Na: Lilian Lundo - MAELEZO
Tume iliyoundwa kwa ajili ya kuchunguza kifo cha Faru John imethibitisha
kuwa Faru huyo alikufa katika eneo la Sasakwa Grumeti kutokana na
kukosa matunzo, uangalizi wa karibu na matibabu alipoumwa.
Hayo
yamesemwa leo Jijini, Dar es Salaam na Mkemi Mkuu wa Serikali Prof.
Samwel Manyele alipokuwa akikabidhi ripoti ya uchunguzi wa Kifo cha Faru
huyo kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim
Majaliwa.
“Sampuli zilizochukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba ni mifupa ambayo
ilichukuliwa katika mzoga wa Faru John uliokutwa eneo la Sasakwa
Grumeti, Pembe zilizochukuliwa hifadhi ya Dar es Salaam na Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), damu kutoka maabara ya NCAA na
Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), ngozi kutoka kwenye mzoga na
kinyesi kilichokaushwa kutoka SUA,” alifafanua Prof. Manyele.
Aliendelea
kwa kusema kuwa matokeo ya uchunguzi wa awali yameonyesha damu, pembe,
mifupa na ngozi ni vya Faru John ambapo mpangilio wa vinasaba umeonyesho
kuwa Faru huyo ni mweusi (Black Rhinoceros) mwenye jinsia ya kiume.
Aidha vielelezo hivyo vilitumwa Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini ambapo timu ya wataalam kutoka Tanzania chini ya Mkemia Mkuu
wa Serikali walishiriki katika uchunguzi wa awali wa vinasaba na
kujadili matokeo kabla ya kuyatuma kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo
Matokeo yameonyesha sampuli na vielelezo vyote ni vya mnyama pori Faru
John.
Vile
vile amesema, uchunguzi umeonyesha kuwa sababu za kifo cha Faru huyo ni
kukosa matunzo, uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea
yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria pamoja na
mapungufu ya kiuongozi kwa Wizara, Hifadhi na Taasisi zake.
Baadhi
ya mapungufu yaliyobainishwa katika uchunguzi huo ni pamoja na
kutokuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha
kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti.
Prof. Manyele amesema kuwa hakukuwa na mkataba rasmi kati ya Serikali na mwekezaji unaoonyesha mnyama ametoka Serikalini kwenda kwa Mwekezaji.
Tume hiyo imeishauri Serikali kuchunguza viwanja
vya ndege ndani ya hifadhi vinavyomilikiwa na wawekezaji kutokana na
kuwepo na uwezekano wa viwanja hivyo kuwa njia ya majangili au matajiri kufanikiisha shughuli za ujangiri nchini.
Aidha
kutokana na mapungufu ya kiutendaji yaliyofanywa na Ofisi ya Mkurugenzi
wa Wanyamapori nchini (kutokutoa kibali rasmi) na mapungufu ya
kiuongozi yaliyofanywa na Mhifadhi wa NCAA kuruhusu Faru John kuondolewa
bila kibali, Tume inashauri hatua za kiutawala zichukuliwe dhidi ya
wahusika.
Kwa
upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza timu hiyo kwa kazi
nzuri waliyoifanya. Ameahidi kufanyia kazi maoni ya tume hiyo na
kutolea maelezo ya hatua zitakazochukuliwa na Serikali muda mfupi ujayo.
Tume
ya uchunguzi ya kifo cha Faru John iliundwa baada ya Waziri Mkuu
kufanya ziara ya kikazi Ngorongoro Disemba 6, 2016, ambapo alibaini
kuhamishwa kinyemela kwa faru huyo na kudaiwa kupelekwa Grumeti.
Waziri
Mkuu alitaka ukweli kuhusu upotevu wa Faru huyo na kuamua kuunda tume
hiyo ili kubaini ukweli wa Faru huyo kama alikufa au alitoroshwa.
No comments:
Post a Comment