Social Icons

Saturday, 25 August 2012

Leo katika Mahusiano: Mapenzi ni afya, nenda vizuri yakuongezee siku za kuishi . Sehemu ya PiliMada hii ina maana kubwa. Ukiisoma na kuielewa barabara, utafahamu vyema jinsi ya kuishi kimapenzi. Itakuondolea matatizo ambayo mwisho, yatakuwezesha kuishi kwa muda mrefu pasipo hekaheka za hapa na pale. Nakusisitiza usome na uelewe.
Mada ni mapenzi ni afya, nenda vizuri yakuongezee siku za kuishi. Upo ukweli kwamba mapenzi ukiyatendea haki, utakuwa umeuridhisha moyo wako. Hapohapo ndiyo utaweza kuongeza siku za kuishi kwa raha mustarehe.
Hakuna maana ya matumizi ya ARV ambayo humuongezea siku za kuishi mwathirika wa VVU, muongozo ninaoutoa hapa ni namna bora ya kuyatumia mapenzi ili uweze kuishi kwa furaha. Hii ni kwa sababu furaha huleta amani ya moyo.
Moyo unapokuwa na amani, inakuweka huru kutoka kwenye msongo wa mawazo. Inakulinda na shinikizo la damu kwa sababu utulivu unaokuwa nao, unawezesha moyo kufanya kazi yake ya kusambaza damu kwenye kona mbalimbali za mwili kama inavyotakiwa.
Kanuni kuu ya kuhakikisha unafanikiwa kwenye lengo lako ni kusimama katoka muongozo huu: Penda unapostahili, wekeza penzi lako kwa mtu anayestahili. Macho na tamaa visikupoteze njia, mengi uyaonayo ni fahari ya macho tu.
Ndugu wengi waliodanganywa na tamaa ya macho, wakaingia kichwakichwa, wameshatangulia mbele ya haki, wengine wanaendelea kuteseka na dunia. Hakikisha unayempenda, anakuwa ni yule anayeweza kurejesha upendo unaompa.
Hakikisha unayewekeza mapenzi kwake, naye yupo tayari kwa ajili yako. Penzi la upande mmoja huzaa matokeo mabaya. Hugeuka mateso makubwa kwako, huumiza moyo kabla ya kusababisha madhara ya kiafya kama nilivyotangulia kueleza hapo awali.
Wapo watu ambao siku zote wanaonekana wana miili dhaifu. Wanaishia kutuhumiwa na wengine kwamba wameathirika na virusi vya ugonjwa wa kisasa, kumbe sivyo, wapo salama kabisa na maradhi hayo, isipokuwa kinachowauguza ni mapenzi.
Hapa nikuongezee kitu kwamba siku zote unapaswa kutambua kwamba uimara wa mwili wako, unaanzia moyoni. Ukiwa na moyo imara, utaona namna mwili wako utakavyokuwa na nguvu, udhaifu wa moyo huzaa udhaifu wa mwili.
Ni ukweli ulio wazi kuwa hakuna kitu kinachouma sana siku zote kama kupenda sehemu ambayo unaamini utapenda kama upendavyo wewe. Vilevile kingine kinachotesa moyo ni kumpenda mtu halafu asijue au kuheshimu thamani ya penzi lako kwake.
Maisha ni fumbo zito, kwa hiyo hutokea kukutana na mtu ambaye siyo sahihi. Inawezekana pia ni mipango ya Mungu kwa mwanadamu kutumbukia kwa mtu ambaye siyo sahihi. Inaweza ikawa pia majaribu ya Shetani. Unajua Shetani ni msumbufu sana.
Wakati mwingine, hali ya kukutana na mtu ambaye siyo sahihi, imesababisha matokeo chanya, kwamba mtu anapoachana na yule aliyemtesa, anaweza kuwa makini mno kwenye uhusiano wake wa baadaye. Haya tumeyaona sana.
Asimuliaye mvua, imemnyeshea. Kutokana na uzoefu huo, siku akiona mawingu atakuwa makini kutafuta hifadhi. Vivyo hivyo, aliyeteseka (kwa kutendwa) au aliyeachwa (baada ya kumtenda mwenzake), ni wajenzi wazuri wa uhusiano.
Hii ni kwa sababu wanajua athari iliyo kinyume chake. Wapo ambao hawakubali kufanya mchezo kama wa mwanzo. Ila wapo vichwa ngumu ambao maumivu yaliyopita hawayazingatii. Hawakosekani, ndiyo maana nakutaka wewe ucheze salama. Mapenzi ni matamu.
Itaendelea wiki ijayo
GPL

No comments: