wakati zilishachangwa.
Familia pamoja na wake za marehemu, Jacqueline na Evelyne walidhani Elemba amekuja na fungu kubwa kwa vile alikuwa akiishi na Mafisango na anajua alipokuwa akihifadhi fedha zake ambazo zilipaswa kugharamia sehemu ya maziko yake ambayo hayakuwa na watu wengi kama ilivyokuwa Dar es Salaam.
Mwananchi ilishuhudia kwa nyakati tofauti ndugu hao wakimzonga Orly na kumueleza atoe fungu la marehemu kuchangia gharama kwa vile hali haikuwa nzuri, lakini kijana huyo alijitetea mara nyingi ingawa hakuna aliyekuwa na imani naye mpaka Mwakilishi wa Simba, Joseph Itang'are akawahakikishia familia kuwa kijana huyo hajapewa fungu.
"Wewe utakaaje na Mafisango siku zote hizo usijue anaweka wapi fedha zake, tupe hata michango ya rafiki zake wa Dar es Salaam zitusaidie hapa," alisikika ndugu mmoja wa familia akimwambia kwa hasira kijana huyo.
Siku ya Jumamosi wakati mwili wa Mafisango ukiwa umelazwa kwenye Uwanja wa Terrain ulioko eneo la Lemba nje ya jiji, marafiki zake waliwafokea kuwafokea ndugu zake wakiwatuhumu kuficha Faranga(fedha) za rafiki yao na kumuacha akiungua jua bila hata viburudisho kwa wafiwa na muziki wa kupoteza mawazo.
Katibu aliniambia atatuma pesa Jumamosi lakini sioni chochote na hapa kuna shida ya fedha kweli, hali si nzuri ingawa unaona mambo yanaenda. Kila mtu anajua kwamba nimekuja na fedha nyingi Dar es Salaam, kitu ambacho si kweli," Papaa Pierre.
Michael Momburi, Kinshasa
Chanzo - http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment