BABA
wa mwanamuziki mkongwe na nguli nchini Tanzania, John Kitime
aliyefariki Agosti Mosi, 2015 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ya
jijini Dar es Salaam amesafirishwa kuelekea mkoani Iringa tayari kwa
mazishi.
Marehemu
Mzee Francis Raphael Kitime alisafirishwa jana baada ya kufanyika ibada
ya kumuombea na kutoa heshima za mwisho kwa ndugu na jamaa wa familia
ya marehemu waishio Dar es Salaam, ibada iliyofanyika katika Kanisa
Katoliki Parokia ya uruma kwa wagonjwa lililopo ndani ya hospitali ya
Muhimbili.
Akisoma
historia fupi ya marehemu, mtoto wa marehemu John Kitime alisema
Francis Kitime alizaliwa Juni 16, 1931 Tosamaganga, Iringa katika
familia ya watoto watatu yaani Joseph, Isabela na Clementina. Alipata
elimu yake ya msingi hadi chuo kati ya mwaka 1939 hadi 1950 katika Shule
za Misheni na Vyuo vya Elimu Tosamaganga, Iringa na mnamo mwaka 1951
hadi 1963 alifundisha katika shule anuai mkoani hapo.
Kitime
alisema mwaka 1964 marehemu alianza kufanya biashara ya kuuza mafuta
(caltex) hadi 1970 ambapo alimiliki kituo hicho na kufanya biashara hiyo
hadi mwaka 1979, mwaka 1980 aliacha biashara na kuajiriwa kwenye idara
ya utawala katika Hospitali ya Ipamba hadi alipostaafu.
Marehemu
pia amefanya kazi za kitume takribani miaka 20 kama Mwenyekiti wa
Baraza la Walei na Mwenyekiti wa Lions Club katika Mkoa wa Iringa, na
pia mtunzi na mwimbaji nyimbo mbalimbali hasa za lugha ya ki-Hehe.
Marehemu kaacha watoto sita, wajukuu nane na vitukuu viwili.
No comments:
Post a Comment