Social Icons

Monday, 28 May 2012

Twanga Pepeta yamtimua kazi Meneja wake kwa kosa la kuhujumu bendi



Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Asha Baraka amesema kuwa wamemfukuza kazi Meneja wa bendi hiyo, Martin Sospeter.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Asha alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kugundua kuwa Sospeter anaihujumu bendi kwa kuwashawishi wasanii kuihama bendi hiyo ili watue bendi ya Mashujaa ambayo naye ana mipango ya kutua huko.

"Tumeamua kumfukuza kazi Meneja wa Twanga Pepeta, Sospeter kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za ubadhirifu na kutowajibika ipasavyo... anasuka mipango ya kwenda bendi ya Mashujaa, hivyo tumeamua kumuondoa mapema ili aende akiwa huru.

"Tumemwandikia barua ya kumfukuza kazi na pia anapaswa kulipa fedha za matamasha alizokwapua... nimeamini kumbe kikulacho kinguoni mwako," alisema Asha.

Pia alisema sababu nyingine ya kumtimua ni kukosa uaminifu baada ya kupokea fedha za matamasha mbalimbali takriban sh. milioni 6, lakini hajaziwasilisha ofisini kama ilivyo utaratibu wa kazi.

Asha alisema uchunguzi uliofanywa kwa muda mrefu kumhusu Sospeter umebainika kuwa ndiye amekuwa mstari wa mbele kuwashawishi baadhi ya wasanii wa Twanga Pepeta waliohamia Mashujaa na yeye ana mpango wa kuhamia katika bendi hiyo, hivyo anawatanguliza wasanii ili iwe rahisi yeye kujiunga nao atakapokamilisha dhamira yake.

"Mashujaa wenyewe wanadai eti Sospeter anajua siri nyingi za mafanikio ya Twanga Pepeta, hivyo atawasaidia kuimarisha bendi yao, tumeamua kumfukuza ili akawape vyema hizo siri," alisema Asha.

Mkurugenzi huyo alisema imebidi wamfukuze akajiunge na bendi hiyo anayoona anataka kuitumikia na kwamba safari aliyokwenda Nyanda za Juu na bendi hiyo ndiyo ya mwisho katika utumishi wake akiwa na Twanga Pepeta.

Mbali ya hujuma za fedha na wasanii walioikimbia Twanga Pepeta kuhamia Mashujaa, Asha alisema kuwa imegundulika kuwa, Sospeter hivi sasa anamshawishi mpiga gita la besi wa bendi hiyo, Jumanne Said 'Jojo Jumanne' ili ahamie Mashujaa, hali aliyosema kuwa haiwezi kuvumiliwa kuendelea kuitafuna bendi hiyo.

"Tumemchunguza na kujiridhisha kumhusu huyu meneja Sospeter, ni mtu asiyeitakia uhai Twanga Pepeta... kama hilo ndilo lengo lake akafanye kazi na hao wanaomhitaji na mimi niendelee na mipango yangu na watu ninaoamini kuwa watanisaidia kuikuza tasnia ya muziki wa Twanga Pepeta," alisema Asha.

No comments: