NDOA inafahamika kuwa ni heshima kwa kila mmoja, namaanisha kwa anayeoa na anayeolewa. Mwanaume akioa, anaheshimika na anajiona ameingia kwenye majukumu ambayo yanamlazimu atie akili ili aweze kukabiliana nayo.
Kwa wanawake ndiyo usiseme. Yaani idadi kubwa ya wanawake wanalilia ndoa hasa kwa wanaume ambao wamewapenda na kuwaamini kwamba wakiwa nao ndani maisha yao yatakuwa ni ya furaha zaidi.
Kwa kifupi ndoa ni tamu ila kama utaijulia na ni chungu kama utakuwa umeingia kwenye maisha hayo na mtu ambaye awali alikuwa akijifanya anakupenda sana lakini baadaye akaamua kutoa makucha yake.
Wapo wanaume ambao leo hii wanalia, wanajuta ni kwa nini waliamua kuwaoa wanawake ambao wamewaoa. Wanajuta kwa kuwa wanakutana na mambo ya ajabu ambayo hawakuyatarajia.
Si hivyo tu, wapo wanawake ambao walifurahi walipovishwa pete za uchumba na hatimaye kuvaa mashela lakini leo hii wanaomba talaka kutoka kwa waume zao kutokana na mazingira tofauti wanayokumbana nayo.
Kwa kifupi baadhi ya walio kwenye ndoa wanalia, unaweza kuwaona wakipita mbele za watu wanachekacheka na kuonesha kuwa wanapendana lakini kumbe katika uhalisia, wamechokana na ndoa zao zimeshikiliwa na nyuzi.
Unaweza kujiuliza ni kwa sababu gani? Inakuwaje watu waliotokea kupendana sana wanaishi kwa muda mfupi tu kisha wanaanza kujutia maamuzi yao ya kuingia kwenye ndoa?
Hakuna sababu nyingine zaidi ya kwamba aidha walikurupuka kufanya maamuzi hayo au kulikuwa na mazingira ya mmoja kujifanyisha na kumfanya mwenzake aone amempata mtu sahihi kumbe hamna kitu.
Ukijaribu kuchunguza sana, utabaini kuwa wengi wako kwenye ndoa za Kichina. Ndoa ambazo hakuna mapenzi ya dhati baina yao na kusalitiana imekuwa ndiyo mtindo wa kisasa. Katika mazingira haya furaha haiwezi kupatikana na ni lazima majuto yatokee.
Nini ninachotaka kuzungumzia leo? Ni kwamba, ndoa kweli ni heshima na kama umetokea kuwa kwenye uhusiano na mtu ambaye unaona ana kila kigezo cha kuwa mwenza wako, una kila sababu ya kufanya kila uwezalo kukaribisha ndoa. Oa au olewa ili furaha yako iweze kukamilika.
Lakini sasa angalizo ni kwamba, si kila anayeonesha kukupenda sasa anafaa kuwa mumeo au mkeo. Elewa kwamba kuna wanawake wengine ambao wao kupenda kwao hawamaanishi ni ili waolewe, wanapenda tu na kufurahia kampani lakini ukiwatajia ndoa, usije ukashangaa wakakataa kuolewa. Hawa wa sampuli hii ukiwalizimisha utakiona cha mtemakuni.
Namaanisha kwamba, wapo wanawake ambao lile neno ndoa tu kwao limewakalia kushoto lakini wanajua kupenda na kuwaridhisha wanaume. Ni sawa na kulazimisha kumuoa changudoa ambaye ni mtaalamu wa kudatisha, mtaalamu wa kubembeleza na mtaalamu wa kumpa furaha mwanaume yeyote kwa kuwa ameona pesa.
Ukimuoa mwanamke wa aina hiyo ukidhani utapata mambo kama hayohayo,umeumia. Hilo lipo pia kwa wanaume, kuna wale ambao wanaweza kuonesha upendo wa hali ya juu lakini hawako tayari kuingia kwenye ndoa. Ukilazimisha kuolewa na mwanaume huyo, umeula wa chuya kwani huwezi kuyapa mapenzi aliyokuwa akikupa kabla ya ndoa.
Kwa maana hiyo nihitimishe kwa kusema kuwa, lazimisha ndoa lakini kwa mtu ambaye una uhakika anahitaji kuingia kwenye ndoa na umemsoma vizuri na kubaini hawezi kuja kukuletea maumivu siku za baadae.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo.
Na GPL
No comments:
Post a Comment