Social Icons

Tuesday 11 December 2012

JALI AFYA AFYA YAKO :VYAKULA VINAVYOONDOA MAUMIVU WAKATI WA HEDHI-2


WIKI iliyopita tulianza makala haya kwa kuangalia aina mbalimbali za matunda yanayoweza kutibu matatizo mbalimbali yanayowahusu wanawake wakati wa siku zao (menstruation period). Miongoni mwa matunda hayo ni pamoja na papai bichi lakini lililokomaa ambalo limeelezwa na wataalamu wetu kuwa na uwezo wa kulainisha misuli ya njia ya uzazi hivyo kufanya kipindi cha hedhi kutokuwa na maumivu.
Aidha, katika kutibu matatizo hayo, pia kuna mitishamba kadhaa inayoweza kutibu matatizo ya hedhi kwa wepesi na bila kuwa na madhara yoyote kiafya, waganga wa jadi mahiri wanaijua miti hiyo.
Katika suala hili, ili wanawake kujiepusha na kupatwa na matatizo ya maumivu, kutokwa damu kwa wingi kusiko kawaida, kuchelewa kuona siku zao na matatizo mengine kama yalivyoainishwa wiki iliyopita, wanashauriwa kuzingatia suala la lishe. Wanapaswa kujua vyakula gani wale na vipi wasile ili kujiwekea kinga ya kudumu dhidi ya tatizo hili.
LISHE YA KUDHIBITI MATATIZO YA HEDHI
Matatizo mbalimbali yanayohusiana na hedhi, yanaweza kudhibitiwa na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa kutibu mfumo mzima wa mwili, ili kuondoa sumu iliyojilimbikiza katika mwili wa mgonjwa kwa kipindi cha muda mrefu, sumu ambayo imegeuka na kuwa chanzo cha matatizo yanayojitokeza wakati wa hedhi.
Mfumo mzima wa mwili unapokuwa umezingirwa na sumu (toxins), ndiyo huwa chanzo cha matatizo mbalimbali, yakiwemo hayo yanayojitokeza kwa wanawake wakati wa hedhi na dawa pekee katika hili ni kuondoa sumu hizo mwilini kwa njia ya lishe.
Ili kuondoa uchafu huo mwilini, mgonjwa anatakiwa kuanza mpango maalum wa kula matunda na mbogamboga pekee, kutwa mara tatu kwa muda wa siku tano mfululizo. Katika siku hizo anachokuwa anakula ni matunda, juisi za matunda na mboga mbalimbali pamoja na maji, kila wakati wa kula unapowadia.
Hii ina maana kwamba mlo wa mtu huyu, katika kipindi cha siku hizo tano, utakuwa vyakula vilivyotajwa hapo juu, kuanzia asubuhi, mchana na jioni, katika kipindi hicho, matunda, mboga na juisi anazokula zitakuwa zinafanya kitu kinachoitwa kitaalamu kama ‘detoxification’, yaani uondoshaji wa sumu mwilini kwa njia ya asili aliyotuumba nayo Muumba.
Hata hivyo, kwa wale wanawake ambao ni wembamba sana, ambao pengine katika kipindi cha funga hiyo ya matunda wanaweza kupoteza uzito sana, wamepewa ahueni ama ruhusa ya kunywa glasi ya maziwa fresh sambamba na mlo wao wa matunda. Hii ni kwa sababu ya kuepuka kupoteza uzito kuliko kawaida.

SAFISHA TUMBO KWA ENEMA
Kama kweli unataka kuondoa sumu mwilini kwa ukamilifu na mwili wako kuwa safi na huru wa aina zote za matatizo ya kiafya, katika kipindi cha funga ya matunda na juisi, fanya ENEMA ya maji ya uvuguvugu ili kusafisha utumbo mpana na kuwa safi. Enema ni njia ya asili ya kusafisha utumbo mpana kwa kuingiza maji tumboni kupitia njia ya haja kubwa na kutoa uchafu wote. (rejea makala zangu za nyuma kuhusu Enema).

UFUATE MLO KAMILI
Baada ya kumaliza siku tano za funga ya juisi na matunda, mtu mwenye kufanya zoezi hili atatakiwa kuzingatia ulaji wa mlo kamili utakaotilia maanani matunda, mboga za majani, vyakula vya nafaka (mahindi, mtama, ulezi n.k) na nafaka zinazoshauriwa ni zile ambazo hazijakobolewa na kuondolewa viini lishe (wholegrain). Waepuke kula vyakula vitokanavyo na unga mweupe, ikiwemo mikate myeupe, sukari, vitu vitamu (confectioneries), vyakula vya kwenye makopo. Aidha, mtu huyu anashauriwa kuepuka kunywa chai iliyowekwa majani mengi au kahawa iliyowekwa kahawa nyingi.

UVUTAJI SIGARA UKOME
Kwa wale akina mama wenye matatizo wakati wa siku zao na ambao wameamua kuingia katika mpango huu wa kusafisha mwili, hawana budi kuachana kabisa na uvutaji sigara ili kufanikisha zoezi zima la kusafisha mwili kwa njia iliyoielezwa hapo juu. Kwa ujumla uvutaji sigara ni mbaya kwa afya ya binadamu.
Tuonane tena wiki ijayo kwa makala nyingine.

Habari kwa hisani ya GPL

No comments: