Social Icons

Tuesday 13 November 2012

LEO KATIKA MAHUSIANO: MAPENZI BORA HUPITIA KATIKA MZANI, JIFUNZE KUPIMA NA ‘KUBALANSI’-3


NIMESHACHAMBUA mengi huko nyuma. Kwa nyongeza, leo nakutaka ujiulize maswali yafuatayo ili uepukane na ugonjwa wa moyo, badala yake, mapenzi kwako yawe kitu rahisi ambacho utakimudu kwa asilimia 100.
*Tazama unavyojisikia pale unapopenda. Je, unapopenda unajisikia vizuri hata kama umpendaye hakupi upendo kama ulionao kwake? Je, kumpenda mtu, ni lazima naye akupende kwa kiwango hicho hicho? Kama ndivyo, ni kwa nini?

*Unajisikia unapendwa hata kama mwenzi wako hayupo? Kama sivyo, ni kwa nini? Je, unajikubali na unaridhika kwa sifa ulizonazo?
*Unafanya vitu kwa ajili ya mpenzi wako? Hata kama hutaki kufanya, je unajitahidi kutekeleza ili kuliweka penzi lenu hai? Unafanya kwa ajili ya mapenzi yake na unahitaji kila unachofanya, naye akufanyie vivyo hivyo?
*Je, umewahi kumueleza mwenzi wako vitu ambavyo ukifanyiwa vinaweza kukufanya ujisikie kupendwa? Amewahi kutekeleza vitu hivyo kwa ajili yako? Kama bado, umewahi kuvumilia na kumfundisha taratibu?
MNAFANANA?
Swali hili lipe uzito. Inawezekana kwenye maswali ya juu ukawa umevuka vizuri. Pamoja na hivyo, haioneshi kama kuna mambo ambayo wewe na mwenzi wako mnafanana. Kama hamuendi sawa, jifunze kumuelewa.
Unaamini katika sanaa, mwenzako anadatishwa na michezo. Unapenda kusoma vitabu na kutoka kwenye matembezi ya hapa na pale, lakini yeye anapenda kusafiri. Hata hivyo, unapaswa kuamini kwamba ndoa ni kujitoa muhanga.
Siyo sawa na kutoa na kuchukua. Inatakiwa uwe mwelewa, katika kuhakikisha mapenzi yenu yanafanikiwa, ni vizuri ukahifadhi mambo yako kisha ukaungana naye kwenye mambo yake. Baadaye utamfanya aungane nawe kwako taratibu.
Hilo litafanikiwa kama utaacha ubinafsi. Tabia ya kutaka upendwe zaidi ni kosa. Katika uhusiano hutakiwi kujifikiria wa kwanza. Wekeza upendo mkubwa, halafu umfanye naye akupende. Si kwa haraka, bali taratibu.
Kama kila unaloamini wewe yeye yupo mbali, jifunze mambo yake kwanza. Muelewe kisha mshirikishe yako. Leo ukimfanya ajue kwamba unapenda kuogelea, keshokutwa mpe lingine na umjulishe kuwa ungependa mwende pamoja.
Kipengele cha jinsi unavyofanana na mwenzi wako ndicho kilitufungia sehemu ya nne ya makala haya. Naendelea kusisitiza kuwa haitakiwi kushindana, unapaswa kukubali kuachia vipaumbele vyako ili umpe nafasi mwenzi wako.
Ni mchezo mdogo lakini mgumu, maana yake ni kuyaweza mapenzi. Ni jambo ambalo lipo karibu na kutowezekana kwa mpenzi wa mpira kuacha ‘rimoti’ ya televisheni kwa mwenzi wake ili aangalie tamthiliya. Hata hivyo, endapo mtagombea rimoti, mwisho mtaanza kuchokana mapema.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: