Taarifa
ya Pamoja kwa Vyombo vya Habari
11 Desemba, 2017
SERIKALI NA UMOJA WA MATAIFA ZAUNGANA NA MRADI WA DUNIA WA XPRIZE ILI KUWAPATIA
WATOTO 2,400 ZANA YA KITEKNOLOJIA YA ELIMU
WILAYA YA MUHEZA, TANGA, TANZANIA – Katika sherehe
zilizofanyika katika kijiji kimoja huko mkoani Tanga, Shirika la Umoja wa
Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la
Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) yaligawa tableti zilizowekewa mfumo wa
elimu kwa watoto. Tableti hizo ziligawiwa kama sehemu ya mradi wa majaribio wa
miezi 15 chini ya Global Learning XPRIZE, ambao ni mradi wa miaka
mitano uliotokana na mashindano duniani yenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 15. Mradi huu wa dunia unatoa changamoto kwa timu za wabunifu kubuni na
kuandaa zana-wazi za kiteknolojia ili kuwawezesha watoto walio na fursa ndogo
ya kupata elimu katika umri wa miaka tisa hadi kumi na mmoja, kujifunza wenyewe
stadi za msingi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Kama sehemu ya
majaribio, zaidi ya watoto 2,400 kutoka katika vijiji 167 katika wilaya za Handeni,
Korogwe, Lushoto, Mkinga, Muheza, na Pangani watapewa tableti mpya ya aina ya Google
Pixel C, zilizotolewa kwa hisani ya Google. Tableti hizo zimewekewa mifumo ya
elimu kutoka kwa washindi watano wa mwisho wa Global Learning XPRIZE. Washindi
hawa walichaguliwa kutoka katika timu 198 na paneli ya majaji 11 wa kujitegemea
na walio wataalamu na kutangazwa mwezi September, 2017 wakati wa wiki ya Baraza
Kuu la Umoja wa Mataifa.
“Teknolojia hii
inayowawezesha watoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu pasipo msaada wa
mwalimu, ni ubunifu wa kiwango cha juu kabisa,” alisema Mayasa Hashim ambaye ni
Afisa Elimu Mkoa wa Tanga. “Msaada huu utaleta matokeo mazuri katika kuwakomboa
watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ili kwamba na wao wajifunze stadi
hizi.”
Tableti hizo
ziligawiwa na WFP kwa sababu shirika hili linasimamia uendeshaji wa kitengo cha
lojistiki na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) cha majaribio katika
mazingira halisi. Jukumu lake ni pamoja na kuingiza zana hiyo ya kiteknolojia
katika tableti, kuanzisha vituo vya kuwekea umeme unaotokana na jua kwenye
tableti hizo vijijini na kusimamia matengenezo, marekebisho na kutoa tableti
mpya katika kipindi chote cha majaribio ya ugani.
“Ubunifu katika
teknolojia unaweza kuwa jibu kwa baadhi ya changamoto kuu duniani,” alisema
Mwakilishi wa Nchi wa Shirika la WFP Tanzania Michael Dunford. “Majaribio haya
yanamaanisha kwamba tunaweza kutumia teknolojia mpya ili iwahudumie watoto
wasio katika mfumo rasmi wa elimu pamoja na watu wengine walio hatarini—na
hivyo kuhamasisha uletaji wa maendeleo zaidi katika mchakato huo. Ubunifu wa
aina hii unafungulia milango kwa Serikali, mashirika na biashara kuendeleza
katika modeli ambazo zimekwishajaribiwa tayari na kuvunja mwiko wa ukomo katika
yale tuliyodhani ndiyo pekee yanawezekana, na si tu katika sekta ya elimu bali
pia katika maeneo mengine ya maendeleo ya watu.”
Upande wa elimu katika majaribio ya ugani unasimamiwa na UNESCO kwa kushirikiana
na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Vilevile, UNESCO ina wajibu wa kusimamia maendeleo ya watoto katika Kusoma, Kuandika na
Kuhesabu ili kuweza kupima ni zana ya mshindi yupi wa mwisho ilileta matokeo
bora zaidi.
“Mradi huu unaendana na majukumu ya UNESCO katika kuhamasisha elimu jumuishi, itolewayo kwa usawa wenye haki na iliyo bora, na wakati huohuo kuchangia kwa kiasi kikubwa katiak juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali wa elimu nchini Tanzania katika kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wale wa jamii za pembezoni na zilizo nyonge, kupata fursa sawa katika elimu,” alisema Msimamizi wa UNESCO Faith Shayo. “Mradi huu unawapa watoto ambao hawakuwahi kujiunga na shule ya msingi pasipo sababu fursa nyingine, huku lengo kuu la kuwapa fursa ya kuingia au kuingia upya katika mfumo rasmi wa elimu ni baada ya kukamilika kwake. Hii inaonyesha juhudi kubwa za pamoja kati ya Umoja wa Mataifa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha viwango vya kujua kusoma na kuandika miongoni mwa vijana wa kizazi kipya nchini kwa kutumia teknolojia zinazotokana na ubunifu, zinazoweza kusambazwa kwa wingi na zenye gharama nafuu. Mradi huu unaweza kupanuliwa na hatimaye kuenewa katika mikoa yote ya Tanzania, ili kuendeleza ujifunzaji katika elimu ya awali.”
Mwisho wa awamu
ya majaribio ya ugani, timu ya washindi wa mwisho ambao masuluhisho waliyotoa yana
tija zaidi watapata zawadi kubwa ya Dola za Marekani milioni 10. Mshindi
atatangazwa mwezi Aprili, 2019. Kufuatia mashindano, kila washindi wa mwisho
watano wataweka huru zana zao na maudhui yake ili zipatikane bure na kwa yeyote
mwingine kuona namna ya kuzipanua. Inatarajiwa kwamba njia hii ya kujifunza
mwenyewe itawaongoza kujifunza na hatimaye kuwawezesha watoto kote nchini
Tanzania kuwa na umiliki zaidi wa elimu yao.
Sherehe itafanyika mapema mwaka 2018 ili kuadhimisha
kuanza kwa majaribio haya ya ugani. Sherehe hizo zitaandaliwa kwa kushrikiana
na Serikali ya Tanzania, UNESCO, WFP na Global Learning XPRIZE.
###
WFP ndiyo
shirika kubwa zaidi duniani la kiutu linalopambana na njaa kote duniani,
likitoa msaada wa chakula katika maeneo yenye dharura na likishirikiana na
jamii ili kuimarisha lishe na kujenga uwezo wa kujinusuru. Kila mwaka, WFP
hutoa msaada kwa takribani watu milioni 80 katika nchi 80.
UNESCO
ni shirika lenye wajibu wa kuratibu ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya
elimu, sayansi, utamaduni na mawasiliano. Linaimarisha uhusiano kati ya mataifa
na jamii na kuhimiza umma mzima ili kwamba kila mtoto na raia apate elimu. UNESCO
ina ofisi katika nchi 54 katika mabara yote.
Tufuatilie katika Twita:
Mpango wa Chakula Duniani: @wfp_tanzania,
@wfp_africa and @wfp_media
UNESCO: @unescodar
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Fizza Moloo, WFP/Tanzania, Simu. +255 (0) 784 720 022
or +255 (0) 759 686 543
Faith Shayo, Ofisi ya UNESCO
Dar es Salaam, Simu +255
(22) 29 15 400
Eric Desatnik /
Jackie Wei, eric@xprize.org / jackie.wei@xprize.org
No comments:
Post a Comment