THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
· Aunga mkono asilimia 100 staili ya Kampeni ya Magufuli
· Asema Tanzania inahitaji mawazo mapya ili iweze kusonga mbele
· Atamani muda wake wa kuongoza Tanzania kumalizika haraka zaidi
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amesema kuwa kama wapo watu binafsi ama taasisi yoyote mahali popote
wenye matatizo na Sheria ya Takwimu mpya ama Muswada wa Habari nchini
basi wawasilishe mapendekezo yake Serikalini ili yafanyiwe kazi badala
ya kukaa na kulalamika pembeni ama kwenye vyombo vya habari.
Rais
Kikwete pia amesema kuwa ni jambo zuri na jema kuwa Mgombea Urais wa
Tanzania kwa tiketi ya CCM anaelezea fikra na matumaini ya
kuleta mabadiliko makubwa zaidi katika uendeshaji wa Tanzania tofauti
na uendeshaji huo ulivyo chini ya uongozi wake.
Vile
vile, Rais Kikwete amesema kuwa anatamani muda uende kwa kasi zaidi ili
aweze kukabidhi madaraka ya kuongoza Tanzania kwa Rais wa Tano, ili
yeye apate muda wa kumpumzika baada ya kazi ngumu ya miaka 10 ambayo
ameilezea kama mzigo mkubwa.
Rais
Kikwete ameyasema hayo, Jumanne, Septemba 22, 2015 wakati alipozungumza
na wafanyakazi wa taasisi nne za Marekani ambazo kwa namna moja ama
nyingine zimefanya kazi na Serikali yake katika miaka 10 ya uongozi wake
mjini Washington, D.C., ambako Rais amefanya ziara ya siku mbili ya
kikazi.
Rais
Kikwete amezungumza na wafanyakazi wa taasisi za National Democratic
Institute (NDI) yenye uhusiano na chama cha siasa cha
Democratic, International Republican Institute (IRI) yenye uhusiano na
chama cha siasa cha Republican, International Foundation for Electoral
Systems (IFES) na United States Institute of Peace (USIP) kwenye makao
makuu ya NDI.
Wakati
wa kipindi cha maswali na majibu na wafanyakazi wa taasisi hizo, Rais
Kikwete ameulizwa swali kuhusu madai kuwa Sheria ya Takwimu na Muswada
wa Habari inavuruga sifa za kidemokrasia za Tanzania chini ya uongozi wa
Rais Kikwete.
Akijibu
swali hilo, Rais Kikwete amesema: “Nimelizungumza hilo huko nyuma na
napenda kurudia. Sheria ya Takwimu inahusu tu takwimu rasmi za Serikali
na wala si takwimu zote. Pili Sheria hii inatokana na matakwa na
taratibu za Umoja wa Mataifa na Sheria yetu imetungwa kwa kutilia
maanani matakwa ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa. Kwa nini hili linakuwa
tatizo kwa Tanzania pekee ni jambo gumu kueleza.”
Kuhusu
Muswada wa Sheria ya Habari, Rais Kikwete amesema: “Nimelisema hili
huko nyuma lakini inaelekea halijaeleweka. Nilipata kusema pale Dar es
Salaam na hata wakati nazungumza na wabunge wa Sweden mjini Stockholm
kuwa kama mtu ana tatizo ama maoni na maudhui ya Muswada ule basi
ayafikishe Serikali. Tutafanyia kazi. Hakuna tatizo na jambo hili. Ajabu
ni kwamba tunachosikia ni malalamiko tu na hakuna yoyote ambaye
amefikisha maoni yake kwetu.”
Hata
hivyo, Rais Kikwete ameongeza: “Jambo muhimu ambalo lazima sote
tuelewane hapa ni kwamba Muswada wowote, uwe wa habari ama wa jambo
jingine, ni lazima ulinde maslahi ya nchi yetu, yalinde umoja wetu,
yalinde utulivu wa nchi yetu na yalinde usalama wa nchi yetu. Haya ni
mambo ambayo hatuna haja ya kujadiliana na yoyote kwa sababu nchi zote
duniani zinalinda kwa namna hii na zinaendeshwa namna hii.”
Rais
Kikwete pia ameunga mkono mwenendo wa mgombea urais wa CCM wakati wa
kampeni ya Uchaguzi mkuu inayoendelea nchini, Mheshimiwa John Pombe
Joseph Magufuli, akisema: “Wamepata kuja watu kwangu… wakaniambia kuwa
Mgombea wetu wa CCM anashutumu na kusahihisha Serikali yangu na utendaji
wake kwenye mikutano ya kampeni. Niliwaambia hivi…..analofanya Mgombea
wetu ni jambo sahihi na barabara kabisa na lazima afanye hivyo.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Niliwaambia nchi yetu inahitaji mawazo mapya na mwelekeo
mpya ulio tofauti na uongozi wangu. Niliwambia kuwa tuliporuhusu jambo
hilo kufanyika, nchi yetu itabakia pale pale ambako nimeifikisha mimi.
Haya yatakuwa na makosa makubwa kwa sababu nchi yetu lazima isonge mbele
kwa mawazo mapya, kwa uongozi mpya na kwa staili mpya ya uongozi. Na
haya ndiyo anayasema Mgombea wetu.
Vinginevyo
ni jambo lisilokuwa na maana kubadilisha uongozi kama hatuko tayari
kukubali kuwa kila kiongozi lazima awe na staili yake ya uongozi na
namna yake ya kuongoza na kuendesha nchi yetu.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

No comments:
Post a Comment