NINA imani u mzima kwa uwezo wa Mungu, yangu hali namshukuru Muumba kwa kunipa uhai na nguvu ya kuweza kukutana nawe leo.
Katika uhusiano, kumekuwa na vitu ambavyo vikifanyika kwa kiasi kikubwa au mtu kukaa kimya sana, lazima watu watahoji na kuona kuna tatizo.
Mtu mmoja akionekana mkorofi sana au kuwa mpole sana kiasi cha kuonekana kama kainamishwa na mwenzake, basi hapo kutakuwa na tatizo.
Siku zote wivu katika mapenzi huwa kachumbari ya kuonyesha kweli kitu chako unatakiwa kukimiliki mwenyewe, lakini ukizidisha huwa karaha, ukimya katika mapenzi ukipitiliza huwa tatizo pia. Wajuzi wa maneno wamesema chochote kikizidi kipimo huwa sumu.
Wapo watu hutumia vitu hivyo kama kinga katika uhusiano wao bila kujua ni tatizo linalopoteza upendo ndani ya nyumba zao.
Kwa nini nasema hivyo?
Wengi tunaamini unapotaka kumdhibiti mpenzi wako, lazima uonyeshe shaka kwake kwa kuamua kufuatilia kila kitu chake, kama utaona kimekwenda ndivyo sivyo, basi unakuwa mkali na kumtishia kumpiga au hata kuachana naye.
Mwingine kutokana na kumpenda sana mpenzi wake, huogopa kumgombeza hata kama kafanya kosa hukaa kimya kwa kuamini kufanya hivyo kunaweza kumuudhi na kusababisha kutengana.
Kinga ipi iliyo sahihi kwa mpenzi wako?
Siku zote nyumba imara huanzia kwenye msingi, hivyo, msingi imara katika mapenzi ndiyo kinga sahihi katika uhusiano.
Kinga hiyo ni ipi?
Kinga katika mapenzi ni kumsoma mwenza wako, naye akusome kisha wote kwa pamoja kuchagua mfumo wa maisha huku mkiwekeana uhuru wa baadhi ya sehemu na ili mtu asitoke nje. Kwa vile mmekubaliana kwa pamoja, mtu akienda kinyume na mliyokubaliana, huyo ni msaliti.
Siku zote mwanadamu huwa hachungwi, bali hujichunga mwenyewe, kama nilivyoelezea muishi katika mfumo gani, baadhi ya mambo hayawezi kukupa presha kwa vile mmezungumza, hivyo si rahisi kwenda kinyume.
Siku zote mtu anatakiwa amuamini mwenzake ili aweze kuishi bila wasiwasi wa kuwaza kila dakika anaibiwa akiwa mbali na mpenzi wake.
Utawezaje kuishi salama?
Kuishi salama kunatokana na mazingira utakayoyajenga wewe na mpenzi wako, kwa vile mpaka unakuwa naye, umejua vizuri tabia zake kwamba ni msikivu na mwaminifu.
Hili ndilo muhimu katika uhusiano, huwezi kuishi na mtu unayejua ana tabia mbaya. Kutokana na kumpenda sana, unamchukua ukiamini utatumia silaha ya wivu wa kinga kwa kuamini itasaidia kumtuliza, la hasha.
Mwingine huteseka kwa kukaa kimya kutegemea huruma ya mpenzi wake kwa kuamini mkiachana hutampata kama yeye. Huko ni kujidanganya na kujiingiza kwenye mateso ya kujitakia kwa vile tabia ya mtu ipo kama ngozi, ni vigumu kubadilika.
Siku zote jitahidi kutafuta mpenzi ambaye unamjua tabia zake vizuri ili katika uhusiano wenu, usiwe mkali sana au mpole sana, kama kinga.
Katika mapenzi, mtu hakatazwi kumuonea wivu mpenzi wake au kumsikiliza, lakini unapomuona anakwenda kinyume, unatakiwa kumuweka chini na kumueleza bila kuangalia uzuri wake. Kuwa na mpenzi mzuri ni furaha, si mateso ya moyo.
Kwa haya machache inatosha, tukutane wiki ijayo.
www.globalpublishers.com
No comments:
Post a Comment