KAMA kawaida tumekutana tena kwenye kona yetu ya Mapenzi na Uhusiano, leo nataka nizungumzie maumivu katika mapenzi ambayo unaweza kukutana nayo na kuyavumilia.
Kumekuwa na matukio mengi katika uhusiano yanayosababisha mmoja kuumizwa na mpenzi wake pale anapokosa uaminifu au kutoonyesha kujali hisia za mwenzake.
Ni kweli wanadamu tuna upungufu ambayo huenda ukasababisha maumivu kwa mmoja. Wapo ambao wamekuwa wakivumilia mateso ambayo wamekuwa wakiyapata kwa wenza wao, wakiamini huenda mwenzake atajirekebisha lakini bahati mbaya anayemtegemea hayaoni maumivu ya mwenzake na kuendelea kumtesa.
Katika mapenzi kitu uvumilivu ndiyo nguzo, hasa penzi linapopoteza mwelekeo kwa mmoja kuvumilia ya mwenzake akiamini ipo siku atajirekebisha.
Kwa vile mwanadamu ni kiumbe cha kujisahau anapokumbushwa basi hurudi katika mstari na faida ya uvumilivu hapo huonekana.
Kwangu, maumivu kwenye mapenzi huwa nayachukulia kama ajali ndani ya mapenzi, lakini yanatakiwa kuvumiliwa kwa kuitafuta suluhu. Wapo wanaofanikiwa kwa uvumilivu wao kwa vile si vema kila kinachokuumiza ukichukulie uamuzi mzito.
Katika maisha ya mapenzi, unapokuwa na mpenzi wako mkawa na malengo ya muda mrefu, tatizo lolote linapotokea hutakiwi kukurupuka kutoa uamuzi, bali ni vema kutulia na kuliangalia ili kubaini kama lilikuwa kosa la makusudi au bahati mbaya! Je, aliyekuumiza maumivu yako yamemgusa? Yupo tayari kuomba msamaha na kuapa kutorudia tena kilichokuumiza?
Kama mtu huyo atakuwa tayari kuyafanya yote hayo, una haki ya kumsamehe na kufungua ukurasa mpya, kwa kuwa kutenda kosa ni kosa lakini kulirudia ni kudhamiria.
Wapo wanaoomba msamaha na kusamehewa lakini kila kukicha hurudia kosa lilelile, nawe unaendelea kuvumilia. Hayo sasa yanakuwa si mapenzi, bali mateso ya mapenzi.
Kwa vile makosa ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, tusiyachukulie kama fimbo ya kuwapigia wenzetu, hasa tunapojua kwamba wanatupenda kwa dhati.
Kama nilivyosema kuwa maumivu katika mapenzi ni sawa na ajali ambayo huwa haiepukiki, lakini yasiwe mazoea, kila siku uwe mtu wa kulia tu kwa ajili ya mapenzi.
Usikubali kumpa moyo wako mtu unayejua kabisa hawezi kukuhifadhi ndani ya moyo wake. Si kila unayempenda lazima awe mpenzi wako kwa hali na mali.
Kupenda hakuna kikomo, wengi huumizwa na mapenzi kwa vile huamini vilivyochaguliwa na mioyo yao, hata kama vina madhara baadaye.
Mapenzi ni sawa na mbegu na udongo wenye rutuba, ukiona haimei ujue huo siyo udongo wake, japo unapendeza machoni mwako.
Si kila anayekutamkia anakupenda ana mapenzi ya dhati kwako. Waswahili wanasema matendo hukidhi haja malidhawa kuliko maneno, wanaojua hakuna kilichojengwa na maneno zaidi ya vitendo, penzi la kweli la vitendo huchukua nafasi kubwa kuliko maneno.
‘Samahani’ huwa ni mara moja, ikizidi huwa utani na kuonyesha dharau kwa yule umpendaye kwa kumuona hana uwezo wa kufikiri zaidi ya kukupenda wewe tu.
Usikubali kuumizwa na ambaye hajui thamani ya maumivu yako, amefanya kosa umemsamehe lakini analirudia kwa njia ileile. Si mkweli si muaminifu, hajali maumivu ya moyo wako lakini bado unavumilia kisha unalia.
Acha kulia, pambana sasa, kwa vile maumivu ya moyo wako hakuna wa kukubebea ila mwenyewe. Kuumizwa ni ajali lakini isiwe mazoea, hakuna aliyeumbwa kuumizwa milele, kwa vile mapenzi ni furaha.
Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment