Social Icons

Thursday 25 July 2013

Mvumilie mpenzi wako huku ukimfundisha

 
KAMA ilivyo ada tumekutana tena kwenye kona ya Mapenzi na Uhusiano ili kujuzana mawili matatu. Leo tupo kwenye chungu cha kumi Ramadhani, napenda kuwatakia wafungaji wote Ramadhani Kareem. Kabla ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa kunipa pumzi na afya na kuweza kuzungumza nanyi siku ya leo.
Leo napenda kuzungumzia mapungufu yetu ndani ya nyumba zetu. Siku zote kila mtu huanza kwa kujifunza ndipo alewe kitu, pia si wote wenye uwezo wa kuelewa jambo haraka, hivyo wanatakiwa wavumiliwe na si kuona wanafanya makusudi.
Kwenye nyumba zetu vilevile kuna matatizo ambayo yanahitaji kuvumiliana ili kujenga familia imara. Katika uhusiano mwingi kumekuwa na mapungufu mengi ambayo baadhi ya watu wamekuwa si wavumilivu. Inawezekana ikawa bado sijaeleweka, hapa ninakusudia mapungufu gani katika uhusiano.
Kwa mfano, unaweza kuwa na uhusiano na mwanamke asiyejua kupika, hajui usafi wake hata wa nyumba au mwanaume asiyejijali kwa kurudia nguo moja zaidi ya mara tatu, kibaya zaidi hata nguo za ndani huzirudia zaidi ya mara mbili.

Hii inatokana na mazingira aliyokulia, wapo wanaoishi katika nyumba ambazo zina wasichana wa kazi, yeye kugusa jiko huwa mtihani pengine asijue hata kuchemsha maji.
Wengine wameishi maisha ya kisela, mwanaume ana chupi moja au mbili unakuta anaivaa zaidi ya siku tatu. Watu kama hao wakibadili maisha na kuingia kwenye uhusiano hukutana na changamoto nyingi. Hawawezi kubadilika mara moja kwani wanatakiwa mafunzo ya taratibu huku wakitiwa moyo kuwa wanaweza.
Huenda wewe unapenda sana usafi na mpenzi wako kila siku unamfulia nguo ili awe msafi, lakini unashangaa kumkuta amerudia nguo ya ndani ya jana yake. Inaweza kukukasirisha pengine umeongea sana kuhusiana na tabia ile. Kwa vile aliishi katika tabia ile kwa muda mrefu mvumilie kwani atabadilika taratibu.
Hata kwa wake zetu au wapenzi wetu wanaweza wakawa wameishi mazingira tofauti na maisha wanayoishi sasa. Japokuwa haipendezi mwanamke kurudia nguo ya ndani mara mbili, mtu wa kujisahau kuoga mpaka akumbushwe kama mtoto mdogo. Usafi wa nyumba hafanyi na mpangilio wa nyumba haukai vizuri.
Hii imekuwa ikiwaumiza watu wengi na kutumia nguvu nyingi bila mafanikio. Hapa nataka tuzungumze wote, kama mpenzi wako ana mapungufu kama nilivyoeleza mwanzo unatakiwa kumtia moyo na si kumfokea.
Unapomuelekeza mtu kwa kumfokea, yeye hujenga hofu moyoni mwake na kujikuta vitu vingi akiharibu badala ya kutengeneza. Siku zote mtu anapokosea na kumwelekeza taratibu huku ukimpa moyo anaweza kuelewa na ni rahisi kauli yako kumpa moyo.
Kila unapoliona kosa jitahidi kumwelewesha mkiwa wawili pasipo na mtu mwingine. Jiepushe kumkaripia mbele za watu. Inawezekana mpenzi wa mwenzako yupo smati tofauti na wako. Anapofanya makosa mwelekeze kwa uratibu.
Unapomkaripia mbele za watu humfundishi bali unamdhalilisha. Si wote wanajua, naye atajua huku ukimtia moyo hasa katika kosa ulilomuelekeza na kulirudia kutokana na kusahau.
Unapomtia moyo kuwa anaweza naye huamini anaweza licha ya kuwa ana mapungufu kama mwingine. Hii itasaidia kuwafanya wapenzi wetu kutojishusha na kujipandisha kwa kutaka kujua mengi kwa vile watakuwa na uhuru wa kuuliza wasichokijua.
GPL

No comments: